2018-07-10 15:49:00

Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani, Panama 2019: Wimbo umekamilika!


Maadhimisho ya Siku ya XXXIII ya Vijana Duniani kwa ngazi ya kijimbo, ambayo kwa mwaka 2018 yaliongozwa na kauli mbiu “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu” Lk. 1:30 yalikuwa ni sehemu muhimu sana ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”.  Itakumbukwa kwamba, maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kuanzia tarehe 22 - 27 Januari 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38  Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mama wa Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu.

Bikira Maria anaendelea kufanya hija pamoja na waamini kwa kuwaongoza vijana wa kizazi kipya katika imani na udugu. Bikira Maria, Mama wa Kanisa awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuishi na kushuhudia vyema imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wajifunze kutoka kwa Bikira Maria kudumisha ukimya wa ndani, wakiyaelekeza macho ya nyoyo zao na imani pendelevu kwa Kristo Yesu, kwa Njia ya Msalaba, inayowapeleka katika mwanga wa furaha ya Ufufuko wa Kristo Yesu, kutoka kwa wafu na hivyo kuwakirimia ile furaha ya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya furaha na matumaini kwa watu wa Mataifa!

Tayari, Baraza la Maaskofu Katoliki Panama limebaini maeneo makuu yatakayotumika katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. Vijana wameanza kuwasha joto miongoni mwa vijana wenzao kwa kuandika nembo pamoja na wimbo maalum utakaotumika kwa ajili ya maadhimisho hayo, ambayo kimsingi ni sehemu ya mbinu mkakati wa Mama Kanisa, katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Kamati ya Maandalizi ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani nchini Panama imezindua wimbo utakaotumika kwa ajili ya maadhimisho haya, wimbo ambao umetungwa katika lugha ya Kihispania, Kiingereza, Kireno, Kifaransa na Kitaalia, lugha kuu tano zinazotumika kwenye maadhimisho haya! Haya yamesemwa na Shemasi Pedro Guevara-Mann, Msanii mkuu wa Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. Wimbo wa maadhimisho haya umetungwa na Abdiel Jimenes na kutafsiriwa katika lugha kuu zitakazotumika kwenye Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019.

Wimbo huu kwa lugha ya Kiitalia umeandaliwa na Monsinyo Marco Frisina, mtunzi maarufu sana wa nyimbo za Kanisa nchini Italia wakati ambapo wimbo huu kwa lugha ya Kiingereza umetungwa na Padre Robert Galea kutoka Australia. Toleo la Kimataifa na wimbo huu limetengenezewa nchini Panama na hivyo kuwapatia wasanii kazi ya “kutengeneza ndimi zao” ili kuboresha vitamkwa. Wasanii wa kimataifa walioteuliwa ni: Gabriel Díaz, Marisol Carrasco, Masciel Muñoz (Kihispania), Lucia Muñoz, Pepe Casis (Kiitalia), Naty Beitia (Kifaransa), José Berástegui na Eduviges Tejedor (Kiingereza) na Erick Vianna na Kiara Vasconcelos (Kireno).

Baraza la Maaskofu katoliki Panama linasema, eneo lililochaguliwa ni “Cinta Costera”, maana yake mji ulioko kwenye “Ukanda wa Ufukwe wa Bahari”. Hili ni eneo linalopambwa kwa rangi ya kijani na mazingira yanayovutia hata kwa macho! Eneo lililokubalika linakidhi vigezo msingi kwa ajili ya kutoa hifadhi kwa mahujaji watakaohudhuria maadhimisho haya, sanjari na kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ulinzi na usalama wa kutosha pamoja na utunzaji bora wa mazingira, mambo ambayo pia yametiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Askofu mkuu Josè Domingo Ulloa Mendieta nasema, idadi kubwa ya familia ya Mungu Amerika ya Kusini inaundwa na vijana wa kizazi kipya, lakini kwa bahati mbaya sana, wengi wao wanakabiliwa na ukosefu wa fursa za ajira, hawa ndio ambao Kanisa linataka kuwaonjesha huruma ya Mungu kwa njia ya sera na mikakati makini ya utume wa vijana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.