2010-04-02 12:04:01

Tafakari ya Maneno Saba ya Yesu Msalabani


Mheshimiwa Padre Leonard Maliva kutoka Jimbo Katoliki la Iringa, mwanafunzi mtaalamu wa Maandiko Matakatifu, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, katika Sikuu hii Mama Kanisa anapotafakari mateso na kifo cha Kristo Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu, anatushirikisha tafakari ya kina kuhusu maneno saba ya Yesu akiwa juu Msalabani. Huu ni utajiri mkubwa unaotuonjesha huruma na upendo wa Kristo kwa ajili ya wadhambi.

YESU MSALABANI

Wakati huo huo wanyang’anyi wawili wakasulibiwa pamoja naye, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto. Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisatikisa vichwa vyao, wakisema, “Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako! Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani.” Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, “Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe. Yeye ni mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani, nasi tukamwamini. Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka. Kwa maana alisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu.’” Pia wale wanyang’anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vilevile.


Mathayo 27:38-44


Sehemu hii ya Injili ya Matayo inatuthibitishia kuwa, Yesu akiwa msalabani, kuna watu ambao walimwambia maneno ya kumdhihaki. Sambamba na Injili ya Matayo, pia Injili za Marko, Luka na Yohane zinathibitisha maneno ya dhihaka dhidi ya Yesu pale msalabani. Lakini pia walikuwepo watu wengine ambao katika tukio hilo la kusulibiwa walimkubali Yesu kuwa ni mkombozi wao na ni mwana wa Mungu.

Tukio hilo la Yesu kusulibiwa msalabani linaweza kuwa ni chachu ya imani kwa wengi na pia linaweza kuwa ni kikwazo kwa wengine. Kama inavyoonesha katika maneno ya watu mbalimbali waliomwona Yesu akisulibiwa. Sisi hatukumuona Yesu pale msalabani; lakini habari zake tunazo. Habari hizo zimetugawa katika makundi mawili kama ilivyokuwa siku ile pale msalabani: tupo ambao tungependa kusikia kuwa Yesu alishuka msalabani na kwenda zake, pia tupo wale ambao tungependa kusikia kuwa watesi wake wanatubu na kumtambua Yesu kuwa ni mwana wa Mungu na Mkombozi. Siku ile pale msalabani wengi walimtaka Yesu ashuke msalabani na aende zake ili kuonesha nguvu na uweza wake. Ni wachache tu waliomtambua Yesu kuwa ni mwana wa Mungu anayewakomboa kwa njia hiyo ngumu ya mateso. Wewe na mimi tupo upande upi?


Maneno ya Watu mbalimbali kwa Yesu Msalabani








































Maneno ya DhihakaManeno ya Imani 
Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako. Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. 
Ukiwa ndiwe mwana wa Mungu, shuka msalabani.Ee Yesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. 
Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe.  
Yeye ni mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani, nasi tumwamini.  
Amemtegemea Mungu, na amwokoe sasa, kama anamtaka, kwa maana alisema mimi ni mwana wa Mungu.  
Tazama, anamwita Eliya.  
Acheni; na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha.  
Kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi, ujikoe mwenyewe.  
Je, wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.  


Mtume Paulo anatufundisha wewe na mimi tuwe upande wa wale waliomkiri Yesu kuwa na mwana wa Mungu na Mkombozi wao:
Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa kuwa imeandikwa: Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, na akili zao wenye akili nitazikataa. Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mleta hoja wa zamani hizi? Je, Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa upumbavu? Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuuzi wa lile neno linalohubiriwa. Kwa sababu wayahudi wanataka ishara, na wayunani wanatafuta hekima, bali sisi tunamhubiri Kristo aliyesulibiwa. Kwa wayahudi ni kikwazo, na kwa wayunani ni upuuzi, bali kwa waitwao, wayahudi kwa wayunani ni Kristo, nguvu ya Mungu na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu.
1 Wakorintho 1:18-25


Msalaba ni nguvu ya Mungu kwa kuwa Yesu ameutumia kama kiunganishi kati ya Mungu mwenye huruma na mwanadamu mwenye dhambi. Huruma ya Mungu na dhambi ya mwanadamu vinapokutana hutokea ukombozi (Huruma + Dhambi = ukombozi). Msalaba ni kama alama ya kujumlisha; miti miwili imekutana ikatengeneza msalaba. Mti mmoja ni huruma ya Mungu na mti mwingine ni dhambi ya mwanadamu. Tukumbuke kuwa dhambi ile ya awali nyakati za Adamu na Eva, ilianzia kwenye mti. Ndiyo maana ili kuiondoa hiyo dhambi, Yesu alichagua kutumia mti wa msalaba. Palepale ilipoanzia dhambi ndipo hapohapo pia Yesu ameiangamiza. Dhambi ya awali au ya asili ilianza pale watu wa kwanza walipodanganywa na shetani ili kumkataa Mungu. Shetani alitumia mti wa matunda kumwingiza mwanadamu kwenye dhambi:
Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, “Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, ‘Msile matunda ya miti yote ya bustani’?” Mwanamke akamwambia nyoka, “Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, ‘Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.” Nyoka akamwambia mwanamke, “Hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.
Mwanzo 3:1-7


Yesu naye alitumia mti wa msalaba kumtoa mwanadamu katika dhambi. Mti alioutumia shetani kumwingiza mwanadamu kwenye dhambi ulikuwa unavutia kwani ulikuwa na matunda. Kumbe mti alioutumia Yesu kumtoa mwanadamu kwenye dhambi unatisha kwani ni mzito na una mateso. Yesu msulibiwa ndiye tunda la mti wa msalaba ambalo halivutii ila linatisha na kukatisha tamaa.


Kwa hiyo, msalaba ni chombo ambacho Mungu amekitumia kama kielelezo cha umungu wa Yesu na ukombozi wake. Yesu, hata kama asingefundisha kitu chochote au asingefanya muujiza wowote, ingetosha tukio hilo la kusulibiwa msalabani kumtambulisha kuwa yeye ni mwana wa Mungu na Mkombozi. Ndiyo maana Kanisa linatufundisha na kutusisitiza kusali Njia ya Msalaba: EE BWANA YESU KRISTO TUNAKUABUDU NA TUNAKUSHUKURU; KWA KUWA UMEIKOMBOA DUNIA YOTE KWA MSALABA WAKO MTAKATIFU. Maneno hayo yanadhihirisha kuwa Kanisa linatambua kuwa, kazi ya Yesu msalabani ilikuwa ya ukombozi wetu. Maneno aliyoyasema Yesu pale msalabani ni Habari Njema ya Ukombozi. Ni maneno yanayojitosheleza kuwa ni mafundisho kwa wafuasi wake kwa nyakati zote. Ingetosha tu kuelewa vizuri maneno hayo na kuyaishi bila hata kusoma maneno mengine katika Biblia.
Maneno Saba ya Yesu Msalabani








































 Maneno ya YesuInjili
1Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo Luka 23:34
2Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami mbinguni. Luka 23:43
3Mama Tazama mwanao; Tazama mama yako. Yohane 19:26-27
4Eloi, Eloi lama sabakthani? Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Marko 19:34
5Naona kiu. Yohane 19:28
6Imekwisha (Yametimia) Yohane 19:30
7Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu. Luka 23:46

Namba saba, kama ilivyo namba arobaini katika desturi za Kiyahudi ina maana ya utimilifu au ukamilifu. Namba saba inathibitisha kuwa kitu ni kamili au kinajitosheleza. Tutafakari kwa pamoja maneno saba ya Yesu msalabani:


(i) “Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo”


Na walipofika mahali paitwapo Fuvu la Kichwa, ndipo walipomsulibisha yeye, na wale wahalifu, mmoja upande wa kuume, na mmoja upande wa kushoto. Yesu akasema, “Baba, uwasamehe, kwa hawajui watendalo.” Wakagawana mavazi yake, wakapiga kura.
Luka 23:33-34




Neno la kwanza la Yesu msalabani lahusu msamaha. Msamaha ni tabia kuu ya Mungu. Mtakatifu Agustino anasema kuwa, kama Mungu hangekuwa na huruma ingekuwa vigumu sana kwetu kuamini kuwa yeye ni Mungu. Ukuu wa Mungu haupo tu katika kazi kubwa na ajabu ya uumbaji, bali pia ukuu wake upo katika tabia yake ya kusamehe.

Neno la kwanza la Yesu msalabani ni habari njema ya wokovu. Inatosha neno hilo moja la msamaha kumtambua Yesu kuwa ni mkombozi. Na kama Yesu hangalisema neno hilo, labda sisi leo tungetia shaka kuwa yeye ni mwana wa Mungu mkombozi. Kazi yote ya kuhubiri na kufanya miujiza ilikuwa inahusu msamaha. Msamaha ndiyo hasa ujumbe mkuu wa mafundisho yote na miujiza yote ya Yesu. Mafundisho yote ya Yesu yalimwelekeza Mungu kuwa ni Baba mwenye huruma, mafundisho hayo yalimwelekeza mwanadamu atumie vizuri tabia hiyo kuu ya Mungu kwa kuomba msamaha. Miujiza yote ya Yesu ilihusu msamaha wa dhambi; ndiyo maana wengi ambao aliwafanyia miujiza aliwaambia, umesamehewa dhambi zako.

Neno la kwanza la Yesu msalabani linatufundisha kuwa jambo la kwanza kabisa kwetu sisi katika kuhusiana na Mungu ni kuomba msamaha. Ombi linaloweza kukubalika mbele ya Mungu ni kuomba msamaha wa dhambi zetu. Mara nyingi sisi mbele ya Mungu tunaomba mambo mengine ambayo tunaamini kuwa na mazuri na tunasahau kuomba jambo kuu kuliko yote mbele ya Mungu. Leo Yesu anatufundisha jinsi ya kuomba mbele ya Mungu.

Yesu anatuonea huruma sisi wanadamu anavyotuona tunatenda dhambi; ndiyo maana anasema hatujui tutendalo. Ni kweli kabisa! Tunapotenda dhambi hatujui tundendalo kwani sisi asili yetu ni Mungu; tuliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Tunapotenda dhambi tunaifuta sura na mfano wa Mungu ili tufanane na ibilisi. Mtoto anapochezea kiwembe hajui alitendalo, kwani kiwembe hakichezewi na mtoto; kitamkata na ataumia.

Lakini, Yesu anatufundisha pia kuwa nasi kati yetu yatupasa kuombana msamaha. Katika mafundisho yake anasema: Iweni na huruma kama Baba yenu wa mbinguni alivyo na huruma. Hata tunaposali, Yesu anatufundisha kuwa Mungu atatumia kipimo kilekile tunachotumia sisi kusameheana kati yetu: Utusamahe makosa yetu kama na sisi tunavyowasamehe wale waliotukosea. Yesu anatufundisha tusameheane siku zote, katika lolote na mara zote:
Kisha Petro akamwendea akamwambia, “Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe?” Hata mara saba? Yesu akamwambia, “Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini.”
Mathayo 18:21-22


Amri kuu ya Mungu ni upendo. Kielelezo kikuu cha upendo ni msamaha. Yesu ametufundisha kupendana, na yeye mwenyewe anakuwa mfano mzuri kwa kutangaza msamaha pale msalabani. Mkristo asiyejua kusamehe, huyu bado hajawa mkristo. Yesu anasema; mkipendana kati yenu, wote watajua kuwa ninyi ni wafuasi wangu. Kwa hiyo, kitambulisho cha ukristo ni upendo; kitambulisho cha upendo ni msamaha. Tena, Yesu katika mafundisho yake, anasisitiza tuwapenda hata maadui zetu na tuwaombee ili tuweze kuwa kweli wana wa Mungu.
“Mmesikia kwamba imenenwa: Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia: Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je, nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je, nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakauwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”
Matayo 5:43-48


Yesu ni mfano mzuri kwetu kwani pale msalabani anawasamehe adui zake wanaomsulibisha na anawaombea msamaha kwa Mungu. Hakika Yesu ni mwalimu halisi kwani kile alichofundisha kwa maneno, yeye mwenyewe ametekeleza kwa matendo.

Msamaha una pande mbili: kuomba msamaha na kutoa msamaha. Kati ya haya mawili ni lipi gumu zaidi?

Jiulize; wewe waweza kumsamehe mtu kwa lolote alilokufanyia?
Kumbuka: kutenda dhambi ni ubinadamu; kusamehe ni umungu.



(ii) “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami mbinguni”


Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana, akisema, “Je, wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi.” Lakini yule wa pili akamjibu, akamkemea, akisema, “Wewe humwogopi hata Mungu, nawe u katika hukumu iyo hiyo? Nayo ni haki kwetu sisi, kwa kuwa tunapokea malipo tuliyostahili kwa matendo yetu; bali huyu hakutenda lolote lisilofaa.” Kisha akasema, “EeYesu, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako.” Yesu akamwambia, “Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami mbinguni.”
Luka 23:39-43




Neno la pili la Yesu msalabani lathibitisha kuwa msamaha una nguvu kuliko dhambi. Yesu amefundisha juu ya msamaha kwa kuwaombea msamaha watesi wake. Yesu ameonesha kuwa yeye ni Mungu kwa kutumia tabia kuu ya Mungu ya kusamehe. Yule mhalifu ametambua kosa lake na amemtambua Yesu kuwa ni Mungu na akaomba msamaha; Yesu mara moja akamsamehe kwa kumpa nafasi mbinguni.

Leo hii utakuwa pamoja nami mbinguni: Neno hili ni habari njema ambayo kila mmoja wetu angefurahi kuambiwa na Yesu. Hapa Yesu anatufundisha kuwa, Mungu humpa msamaha papo kwa papo mtu yeyote anayeomba msamaha bila kujali amekosa nini. Ni dhambi kubwa kuishi na dhambi bila kuomba msamaha. Kutoomba msamaha kwa Mungu ni dharau kubwa. Yule mhalifu mwingine alimdharau Mungu na kumtaka amshushe msalabani; kumbe huyu mwingine alimwogopa Mungu na kuomba msamaha.

Katika neno la kwanza Yesu alifundisha kuwa jambo la kwanza mbele ya Mungu ni kuomba msamaha. Mhalifu wa kwanza hakuelewa mafundisho hayo, ndiyo maana badala ya kuomba msamaha akaomba muujiza wa kushushwa msalabani. Muujiza huo hakuupata kamwe. Kumbe yule mhalifu wa pili alielewa vema mafundisho ya Yesu; akaomba msamaha. Huyu alipata alichokiomba palepale bila kupewa ahadi; Leo hii utakuwa pamoja nami mbinguni.

Ukombozi ni msamaha wa dhambi zetu na kuingizwa mbinguni. Ukombozi ni tendo au jambo la leo na sio kesho. Ukombozi hautafutwi kesho na wala hauombwi kesho. Ukombozi daima ni leo; ndiyo maana Yesu anasema: Leo utakuwa pamoja nami mbinguni. Yesu hakusema, Ngoja kwanza nifufuke siku ya tatu nitakukaribisha mbinguni.

Neno LEO katika Injili ya Luka lina maana ya kufuta yaliyopita na kumwingiza mtu katika maisha mapya.


Kwa hiyo, neno LEO lina maana ya kufuta historia ya zamani ya dhambi na kumwingiza mtu katika historia mpya ya neema, yaani uwepo wa Mungu rohoni mwetu. Yesu anatualika mimi na wewe tuingie leo hii katika historia mpya. Katika ukombozi hakuna neno kesho; ukombozi ni leo.

Anza leo hii kuomba msamaha kwa Mungu. Anza leo kuomba msamaha kwa wote uliowakosea. Anza leo kuwasamehe wote waliokukusea. Leo hii, utakuwa mwana wa Mungu na mbinguni ndiko kutakuwa nyumbani kwako milele.

  (iii) “Mama tazama mwanao; Tazama mama yako”

Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene. Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, “Mama tazama mwanao.” Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama, mama yako.” Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.
Yohane 19:25-27




Neno la tatu la Yesu msalabani linahusu watu wawili; Maria, mama yake na Yohane, mwanafunzi na mtume wake. Yesu ana uhusiano mkubwa sana na mama yake kuliko mtu mwingine yeyote. Ni kawaida ya mila na desturi za watu mahali popote duniani kuwa mtu kuwa na uhusiano wa jirani sana na wazazi wake. Wazazi ndiyo waliomleta mtoto duniani, wanaomlea na kumfundisha katika hatua zake za kwanza za maisha. Mungu mwenyewe ametufundisha kuwa mzazi anachukua nafasi ya pili; nafasi ya kwanza ni Mungu. Katika amri 10 za Mungu; amri 3 za kwanza zahusu uhusiano wetu na Mungu, amri 7 zilizobaki zahusu uhusiano wetu. Katika hizo amri 7 zinazohusu uhusiano uhusiano wetu sisi wanadamu, amri ya kwanza (yaani ya nne) inahusu wazazi wetu: Waheshimu Baba na Mama upate miaka mingi na heri duniani.

Yesu akiwa msalabani anatukumbusha siri ya kuishi miaka mingi na kupata mafanikio duniani; siri hiyo ipo katika amri ya nne ya Mungu. Wazazi ndiyo miungu wetu hapa duniani; watu wote waliotuzidi umri ni wazazi wetu. Yesu alimheshimu na kumpenda sana mama yake na hata hapo msalabani anamkabidhi kwa mtume kijana zaidi ya mitume wengine.

Yesu alimfahamu vema mama yake kuwa ni mcha Mungu. Ni wazi kuwa Yesu alijifunza mambo mengi ya Mungu toka kwa mama yake. Kumlea mtoto ni moja kati ya kazi za mzazi; hivyo basi Maria na Yosefu ndiyo waliomfundisha Yesu habari za kwanza za Mungu. Yesu ni mwalimu na hapo chini ya msalaba anamkabidhi mwanafunzi wake Yohane mikononi mwa Bikira Maria. Yesu anataka kumwambia Yohane kuwa sasa Bikira Maria ndiye mwalimu wako. Sisi sote ni wanafunzi wa Yesu; Yesu ametukabidhi kwa mama Maria aendelee kuwa ni mwalimu wetu. Tunajifunza toka kwa Bikira Maria mambo mengi na hasa unyenyekevu.


Mtume Yohane analiwakirisha Kanisa pale chini ya msalaba. Yesu aliliasisi Kanisa baada ya kuiona imani ya mitume wake. Akalianzisha Kanisa na kulipa uweza wa kimungu wa kutangaza msamaha wa dhambi na kuiondoa dhambi: “Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za Ufalme wa Mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni, na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni”

Yesu anapomkabidha mama yake kwa Yohane na Yohane kwa mama yake; maana yake, anamkabidhi mama yake kwa kanisa, pia analikabidhi Kanisa kwa mama yake. Yesu anataka Kanisa lisitengane kamwe na mama yake. Wakristo ambao hawampe Mama Maria heshimu aliyopewa na Yesu pale msalabani, hao sio wafuasi wa Yesu. Kanisa linampa Mama Maria nafasi ya kwanza kabisa kati ya watakatifu kwani Yesu mwenyewe mwasisi wa Kanisa ndivyo alivyofanya.

Tendo la Yesu kumkabidhi mama yake kwa mtume Yohane pia linathibitisha kuwa Mama Maria hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu. Yesu alizaliwa peke yake kwa mama yake; yaani, Bikira Maria hakuwa na watoto wengine zaidi ya Yesu. Tukio la Yesu kusulibiwa msalabani ni tukio kubwa sana kwa Yesu na kwa ndugu zake. Kama Yesu angekuwa na wadogo zake wa tumbo moja, lazima siku ile, pale chini ya msalaba wangekuwepo. Kama angekuwa na wadogo zake asingemkabidhi mama yake kwa Yohane ambaye wala si ndugu yake; angelimkabidhi kwa wadogo zake wamtunze mama yao. Yesu alipokufa msalabani, ni Yosefu wa Arimateyo ndiye alienda kwa Pilato akaomba amzike Yesu. Kuzika mtu ilikuwa ni wajibu wa baba mzazi au ndugu wa tumbo moja; lakini Yesu alizikwa na Yosefu wa Arimateyo kwa kuwa baba yake mlishi Yosefu alishakufa zamani. Hii ina maana kuwa Yesu hakuwa na wadogo zake ambao ndiyo wangechukua nafasi ya baba mzazi aliyekufa.

Yesu alimkabidhi Yohane kwa mama yake ili mama huyo awe mwombezi wa kwanza wa Kanisa. Mama Maria ndiye mwombezi wetu kwani yeye ni mama yetu.

(iv) “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”

Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, “Eloi, Eloi, lama sabakthani?” maana yake, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?” Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, “Tazama, anamwita Eliya”.
Marko 15:33-35




Neno la nne la Yesu msalabani lahusi kilio chake kwa Baba yake. Kilio hicho kina ladha ya kukata tamaa. Je, ni kweli kuwa Yesu aliachwa na Baba yake? Je, ni kweli kuwa Yesu alikata tamaa? Kilio cha Yesu msalabani hakikuwa ni kilio cha kuachwa na Baba yake; wala hakikuwa ni kilio cha kukata tamaa.

Yesu pale msalabani alikuwa anasali Zaburi ya 22. Zaburi hii ilitungwa na mfalme Daudi na akaiita ni zaburi ya mateso na matumaini ya mwadilifu. Katika zaburi hii ukisoma utaona kuwa mtu huyo anaanza kumuuliza Mungu kwa nini amemwacha, kisha anaanza kuelezea sifa za Mungu. Halafu ndiyo anaanza kumweleza Mungu wake mateso yake, lakini katika hayo mateso anamwambia Mungu kuwa yeye ni tegemeo na tumaini lake. Na mwisho anamhakikishia Mungu kuwa hata katika mateso yake ataendelea kumsifu na kumtukuza Mungu mbele za watu wote.

Tukumbuke kuwa, wayahudi walizijua zaburi zote kwa kichwa; hawakuwa na vitabu vya kutosha. Kujifunza kwa kichwa ilikuwa ndiyo namna ya kawaida kuweza kueleaw vitu. Hawa wayahudi walikuwa wanasali daima, na zaburi ndizo zilikuwa sala zao. Kila mwaka wakati wa Pasaka wayahudi waliokuwa mbali na Yerusalemu walikuwa wanakwenda huko kuhiji. Nyakati hizo hakukuwa na magari; hivyo basi walitembea kwa miguu au kupanda punda, na safari ilikuwa ya siku kadhaa. Wakiwa njiani walisali zaburi wanapotembea. Na kwa kuwa walikuwa wanazijua zaburi zote 150 kwa kichwa; ilitosha ukitaja maneno ya kwanza ya zaburi kuwa umesali zaburi yote. Ndivyo Yesu alivyofanya pale msalabani; alisema tu maneno ya kwanza ya zaburi ya 22 Mungu wangu, Mungu wangu mbona umeniacha? Hii ilikuwa ni sala ya Yesu pale msalabani. Baadae ukaisome zaburi ya 22 utaelewa kuwa si zaburi ya mtu aliyekata tamaa bali ni sala nzuri yenye matumaini makubwa katika mateso.

Yesu hapo anatufundisha kuwa katika mateso tusikate tamaa bali tumkimbilie Mungu. Sisi kwa kawaida kwenye matatizo twaenda kwa waganga wa kienyeji na wachawi kwani tunadhani Mungu ametuacha na kutusahau. Kumbe, wakati wa matatizo ndiyo hasa wakati muafaka wa kusali zaidi na kumkimbilia Mungu.



(v) “Naona kiu”

Baada ya hayo Yesu, hali akijua ya kuwa yote yamekwisha kumalizika ili andiko litimizwe, akasema, “Naona kiu.” Kulikuwa huko chombo kimejaa siki; basi wakatia sifongo iliyojaa siki juu ya ufito wa hisopo, wakampelekea kinywani.
Yohane 19:28-29




Neno la tano la Yesu msalabani lahusu hitaji la msingi la uhai wa watu; maji. Hapa kiu ya maji inawakilisha njaa. Kati ya majanga makubwa kwa wanadamu ni njaa, kukiwa njaa basi kifo kimeshafika, tena ni kifo cha taratibu kwa mateso makubwa. Yesu ametumia neno kiu na sio njaa kwa kuwa kiu huuma zaidi kuliko njaa. Ni kweli kuwa njaa ya chakula na kiu ya maji huenda pamoja, lakini kiu ya maji inatesa zaidi kuliko njaa ya chakula. Mwanadamu bila chakula na kinywaji hakika hawezi kuishi bali atakufa. Chakula na kinywaji ni hitaji la lazima katika maisha.

Kiu aliyonayo Yesu pale msalabani haikuwa ya kinywaji; ilikuwa ni kiu ya kuona kuwa kazi aliyoianzisha inaendelezwa. Yesu alikuja duniani kutangaza msamaha wa dhambi; hivyo basi ni kiu yake kubwa kuona kwa watu wanamuelewa na wanaomba msamaha wa dhambi zao kwa Mungu. Mafundisho yote ya Yesu na miujiza yake yote inajikita kwenye msamaha wa dhambi. Kanisa lake alilianzisha ili lifanye kazi hiyo ya kusamehe na kuondoa dhambi: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa”.

Ni kiu ya Yesu kuona kuwa, mimi na wewe tunaungama na tunatubu dhambi zetu. Kuungama dhambi zetu ni kielelezo cha kuthamini kazi ya Yesu msalabani. Kuungama dhambi zetu ni kumpa Yesu maji ili akate kiu yake pale msalabani. Kuishi na dhambi bila kuungama ni sawa na kumpa Yesu siki badala ya maji pale msalabani katika kiu yake: wakanipa uchungu kuwa chakula changu, nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki. Siki ni divai iliyopoteza radhi yake na hivyo huongeza maumivu kwa mtu mwenye kiu ya maji.



(vi) “Imekwisha/ Yametimia”

Basi Yesu alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, “Imekwisha”. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake.
Yohane 19:30




Neno la sita la Yesu msalabani lina uhusiano mkubwa na neno la sita; au ni mwendelezo wake. Ni neno linalohusu kiu. Ajabu ni kwamba Yesu alipopewa ile siki ili ainywe, hakuinywa bali akasema kuwa kiu yake imekwisha. Hapa ndipo twatambua kuwa Yesu hakuwa na kiu ya maji kama kinywaji, bali alikuwa na kiu ya kuona wanafunzi wake au wafuasi wake wanabadilika. Mabadiliko anayoyaleta Yesu ni toba. Toba ni tendo la mtu kutafuta rehema au huruma ya Mungu. Katika Agano la Kale watu walipotaka kumpendeza Mungu walimtolea sadaka. Kumbe katika Agano Jipya Yesu anatuambia kuwa Mungu hataki tena sadaka bali anataka rehema. Rehema ni tendo lenye pande mbili; upande mmoja ni mtu kutambua dhambi zake na kuziungama, upande mwingine ni Mungu kumsamehe mkosefu aliyezitambua na kuzijuta dhambi zake.

Yesu anaposema kuwa kiu yake imekwisha anataka kuonesha kuwa kiu yake haitulizwi kwa siki. Siki ni divai iliyoisha nguvu ambayo hutumika kuua wadudu na pia hutumika kuwatesea wahalifu ili kuwaongezea maumivu kwenye makovu yao. Wale watesi wa Yesu walimpa siki sio kwa lengo la kutuliza kiu bali kwa lengo la kumtesa zaidi. Siki hata siku moja haitulizi kiu ya mtu wala kiu ya mnyama.

Yesu daima anaona kiu, na anatuambia wewe na mimi kuwa anaona kiu. Je, tumpe siki au maji. Kila tunapozitambua dhambi zetu na kuomba msamaha kwa Mungu na kwa wale tuliowakosea tunakuwa tunampa Yesu maji ili kiu yake iishe. Lakini tunapoishi na dhambi zetu bila kuungama na kuomba msamaha, basi sisi tunampa Yesu siki ili aendelee kuteseka zaidi. Yesu anatarajia kuwa tutampa maji na sio siki. Sisi wafuasi wake yatupasa kumpa Yesu maji ili asione kiu tena. Kubadilisha maisha yetu ni zawadi kubwa sana tunayoweza kumpa Yesu katika mateso yake. Je, wewe bado unampa Yesu siki?

Kiu ya Yesu ni kutubadilisha. Kumbuka alipomwambia yule mwanamke msamaria pale kisimani: Nipe maji ninywe. Yesu alikuwa na njaa na kiu akawatuma wanafunzi wake waende mjini kutafuta chakula, lakini walipomletea chakula aliwaambia: chakula changu ndicho hiki: niyafanye mapenzi ya Baba aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake. Yesu alipomfundisha yule mwanamke na kumfanya atubu dhambi zake, Yesu hakuona njaa tena; maana njaa yake ilikuwa ni kumuokoa yule mwanamke. Kumbe kiu na njaa ya Yesu ni kufanya mapenzi ya Mungu. Neno mapenzi ya Mungu lina maana ya kile anachokitaka Mungu. Anachokitaka Mungu ni kumuona mwanadamu anaujua ukweli, anatubu dhambi zake na kuingia mbinguni.



(vii) “Ee Baba mikononi mwako naiweka roho yake”

Hapo ilikuwa yapata saa sita, kukawa giza juu ya nchi yote hata saa kenda, jua limepungua nuru yake; pazia la hekalu likapasuka katikati. Yesu akalia kwa sauti kuu, akasema, “Ee Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha kusema hayo alikata roho.
Luka 23:44-47




Neno la saba na la mwisho la Yesu msalabani lahusu kifo. Kifo ni tukio la mwisho kwa mtu yeyote na ni tukio lisilokwepeka. Kila mtu ni lazima akutane na kifo; apende asipende, ajue asijue, kifo kipo na kinatungojea. Wakati ule adhabu ya msalaba ilikuwa na lengo la kumuua mtu; ilikuwa ni hukumu ya kifo. Hii ilikuwa ni adhabu ya Warumi. Kumbe kwa Wayahudi kutundikwa msalabani ilikuwa ni jambo paya zaidi ya kifo; ilikuwa ni kifo cha laana: kwani aliyetundikwa juu ya mti amelaaniwa na Mungu.

Kifo cha Yesu pale msalabani kilihesabika kuwa ni laani kadiri ya imani ya Wayahudi. Lakini kumbe Yesu kwa kufa msalabani aliigeuza hiyo imani yao ya kale na kuwaingiza katika imani mpya:
Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa: Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.
Wagalatia 3:13-14




Kumbe Yesu amekufa kwa ajili ya watu wa mataifa yote ili mapenzi ya Mungu ya kuwaalika watu wote mbinguni yatimie.

Yesu anapokufa msalabani kwa mateso makubwa anatukumbusha kuwa mwisho wa mateso yetu upo katika kifo chema. Kufa kwake msalabani kwa mateso lakini kwa kutamka maneno mazuri ya kuisalimisha roho yake kwa Mungu ni jambo kubwa kwetu kujifunza. Ni kweli kuwa siku moja lazima kila mmoja wetu atakufa; tuna uhakika wa kifo chetu kwa asilimia mia moja. Lakini, tutakufa vipi? Vizuri au vibaya?

Kufa vibaya ni kufa katika hali ya dhambi. anayekufa na dhambi anakuwa ameisalimisha roho yake mikononi mwa ibilisi. Kufa vizuri ni kufa katika hali ya neema, yaani kuisalimisha roho yako mikononi mwa Mungu. Tukumbuke kuwa Yesu alikufa msalabani ili kuushinda utawala wa ibilisi ulioleta dhambi na kifo. Kila tunapotenda dhambi tunakuwa tumekufa na kujiweka mikononi mwa ibilisi. Lakini, kila tunapoungama dhambi zetu tunakuwa tumefufuka pamoja na Yesu na kumshinda ibilisi. Kuungama dhambi zetu katika sakramenti ya kitubio ni matayarisho ya kifo chema.
Yesu kabla ya kufa alikumbuka kusali na kuiweka roho yake mikononi mwa Mungu. Yesu alisali zaburi ya mfalme Daudi ambayo ni sala ya kusali wakati wa majaribu: “Mikononi mwako naiweka roho yangu; umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli. Mimi na wewe, je, tutakumbuka kusali saa ya kufa kwetu na kujiweka mikononi mwa Mungu. Au kabla ya kufa tutaanza kukumbuka mambo yetu ya duniani na kusahau kuwa tupo mlangoni mwa mbinguni au motoni. Ukiwa na dhambi unapokaribia kufa unakuwa upo mlangoni mwa motoni; yakupasa usali na kuomba kitubio. Ukiwa na neema unapokaribia kufa upo mlangoni mwa mbinguni; yakupasa usali na kumshukuru Mungu.

Hitimisho
Maneno ya Yesu msalabani yanatosha kabisa kutufanya sisi leo hii tumkiri yeye kuwa ni mwana wa Mungu na mkombozi wetu. Yesu anamwalika kila mmoja wetu auchukue msalaba wake na kisha amfuate katika mafundisho yake: “Mtu yeyote asiyechukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.”




Ee, Bwana Yesu Kristo tunakuabudu na tunakushukuru:
Kwa kuwa, umeikomboa dunia yote kwa msalaba wako mtakatifu.








All the contents on this site are copyrighted ©.