2018-07-16 15:09:00

Mkutano wa 19 AMECEA: Ajenda 7 za Mababa wa AMECEA, mwaka 1961


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA kuanzia tarehe 13 - 23 Julai 2018 linaadhimisha mkutano wake wa 19 unaoongozwa na kauli mbiu “Tofauti mtetemo, Hadhi sawa, Umoja wa Amani ndani ya Mungu kwenye kanda ya AMECEA”. Padri Ferdinand Lugonzo, Katibu mkuu wa AMECEA amesema kuwa, AMECEA ilizaliwa kwa lengo la kuwa na mbinu za pamoja  za kichungaji kwa maslahi ya watu wa kanda ya AMECEA. Miongozo ya Mababa waanzilishi wa AMECEA ilikuwa kuimarisha Imani Katoliki na maendeleo endelevu na fungamani ya jamii kwa kuwa na Mpango Mkakati  wa muda mrefu  uliowekwa katika Mkutano  Mkuu wa AMECEA uliofanyika Julai 1961, kwenye Ukumbi wa Msimbazi Center, Jimbo kuu la Dar es Salaam ukiwa na  dhamira kuu ya  “Kesho ya Kanisa la Bara la Afrika.”

Mkutano huu ulitoa ajenda kuu saba: Ajenda ya kwanza ilikuwa Kanisa na Vyombo vya mawasiluiano ya jamii: Uanzishwaji wa vituo vya televisheni, Radio na Uchapishaji wa magazeti. Ajenda ya pili ilikuwa, Mafunzo ya awali na endelevu ya maisha ya kiroho kwa wakleri wa majimbo, ya tatu  mahitaji ya Kituo cha uchungaji  na  malezi endelevu.  Ajenda ya nne ilikuwa ni  uwezekano wa kuwa na Chuo Kikuu cha AMECEA au angalau Chuo Kikuu kishiriki. Ya tano ni  kuwa na Programu ya Kujitegemea na kulitegemeza Kanisa Afrika Mashariki na Kati. Agenda ya sita ilikuwa  mwelekeo wa  shule za kikatoliki na Elimu  Katoliki ili kuwa na silabasi ya dini ya kikristo) na ya saba ni haki na amani katika Ukanda wa AMECEA.

Kumbe, jukumu kubwa la AMECEA ni kuhamasisha na kuwezesha familia ya Mungu kuwa na moyo wa uinjilishaji na maendeleo endelevu na fungamani; kwa kuwawezesha waamini kuwa ni mashuhuda na vyombo vya furaha ya Injili Barani Afrika ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, umoja na mshikamano kati ya watu wa Mungu. Haya ndiyo malengo ambayo yataiwezesha AMECEA kuwa na mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa muda mrefu zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa Barani Afrika.

Askofu mkuu mstaafu Telesphore Mpundu wa Jimbo kuu la Lusaka, Zambia, katika hotuba yake, amekazia umoja na mshikamano miongoni mwa familia ya Mungu Ukanda wa AMECEA; umuhimu wa maboresho ya maisha ya kiroho, kwa kuwa na sera na mbinu mkakati wa pamoja unaolenga kupyaisha ari na moyo wa sala, ibada na uchaji wa Mungu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kidunia. Amegusia kuhusu Jumuiya Ndogo ndogo za Kikristo zilizoibuliwa kwa mara ya kwanza kutoka DRC na kuimarishwa na AMECEA kama sehemu ya mbinu mkakati wa shughuli zake za kichungaji kwa familia ya Mungu, Afrika Mashariki na Kati kunako mwaka 1974.

Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni sehemu muhimu sana ya Kanisa Mahalia; mahali ambapo Wakristo wanasali, wanasikiliza na kutafakari Neno la Mungu; wanashiriki adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu wanalolimwilisha katika: imani, matumaini na mapendo yaani ”Koinonia”. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo ni mahali pa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu yaani “Kerygma”. Hapa ni mahali ambapo imani ya Kikristo inamwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji yaani “Diakonia”.

Lengo kuu ni kuwawezesha Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda wa Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za Bara la Afrika. Kimsingi, Jumuiya ndogo za Kikristo ni chombo makini cha uinjilishaji, zinazosaidia kujenga na kuimarisha ujirani mwema, udugu na upendo wa Kikristo. Ni mhimili wa maisha na utume wa Kikristo katika kujenga imani, maadili na utu wema. Ni sehemu ya muundo wa Kanisa Mahalia Barani Afrika, katika maisha na utume wake. Ni mahali pia pa kukuza na kudumisha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene kwa ajili ya huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo zinakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinaendelea kufanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.

Askofu mkuu mstaafu Mpundu, amewataka Maaskofu kuonesha upendo na mshikamano kati yao, kwa kuhangaikiana na kusaidiana wakati wa raha na shida; kwa kuwa na mbinu mkakati wa muda mfupi, muda wa kati na mrefu katika mchakato wa uinjilishaji, sanjari na kuwahusisha waamini walei, ili waweze kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Utu na heshima ya wanawake Barani Afrika, vipewe msukumo wa pekee na Kanisa kwa kutambua kwamba, wanawake wanachangia sana katika ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Mungu Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.