2018-07-14 06:58:00

Mnatumwa kuwa mashuhuda wa furaha ya Injili ya Kristo kwa Mataifa!


Majaalimu wawili walikuwa wakishirikishana uzoefu wao na utaalamu wao juu ya maisha. Mmoja akamwambia mwenzake, Henry ameniambia kuwa ni mmoja wa wanafunzi wako. Yule akajibu, ni kweli. Huyu Henry huwa anahudhuria vipindi vyangu vingi lakini si mmoja wa wafuasi wangu. Bahati mbaya wapo wahudhuriaji wengi tena kwa mbali lakini wapo mitume/wafuasi wachache.

Injili ya Luka ina habari mbili za utumaji. Katika sura ya 9 wanapelekwa wale 12 na sura ya 10 wale 70. Injili ya Matayo ina habari ya kutumwa mitume wale 12 tu. Huku kupelekwa 70 kadiri ya Luka kunaelezea utume wa kimataifa na ule wa Matayo 10:6 yaani wale 12, kwaelezea utume katika taifa ya Israeli – kwa kondoo waliopotea wa Israeli. Kadiri ya Wayahudi yapo makabila 12 ya Israeli na mataifa 70 katika ulimwengu. Katika injili ya Marko wale 12 wanaitwa mitume, yaani waliotumwa. Pengine pote wanaitwa wafuasi, yaani wanafunzi. Hivyo yule aliyetumwa anakuwa sehemu ya wokovu wa watu kwa kutangaza hiyo habari njema. Kadiri ya wataalamu wa maandiko matakatifu utume wa mitume 12 unawekwa wazi siku ile ya karamu ya mwisho. Mtume Paulo anasema ili ufuasi uwezekane ni lazima kuongozwa na roho ya Kristo inayotuita tuwe huru na inayotuwezesha kutoa jibu katika huo ufuasi. Wito wa ufuasi hautegemei kusikia sauti ya roho zetu bali twaitwa kusikiliza sauti ya roho yake Kristo. Kwa namna hii ufuasi utawezekana.

Katika ujumbe wa utume, Yesu anaweka wazi sifa za hao mitume na utume wenyewe – upole na unyenyekevu na anaweka wazi wajibu rasmi akisisitiza kuwaponya wagonjwa – lengo kuu likiwa ni kuutangaza ufalme wa Mungu. Yesu anawaagiza wawekeze katika Injili na kujiepusha na mahangaiko ya kawaida ya maisha. Wasibebe kitu cho chote kitakachosababisha kuchelewesha utume wao.  Katika aina hii ya utume inaonekana wazi kuwa yahitajika roho mpya na moyo mpya. Mtume Paulo anajivunia ushindi unaoletwa kwa msalaba wa Kristo – Kristo mzima, anajivunia Kristo. Anasema wazi anayejivuna na ajivune katika Kristo – 1 Kor. 1:31; 2 Kor. 11:16-21. Majivuno yetu leo ni yapi au yako katika jambo lipi? Mtume Paulo alitimiza wajibu wa kwanza kabisa wa mbatizwa, yaani kuutangaza ufalme wa Mungu.

Katika mwaliko huu wa utume na ufuasi kila kitu kinapata maana mpya katika ufalme wa Mungu. Yesu anaposema ufalme wa Mungu umekaribia anatoa mwaliko wa utendaji na mtazamo mpya wa maisha. Mwaliko wa Yesu kama  tubuni na kuiamini injili, mpende adui yako,  kama mkono wako ukikukwaza ukate, ni afadhali kuingia ufalme wa Mungu u kigutu kuliko kuukosa ni mwaliko wa kufanya mabadiliko na kuwa tayari kuutangaza ufalme. Maisha mapya ya Mtume Paulo baada ya kuitwa yanaweza kutoa kielelezo wazi ni aina gani ya maisha ambayo mtume na mfuasi wa Kristo anapashwa kuishi.

Injili ya leo inaweka wazi kile ambacho mitume wanatakiwa kuhubiri kwa watu – ‘watubu’ wakati ikielezea kwa kirefu jinsi wanavyotakiwa kuhubiri. Kwenda wawili wawili wakati ule ilikuwa ni kitu cha kawaida. Yesu aliwapeleka wawili wawili, anasema Mtakatifu Gregory Mkuu, ili kupandikiza upendo, kwa sababu umoja wa watu wawili unaonesha upendo. Ushuhuda wa kwanza wa kutoa ni upendo na kwa njia hiyo watu wote watawatambua kuwa ni wafuasi wangu, kama mkipendana kati yenu – Yoh. 13:35. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika kitabu ‘Yesu wa Nazareti’, anasema kuwa upya na upekee wa habari ya Yesu ni kwamba daima Mungu anatualika tutende sasa. Toka hapa twaweza kuelewa hitaji haraka la utendaji kadiri ya mafundisho ya Yesu kuhusu ufalme. Anayetaka kunifuata na akaangalia nyuma hafai kwa ufalme.

Kule kukung’uta mavumbi kueleweke kama ni nia ya Yesu kuwa ushuhuda kwao na siyo kuwa kinyume na wale watu.  Mitume huenda kwa watu kwa ajili ya wokovu wao na hivyo kuwa kinyume chao ingekuwa ni kwenda kinyume na utume wao. Lengo la utume si kupata fedha au sifa au pia kupata mavumbi yao. Msisitizo hapa ni kwamba wasihangaishwe na vipingamizi bali waendelee mbele na safari ya kuhuhiri Habari Njema ya Wokovu. Kwake Kristo ufalme wa Mungu uliongoza maisha yake na ushuhuda wake na anatualika kwa ujio wake kila siku. Sisi tunamgeukia Mungu tukisema – ufalme wako ufike. Lakini Mungu anatugeukia na kusema kupitia Kristo, ufalme wa Mungu upo kati yetu. Usingoje wala kusubiri. Karibu. Ujumbe wa Neno la Mungu katika Mk. 1:15 – wakati umefika, na ufalme mwa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini injili bado unabaki ujumbe hai kama ulivyotamkwa na Yesu mwenyewe. Mungu na watu wake watudai kuuweka katika matendo.

 Tumsifu Yesu Kristo,

Na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.