Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema!
Mpendwa mwanatafakari, unayeitegea sikio Radio Vatican, kwanza ninakutakieni heri
na baraka tele za kuzaliwa Mwana wa Mungu. Leo ni Krismas, ni Noeli, ni neema ya Mungu
iliyofunuliwa kwetu.
Kwa hakika
ile ahadi ya Mungu aliyoitoa tangu zamani sasa imefunuliwa na hivi tunafurahi na kushangilia
tukiimba utukufu kwa Mungu juu na amani duniani kwa watu wenye mapenzi mema. Mtoto
Emanueli aliye na uweza wa kifalme mabegani mwake, Mungu pamoja nasi amezaliwa kwa
ajili yetu. Kanisa duniani kote linaimba “Pangoni Batlehemu amezaliwa Mtoto Yesu,
twendeni sote tukamwone na kumpa zawadi”
Nabii Isaya anayeishi karne ya nane
kabla ya Kristo, anaonesha katika masomo ya sherehe za Noeli jinsi Waisraeli wanavyofurahi
kurudi nyumbani toka utumwani Babeli. Wanafurahi kwa sababu wamekaa chini ya kandamizo
la utumwa kwa muda mrefu, na kandamizo hilo lilikuja kwa sababu wao wenyewe walishindwa
kutii mausia ya Mungu wakaingia katika ugomvi kati yao na hivi wakapelekwa utumwani.
Sasa Nabii Isaya akiona mwisho wa utumwa huo katika maono anaimba akisema “watu wote
waliokwenda katika giza wameiona nuru kuu na wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa
mauti nuru imewaangaza”
Uaguzi huu wa Nabii Isaya unakamilika kwa kuzaliwa
Masiha, Mwana wa Mungu, aliye mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele
na mfalme wa amani. Enzi yake haina mwisho, atahukumu kwa haki. Na kwa hakika hakuna
mfalme mwingine kabla na baada yake aliyeweza kuwa na sifa hizi.
Katika nyakati
zetu nasi tuko utumwani, tuko katika taabu mbalimbali kama vile ukosefu wa mahali
pazuri pa kuishi, shida ya umeme, maji, sukari, rushwa na ugomvi kati yetu, pamoja
na ajali barabarani. Je haya amesababisha nani? Ni sisi wenyewe. Sasa leo Nuru imetushukia
kutoka mbinguni kama tulivyokuwa tukiimba wakati wa majilio “ushukie Masiha kuwakoa
watumwao” Je kuzaliwa kwa Bwana au kushuka kwa Nuru hii kwatufanya kweli tuonje lile
pendo la kweli walilolionja Waisraeli toka utumwani Babeli? Ewe mpendwa, Mwana wa
Mungu ni Emanueli anakuja kutuondolea utumwa cha msingi tuaanze pamoja naye kuacha
ubaya na kutenda wema.
Kuacha ubaya na kutenda wema ni ujumbe kamambe ambao
Mtume Paulo anamtumia Mtakatifu Tito akimsistizia kuwa Neema ya Mungu Mwokozi inayookoa
wanadamu wote imefunuliwa kwetu na hvi kazi yetu kama twataka kuifaidi neema hiyo
ni kuambatana na maisha ya uongofu, maisha ya kupokea na kuzitumia neema za Mungu
pamoja nasi yaani Emanueli. Kuzaliwa kwa Kristu ni amani na uhuru kwa wana wa Mungu.
Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu ni ufunuo mkamilifu wa Mungu kwetu kwa maana tangu zamani
Mungu alisema nasi kwa njia ya mababu, manabii na sasa anasema nasi kwa njia ya Masiha,
Mwanae mpenzi tunaye paswa kumfuata.
Mpendwa Mwana Noeli, Mwinjili Luka akitupeni
habari ya furaha, kwanza anamweka Bwana katika mazingira ya mwanadamu. Anaweka mbele
yetu kwanza jambo la kijiografia na la kihistoria, akisimulia juu ya Masiha anayezaliwa
wakati wa mfalme wa Kirumi Kaisari Augusto, pia anazaliwa Betlehem kijiji cha wachungaji
kama ilivyokuwa imeaguliwa kwamba atazaliwa katika ukoo wa Daudi. Hili laonesha kuwa
Masiha anaingia katika maisha ya mwandamu. Pamoja na hilo pale pangoni Betlehemu anashuhudiwa
na wachungaji kielelezo cha upendo wa Mungu kwa wote na hasa walio fukara na maskini,
na kwa jinsi hiyo Mungu atufundisha kushinda uovu si kwa vita bali kwa upendo na
msamaha.
Wote twatambua kuwa wachungaji wakati ule walikuwa ni watu wa kulala
machungani, waliodharauliwa na hata hawakuruhusiwa kuingia kwenye masinagogi, walikuwa
wakisadikika kuwa waongo na wagomvi. Mwana wa Mungu anaona hao ndio wapewe habari
ya kuzaliwa kwake wakiwa wa kwanza. Maana yake Mungu ni kwa ajili yao na anachagua
kukaa katikati yao yaani walio maskini.
Mwinjili Yohane anaweka mbele ya mataifa
Neno wa Mungu aliyefanyika Mwili na akakaa kwetu. Masiha ni Neno wa Mungu ambaye anatumwa
na Mungu kwetu kwa sababu ya upendo upeo. Ni nuru ileile ambayo Nabii Isaya anaitanganza
katika Agano la kale ya kwamba miisho yote ya dunia imeiona nuru na wokovu wa Mungu.
Mungu
amefanyika mwili nasi tukauona wokovu wake na hivi tunaalikwa kusikiliza na kutenda
kadiri ya mapenzi yake. Mwinjili Yohane anatupatia fumbo la umwilisho kielelezo wazi
cha upendo wa Mungu, Mungu anayejishusha na kutwaa mwili wako dhaifu! Anataka kugeuza
mwili wako uwe mwili wa utukufu. Kwa fumbo hili la Bwana kukaa kwetu ni fundisho la
amani kwa mataifa, kumbe kugombana tishio dhidi ya upendo katika jamii uliowekwa kwa
njia ya fumbo la umwilisho. Yafaa kufikiri kidogo juu ya vita vinavyoendelea duniani.
Kumbe Neno akafanyika mwili ni nuru na amani kwa watu wote. Ni sura na utukufu wa
Mungu Baba na kielelezo cha mapendo yasiyopimika kwa Mwanadamu.
Ninakukumbusha
kwamba, Bwana amekuja na kukaa kwetu, maana yake anakaa kwenye familia kumbe ni sherehe
ya familia ni siku za kukaa pamoja Baba mama na watoto. Na kama vile ambavyo mtoto
anapozaliwa tunapeleka habari ya furaha kwa majirani basi kukaa kwetu pamoja na Bwana
katika familia kuwe ni chimbuko la habari njema ya furaha kama Wachungaji walivyopeleka
habari njema ya furaha kwa watu wote.
Kumbuka kule Betlehemu Bwana alikosa
nafasi katika nyumba ya wageni na hivi asije akakosa nafasi katika moyo wako katika
sherehe hizi za Noel na daima. Nafasi ya Bwana yapaswa kutayarishwa daima kwa maisha
ya sala na sakramenti. Kuna desturi ya kubatiza watoto katika sikukuu ya Noeli, yafaa
kuelewa kuwa ni nafasi muhimu na ya pekee inayotayarisha mahali Bwana atakapokaa katika
mtoto huyo, kumbe wazazi itunzeni nafasi iletwayo kwetu kwa njia ya ubatizo. Ninakutakieni
heri na baraka tele za Mungu leo na daima.
Tumsifu Yesu Kristu na Maria Tafakari
hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.