2018-07-21 08:41:00

Vipaumbele vya Kanisa kwa Mwaka 2018-2019: Vijana na familia


Mkutano mkuu wa tano wa Shirikisho la Baraza la Maaskofu wa Amerika ya kusini na Carrebean, CELAM, uliitishwa na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, na kufunguliwa rasmi na Baba Mtakatifu Benedicto XVI tarehe 13 Mei 2007, karibu na Madhabahu ya Bikira Maria wa Aparecida, nchini Brazil. Tema zilizopamba moto kipindi hicho ni utume wenye kujali zaidi maskini na wanyonge, Kanisa linalojikita katika jumuiya mahalia, Kuona, kuamua na kutenda, Uinjilishaji mpya, taalimungu ukombozi, na utume wa bara la Amerika kusini.

Mkutano huo ulichukua takribani siku 20, ambapo ulifungwa tarehe 31 Mei 2007, wakati Baba Mtakatifu Francisko, akiwa Kardinali na Askofu mkuu wa Buenos Aires, alishiriki kikamilifu katika majadiliano na aliwajibika kwa namna ya pekee sana katika kuongoza Sekretariat kuu ya kuandaa nyaraka ya mwisho ya mkutano huo, ambapo Padre Alexandre Awi Mello alikuwa mmoja wa makatibu wa Sekretariat hiyo. Mnamo tarehe 31 Mei 2017 Baba Mtakatifu Francisko alimteua  Padre Alexandre Awi Mello kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha.

Katika mahojiano na gazeti la Osservatore Romano, Padre Alexandre Awi Mello anasema, hakuwahi kudhania hata mara moja katika maisha yake, kwamba angekuja kufanya utume katika moja ya Ofisi za kipapa, na alipokea kwa kusita sana uteuzi huo. Katika utendaji wake, anaahidi kujitoa yeye kwa ufahamu, karama, weledi, uwezo, ubnifu alio nao, akijifahamu pia na madhaifu aliyo nayo ya kibinadamu. Katika utume, cha msingi zaidi ni utayari wa kumhudumia Kristo na Kanisa lake, ikiwa ni pamoja na Papa, Maaskofu, walei, familia, vyama vya kitume, na kwa namna ya pekee vijana, ambapo Kanisa hivi karibuni limeamua kuweka kipaumbele kwao.

Miaka hii miwili, yaani 2018 – 2019, itakuwa na matukio mawili makubwa yanayowahusu vijana: Sinodi ya maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayofanyika mjini Vatican mwezi Oktoba 2018, ikiongozwa na kauli mbiu, vijana, imani na mang’amuzi ya miito; halafu Maadhimisho ya Siku ya Vijana kimataifa, yatakayofanyika Panama mnamo mwezi Januari 2019, maadhimisho yenye vionjo vya Bikira Maria kwa kauli mbiu, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. (Lk. 1:38), ili kuendeleza ile nembo ya Kanisa kama mbeleko ya mama anayesikiliza na kulea vema wanae. Padre Alexandre Awi Mello anasema, hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kanisa, ambapo vijana wanapewa kipaumbele kikubwa kiasi hiki, ili kusikilizwa kwa uhuru na upendo, kusaidiwa na kupewa maelekezi sahihi, na kupewa nafasi ya kulishangaza kanisa na ulimwengu kwa uwezo, karama, vipaji na ubunifu walivyotunukiwa na Mwenyezi Mungu. Kwa sababu hiyo, inasikitisha sana kuona baadhi ya wachungaji makasisi hawachangamki katika utume huu wa vijana, na wakati mwingine wapo wanaowapotezea kabisa.

Vijana wa kizazi kipya wana changamoto nyingi, wamo kwenye hatari mbalimbali zinazosababishwa na mamboleo, utandawazi, na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Baadhi ya vijana wa leo wamekumbwa na matukio kadhaa ambayo yamewapiga mweleka wa kishindo na kuwaacha na vidonda, vilema na maumivu makubwa. Hatari zaidi ni wale wanaoelekea kujikatia tamaa. Iwapo Kanisa halitachangamka na kusimama kidete kwenye utume kwa vijana, dunia itapoteza mwelekeo na matumaini kwa vizazi vijavyo. Ndiyo sababu Baba Mtakatifu amelishikia kidedea suala hili la utume kwa vijana wa kizazi kipya. Padre Alexandre Awi Mello ni Padre mwenye asili ya kibrazil, na ni mmoja wa wanachama wa chama cha kipapa cha kitume, Schoenstatt, kilichoanzishwa mnamo mwaka 1914 na padre Joseph Kentenich kilicho na lengo la kupyaisha kiroho maisha ya wanadamu wa nyakati hizi, kwa maombezi na usimamizi wa Bikira Maria. Padre Mello katika maisha yake kwa asilimia kubwa amepangiwa utume kwa vijana. Malezi haya yote yanachangia matumaini ya watu wengi kwa nafasi aliyo nayo katika Baraza la kipapa la Walei, Familia na Maisha, na kwa namna ya pekee utume kwa vijana.

Na Padre Celestine

Vatican news!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.