2018-07-16 07:00:00

Papa Francisko asema, vijana ni chachu ya mageuzi ya familia!


Baraza la Maaskofu Katoliki Antilles kuanzia tarehe 10 -23 Julai 2018 linaendesha Kongamano la Vijana Kitaifa linalongozwa na kauli mbiu “Vijana chachu ya mageuzi ya familia ya Caribbean”. Hii ni sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya kuanzishwa kwa Utume wa Vijana nchini humo kunako mwaka 2015. Ni tukio linalowashirikisha vijana kuanzia umri wa miaka 16-35, lakini vijana kati ya umari wa miaka 16-18 walipaswa kupata kibali maalum kutoka kwa wazazi wao.

Maadhimisho haya yanaendelea kutimua vumbi katika Jimbo Katoliki la Martinique. Hiki ni kipindi cha sala, tafakari na Kuabudu Ekaristi Takatifu; Katekesi na majiundo makini; michezo na tamaduni. Nyaraka elekezi katika Kongamano la Vijana Kitaifa huko Antilles ni “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” ulioandikwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na  Wosia wa Kitume wa Mtakatifu Yohane Paulo II “Familiaris consortio” yaani “Utume wa familia ya Kikristo” alikazia na kusisitiza mpango wa Mungu katika kweli ya asili ya upendo wa kindoa na ya familia: mahali pekee pa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika upendo na umoja thabiti kati ya mume na mke. Anakumbusha kwamba, ndoa ni hitaji la ndani kabisa katika maisha ya binadamu linalojikita katika uaminifu na uhuru kamili kadiri ya mpango wa Mungu Muumbaji na Mkombozi dhidi ya unafsia  na mwono binafsi

Katekisimu ya Kanisa Katoliki hukusanya pamoja vipengele vya msingi vya mafundisho hayo: Agano la ndoa, ambalo kwalo mume na mke huunda kati yao jumuiya ya ndani ya uzima na mapendo, limeanzishwa na kupewa sheria zake na Muumba. Kwa maumbile yake limepangwa kwa ajili ya mema ya wanandoa, pia kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Kristo Bwana aliiinua ndoa baina ya wabatizwa katika hadhi ya Sakramenti [Rej. GS, 48; Sheria Kanuni ya Kanisa, 1055, 1]” (KKK 1660). Mtakatifu Yohane Paulo II ameutangazia ulimwengu ujumbe makini wa Ndoa na Familia inayopaswa kusherehekewa katika mwanga wa neema ya Mungu, kwa kuendelea kutangaza Injili ya Familia: Uzuri, ukuu na utakatifu wake hata kama itapingana na mawazo ya watu wa nyakati hizi.

Kanisa liwasindikize wanafamilia ili waweze kuwatangazia jirani zao ukweli na upendo wa maisha ya ndoa na familia unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya Familia ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa mahalia. Hii ni changamoto kwa Wakristo kujitosa kimasomaso kutangaza Injili ya familia inayojikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliowaandikia wajumbe wanaoshiriki katika Kongamano la Kitaifa la Vijana huko Carribean anawataka vijana kuonesha jeuri na uzuri wa ujana, kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia nguvu ya ujana wao kuleta mageuzi makubwa katika jamii kwa kupambana na hali na mazingira hatarishi dhidi ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya familia, kwa ajili ya leo na kesho iliyo bora zaidi, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, SURA YA NNE: Upendo ndani ya ndoa ndicho kiini cha Injili ya familia inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Baba Mtakatifu anaianza sura ya nne kwa utenzi wa upendo kati ya ndugu kama anavyoutafakari Mtakatifu Paulo mtume, katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho 13: 4-7 na kuuweka katika mazingira ya familia: Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari, haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; haoni uchungu, hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote, huamini yote. Baba Mtakatifu anasema huu ndio urafiki unaojengwa katika upendo wa dhati; unathamini na kujali utajiri wa mwingine pamoja na kuwa na jicho pana zaidi kwani ndoa ni mchakato unaomwilisha zawadi za Mungu kwa binadamu!

Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kuchangamkia maisha ya ndoa na familia na wala wasione kuwa ni mzigo usioweza kubebeka bali safari ya maisha inayowaelekeza kwenye ukomavu, kwa kupokea kwa ukweli na busara mapungufu yao ya kibinadamu na changamoto zilizoko mbele yao. Vijana wanapaswa kujikita katika majadiliano ili kushuhudia, kuishi na kukomaa katika upendo. Watambue kwamba, wanatofautiana na kwamba, tofauti zao ni sehemu ya utajiri wao!

Upendo wao ni chachu muhimu sana katika maisha ya ndoa, familia na huduma kwa maisha ya pamoja. Hapa kuna haja kwa vijana kupata malezi makini kuhusu vionjo vya kimwili, ili kuwa na mwelekeo sahihi na mpana zaidi. Upendo ni zawadi ya ajabu inayofumbata utakatifu na tunu msingi za maisha! Vijana wawe na mwelekeo sahihi wa tendo la ndoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia. Vijana waheshimu na kuthamini tendo la ndoa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata ubikira ni kielelezo cha upendo na kwamba, ndoa na ubikira ni mielekeo miwili tofauti ya upendo.

Wanandoa wanaendelea kuhamasishwa na Kanisa kuhakikisha kwamba, wanaboresha mahusiano ya upendo wao kila siku kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo ni kiini cha maisha, uzuri na utakatifu unaoweza kuleta mabadiliko makubwa kwa siku za usoni, kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia! Baba Mtakatifu anawataka vijana kuangalia daima historia ya wazazi na walezi wao, ili kuwa na nguvu ya kuleta mageuzi katika familia. Sura ya nne ya Wosia wa Kitume, Furaha ya upendo ndani ya familia ni muhtasari wa mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika maisha ya ndoa na familia. Hii ni nguvu ya kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, daima kwa kujikita katika imani, matumaini na mapendo yanayodumu daima. Mwishoni, amewapatia washiriki wote baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.