2018-07-17 14:45:00

Shirika la Roho Mtakatifu linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 Tanzania


Roho Mtakatifu ni Nafsi ya tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ni Bwana mleta uzima; atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: Aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Shirika la Roho Mtakatifu, Sherehe ya Pentekoste 27 Mei 1703 likaanzishwa rasmi huko nchini Ufaransa na Padre Claude Poullart des Places. Hiki kilikuwa ni kikundi cha Waseminari waliojiaminisha na kujiweka wakfu chini ya ulinzi na tunza ya Roho Mtakatifu na kwa msaada wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili, kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili huduma kwa Kanisa, hususan katika maeneo na mazingira tete na hatarishi; bila kusahau uinjishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Shirika la Roho Mtakatifu Kanda ya Tanzania linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu kuanzishwa kwake. Itakumbukwa kwamba, familia ya Mungu nchini Tanzania inaadhimisha pia Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara kwa kuongozwa na kauli mbiu “Miaka 150 ya Uinjilishaji, Furaha ya Injili”. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara linahimiza roho na sadaka ya umisionari na kwamba, sasa ni zamu ya Wakristo Barani Afrika kuwa wamisionari kwa kuwasaidia wengine kukua kiroho, kuamsha imani, kutangaza na kushuhudia Injili.

Padre Joseph Shiyo kutoka Shirika la Roho Mtakatifu katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, Shirika lake, tarehe 18 Julai 2018 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 tangu lilipoingia Tanzania Bara na kwa sasa limeenea katika nchi 62 duniani. Ustawi, maendeleo na mafanikio ya Tanzania ni sehemu ya mchango mkubwa uliotolewa na Kanisa kwa njia ya wamisionari wake waliojisadaka bila ya kujibakiza na kwamba, Kanisa Katoliki Tanzania Bara ni matunda ya kazi ya Wamisionari wa Roho Mtakatifu waliofika mjini Bagamoyo kunako mwaka 1868 na kuanza mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu sanjari na harakati za kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo ya watanzania katika ujumla wao. Limechangia katika ujenzi wa miundo mbinu na hata wakati mwingine ujenzi wa barabara. Shirika la Roho Mtakatifu liliwekeza sana katika sekta ya elimu kwa kujenga vyuo vya elimu huko Mandaka na Singachini, Jimbo Katoliki la Moshi bila kusahau Chuo cha Ualimu Morogoro, kilichoko Jimbo Katoliki la Morogoro. Taasisi za elimu zilizokuwa zinaongozwa na kumilikiwa na Kanisa zilichangia sana hata katika mchakato wa kutafuta uhuru wa Tanganyika wakati huo. Zote hizi zilikuwa ni jitihada za ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika haki, umoja, udugu na upendo miongoni mwa watu wa Mataifa. Kanisa la Tanzania linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki, iwe ni fursa ya kukuza na kupyaisha ari, moyo, sadaka na majitoleo ya kimisionari, ili kuendeleza chachu ya ukombozi wa mtu mzima: kiroho na kimwili, na kuiwezesha Injili kusonga mbele kwa ari na kasi kubwa zaidi, ili watu waweze kutembea katika mwanga wa Injili kwa kushuhudia na kutangaza furaha ya Injili ya Kristo ndani na nje ya Tanzania.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.