2018-07-10 15:09:00

Mbinu mkakati wa kuwalinda watoto kwenye maeneo ya vita na kinzani


Kisheria Mtoto ni mtu mwenye umri walau chini ya miaka 18 na kwamba, kuna haki msingi ambazo mtoto anapaswa kupewa kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa. Kimsingi, ustawi wa mtoto: yaani furaha, amani na utulivu ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee na taasisi, serikali na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Mtoto anayo haki ya kuishi huru, bila kutengwa kutokana na jinsia, rangi, umri au dini yake!

Lakini si ajabu kukutana na watoto ambao wanaishi katika mazingira ya vita na machafuko ya kila aina kiasi kwamba, watoto hawa wanajikuta wakikabiliwa na matatizo na changamoto mbali mbali katika maisha, malezi na makuzi yao. Wakati mwingine watoto hawa wanalazimika kuzikimbia familia zao, hali inayohatarisha matumaini yao kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, inabuni mbinu mkakati wa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi ya vita na kinzani.

Huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernardito Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati akichangia mada kuhusu mbinu mkakati wa kuwalinda watoto wanaoishi katika mazingira ya vita, yanayopelekea mara kwa mara watoto kama hawa kunyimwa haki zao na matokeo yake kunyanyasika sana. Vita haina macho, kumbe, katika mazingira ya vita, hata watoto pia wanajikuta wakipoteza maisha.

Watoto wamekuwa wakitumiwa kama chambo katika mapigano kwa kupelekwa mstari wa mbele au kutumiwa kama ngao dhidi ya mashambulizi ya kijeshi. Inawezekana kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ikashindwa kutatua migogoro yote ya vita kwa wakati huu, lakini Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halina budi kuhakikisha kwamba, watoto wanaoishi katika maeneo na mazingira ya vita wanalindwa na kuheshimiwa na kwamba, wale wote watakapatikana wanavunja sheria na taratibu za Jumuiya ya Kimataifa washughulikiwe kikamilifu na kwamba, utekelezaji wake unafanyika mara moja!

Askofu mkuu Bernardito Auza amekazia mambo makuu matatu yanayopaswa kupewa kipaumbele na Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaL: wajibu wa kuwalinda watoto; umuhimu wa kuwarejesha watoto waliokuwa vitani kwenye jamii zao pamoja na kuhakikisha kwamba, watoto wanapata nafasi ya elimu. Mosi, wawajibishwe kisheria wale wote wanaowapelekea watoto mstari wa mbele kama chambo cha vita; wanaowatumbukiza watoto katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Sheria ishike mkondo wake kwa wale wote watakaokamatwa wakiwateka nyara watoto, kuwanyanyasa na kuwanyonya watoto. Jambo la msingi ni kuhakikisha haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa sanjari na kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa zinazowalinda watoto wadogo.

Pili, Watoto waliokuwa mstari wa mbele vitani wanaporejea wasaidiwe kuingia katika jamii zao; kwa kupewa mafunzo maalum yatakayowasaidia kurekebisha tabia mbaya walizojifunza wakati wakiwa vitani. Juhudi hizi zifanywe kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mtoto mwenyewe na jamii katika ujumla wake. Ilikufanikisha zoezi hili kuna haja ya kutenga rasilimali fedha na watu, ili hatimaye, kuwajengea watoto matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Tatu, Jamii ihakikishe kwamba, watoto wanapata elimu kama sehemu ya haki zao msingi, ili hatimaye, waweze kuwa ni wajenzi na mashuhuda wa haki na amani kwa siku zijazo. Elimu ni muhimu sana katika mapambano dhidi ukosefu wa usawa na umaskini kama inavyobainishwa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Vatican na Kanisa Katoliki katika ujumla wake, limekuwa mstari wa mbele kwa kuwekeza katika sekta ya elimu, ili kuwapatia watoto na vijana elimu bora itakayowajengea uwezo wa kupambana na mazingira yao. Watoto ambao wamekuwa ni wahanga wa vita, nyanyaso na dhuluma wasaidiwe kikamilifu, ili hatimaye, waweze kuandika tena upya historia ya maisha yao na hivyo kutekeleza ile ndoto ya maisha yao, tayari kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Juhudi hizi zitasaidia sana kuzuia kinzani na mipasuko ya kijamii na hatimaye, kujenga jamii inayojikita katika msingi wa amani na jumuiya fungamani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.