2010-02-19 08:01:05

Siku arobaini za mfungo!


Tulianza hija ya kipindi cha Kwaresima kwa uchambuzi wa kina uliofanywa na Mheshimiwa Padre Alcuin Nyirenda, OSB, maana ya mfungo katika maisha ya kijamii na kidini. Leo anaendelea kutumegea maana ya namba arobaini katika maisha ya kijamii lakini zaidi katika maisha ya Kanisa, wakati huu wa Kwaresima, yaani, Siku arobaini za: Sala, Toba, Tafakari ya Neno la Mungu, Matendo ya Huruma.

Ninakualika, ujiunge sasa na Mheshimiwa Padre Nyirenda, uweze kujitajirisha na tafakari hii wakati huu wa Kwaresima, kwani ndio muda uliokubalika. RealAudioMP3

Hebu sasa tutafakari juu ya namba hii arobaini.Kwetu wakristo kanisa limetenga kipindi cha mfungo cha  siku 40 kabla ya kuliadhimisha Fumbo kuu la maisha, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo (Pasaka).

Namba hii arobaini inatajwa na kutumika pia katika mazingira mengine nje ya mfungo, na ina maana mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa dini. Mathalani ili kuonyesha kwamba kila tendo lina kikomo chake, kama tendo bovu la wizi, kuonyesha kuwa lina kikomo chake mswahili atakuambia “mwizi siku zake arobaini”. Kadhalika kuna mti ambao majani yake ni machungu sana, na unaaminika kutibu magonjwa arobaini, mti huo unaitwa mwarobaini.

Kutokana na uchachu wa majani yake mara nyingine neno hilo hutumika kumtaaridha mwovu kuwa atapata tiba inayochacha ya kuukomesha uovu wake, hapo mswahili atakuambia: “Nitakunywesha mwarobaini”. Kuna pia utamaduni uitwao “arobaini,” yaani siku ya arobaini baada ya kifo na maziko ya ndugu ambapo wafiwa hukutana na kufanya ukumbuko wa msiba kwa kusali na kupanda msalaba makaburini.

Katika Biblia tunaikuta namba 40 ikitajwa katika sehemu kadhaa za Agano la Kale na Agano Jipya. Mathalani, wayahudi walitangatanga na kuhamahama Jangwani kwa miaka 40 kabla ya kuingia nchi ya ahadi. Yaonekana kwa miaka arobaini taifa hili lilikuwa katika giza la uovu na kumchukiza Mungu Muumbaji wake. Hata mzaburi anasema: “Miaka arobaini nilichukizwa na kizazi hiki, nikasema: ‘Ni watu waliopotoka mioyo, wala hawakuzijua njia zangu.” (Zab. 95:10).

Katika nafasi nyingi za Agano la kale na jipya namba hii inahusiana na kufunga: Musa alifunga siku 40 kabla ya kupokea amri kumi za Mungu “Naye alikuwa huko pamoja na Bwana siku arobaini na masiku yake; hakula chakula, wala hakunywa maji. Naye akaandika katika hizo mbao hayo maneno ya maagano, hizo amri kumi.” (Kutoka 34:28). Nabii Eliya alifunga siku 40 kabla ya kuonana na Mungu kwenye mlima Orebu: “Akainuka, akala akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu mlima wa Mungu.(I Wafalme 19:8)

Katika Agano jipya, Yesu alifunga siku 40 (jangwani) akipambana na majaribu kabla ya kuanza kazi yake. Aidha baada ya kufufuka kwake, mitume walijifungia ndani ya chumba kwa siku 40 kwa ajili ya kuwaogopa Mayahudi.

Kwa mitume, kipindi hiki kilikuwa cha wasiwasi na woga. Hadi siku ya hamsini (Pentekoste) ndipo wakapata nguvu ya kutoka nje na kuanza kuhubiri bila woga hadi kufa kama mashahidi. Wataalamu wengi wa maisha ya kiroho, kitelojia na hata ya kisaikolojia wameinyambua namba hii 40 hadi kugusa maisha ya mtu binafsi na ya jamii. Wanaanza kwa kunukuu zaburi isemayo:“Jumla ya miaka yetu ndiyo sabini, tukiwa na afya njema, themanini” (Zab.90:10).

Kwa hiyo, kwa mwenye nguvu na afya njema nusu ya miaka hiyo 80 ni miaka 40 nayo huitwa kipindi cha umri wa kati wa binadamu. Wataalamu hao huitumia namba hiyo ya umri wa kati (miaka 40) kumaanisha mwisho wa sehemu ya kwanza ya maisha ya binadamu na mwanzo wa maisha mapya. Wameonyesha pia kwamba kwa binadamu, kipindi hicho ni cha matatizo na cha kukosa msimamo yaani “middle age crisis”. Ama kweli miaka arobaini ni katikati ya maisha, ni muda unapoisha ujana wa kwanza na kuanza ujana wa pili.

Ni kama katikati ya mchana (saa sita) yaani adhuhuri ya maisha yenye maradhi na hatari zake kama asemavyo mzaburi, “Hutaogopa tauni izungukayo gizani wala maradhi yaangamizayo adhuhuri” (Zab. 90:6) Kama ukali wa jua unavyoanza kufifia kuanzia adhuhuri kuelekea jioni, ndivyo maisha ya mtu baada ya kutimiza umri wa kati. Tunaweza basi kusema kwamba kitambo cha namba 40, hutumika katika nyanja nyingi za maisha, yawe ya kijamii, kidini na kibiblia.

Halafu kitambo hiki cha 40 chaweza kumaanisha giza, (uovu), taabu, wasiwasi, uzuzu, woga, kukosa msimamo au mwelekeo. Bahati iliyoko ni kwamba kipindi hiki ni cha mpito na si cha kudumu. Yaani, ni namba imaanishayo kikomo na mwanzo wa kitu kipya. Baada ya arobaini hufuata 50 (Pentekoste) kila kitu kinapodhihirika kilivyo, maisha yanapoonekana katika mwanga mpya, kwa vile inaanza ngwe mpya ya maisha.

Ni kipindi ambapo mtu unachukua uamuzi upya wa maisha, kama asemavyo mswahili: “Akachukua zake hamsini”. Licha ya kumaanisha kikomo, namba hiyo yaweza kuchukuliwa kuwa ni kipindi cha tafakari ya yaliyopita na kujiandaa kwa yajayo. Ndugu zangu, baada ya kulitafakari neno mfungo na namba hii arobaini, sasa itatuwia rahisi kutafakari kwa nini wakristu tufunge kwa siku arobani?

Awali ya yote, kwaresima ni kipindi cha kufunga kinachotangulia tukio kuu la kufufuka Bwana wetu Yesu Kristu. Kuanzia karne ya kwanza, kwa wakristu wenzetu wa kanisa la mwanzo, mfungo kabla ya Pasaka uliitwa Mfungo wa Pasaka (Easter Fasting).

Hadi karne ya tatu Mfungo huo ulikuwa unadumu kwa siku 3, 4 hadi 7 tu basi, ikiwa kama maandalizi ya karibu ya Pasaka yenyewe. Mtaguso wa Laodikea wa mwaka 360 BK (karne ya 4), ikaamriwa kwamba mfungo uwe kwa siku 40 ndiyo maana ya jina hili la kilatini kwaresma.

(Baadaye mfungo ukaendelezwa hadi kufikia siku hata 50, 60 hadi 70, ndiyo maana ya majina ya kilatini kama quinquagesma (50), sexagesma (60) na septuagesma (70).) Kwa wakristu wa kwanza kipindi hiki kilikuwa pia ni cha kuwaandaa makatekumeni (watu wazima) kwa ajili ya ubatizo utakaofanyika Jumamosi kuu.

Naam, hadi hapa tunafunga pazia kwa sehemu hii ya pili ya tafakari kuhusu maana ya namba arobaini katika uelewa wa maisha ya kawaida, lakini maana yake halisi mintarafu Maandiko Matakatifu na maisha ya Yesu kwa ujumla. Mheshimiwa Padre Alcuin Nyirenda, atajimwaga tenda ndani ya nyumba, akijitahidi sasa kuunganisha maana ya mfungo wa kwaresima unaofanyika kwa Siku arobaini. Tafadhali, usikose kubofya bofya kwenye ukurasa huu, ili kujitajirisha na Tafakari ya Neno la Mungu. Ukigundua siri ya utajiri huu, usikose kumshirikisha jirani yako.

 
 







All the contents on this site are copyrighted ©.