2018-07-11 16:58:00

Kardinali Bassettti: Ulaya bado ina kiu ya tunu msingi za Kikristo!


Mama Kanisa tarehe 11 Julai 2018 ameadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Benedikto, Abate, Mlinzi wa Bara la Ulaya. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya, anasema, umefika wakati kwa Bara la Ulaya kugundua tena fadhila ya matumaini, kwa kumweka mwanadamu kuwa ni kiini cha taasisi zake. Mtakatifu Benedikto, awaombee watu wa Bara la Ulaya! Katika maadhimisho haya, Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 1000 tangu kuanzishwa kwa Kanisa kuu la Abbasia ya “San Miniato al Monte” iliyoko Jimbo kuu la Firenze, Kaskazini mwa Italia.

Abbasia hii ilianzishwa kunako tarehe 27 Aprli 1018 na kuwekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa watoto wa Mtakatifu Benedikto Abate, ambao walijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kazi ya Mungu na ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, utakaopata utimilifu wake kwa wakati! Ni muda wa shukrani kwa Wabenediktini wanaoishi na kufanya utume wao katika Abbasia hii, kwa kuacha yote kwa ajili ya ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Mtakatifu Benedikto Abate, aliacha yote, akaamua kumfuasa Kristo Yesu na hivyo kuanzisha nyumba na familia mpya; akawa muasisi wa monasteri na shule na taasisi ambazo Barani Ulaya zimekuwa ni amana na utajiri wa utamaduni wa Kikristo!

Mtakatifu Benedikto Abate, katika maisha yake, akapewa karama ya kuwaongoza watu wa Mungu katika safari ya maisha ya kiroho, kuelekea katika uzima wa milele. Akawa Hakimu na Kiongozi kwa ajili ya watu wa Mungu, changamoto kwa Bara la Ulaya, kujikita tena na tena katika tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kitamaduni, daima kwa kuambata hekima ya Mungu katika sera na mikakati yake ya maisha, ili kukuza na kudumisha: usawa na haki kati ya watu, daima wakitafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Hii ni changamoto ya kujikita katika fadhila ya ukarimu na upendo kwa wageni, wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Hawa ni watu wanaopaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma na mapendo na wala si kama wavamizi, wezi na majambazi; watu wanaopaswa kupewa taabu na kushughulikiwa kama Mbwa koko kama inavyoonekana kwa sasa! Ikumbukwe kwamba, Mtakatifu Benedikto Abate, amechangia sana ustawi, maendeleo na mafao ya Bara la Ulaya katika ujumla wake. Ameacha utajiri, urithi na amana kubwa katika maisha ya sala na kazi; Ora et Labora! Utajiri wa Liturujia hauna mfano kama ilivyo pia katika Sanaa ya Mambo matakatifu.

Kardinali Gualtiero Bassetti, anahitimisha mahubiri yake kwa kusema, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anayeongoza nyoyo za waja wake, historia na maisha yao, alinde na kuiongoza familia ya Wabenediktini popote pale ilipo, ili kweli iweze kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wake kwa walimwengu; kwa kuonesha uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji; kwa kumwimbia sifa na utukufu, kwa zawadi ya maisha, neema, baraka, na mapaji mbali mbali ya akili na unabii kwa ajili ya ulimwengu mpya unaojikita katika upendo na udgu, sheria kanuni kwa watu wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.