2018-07-09 16:07:00

Siku ya Sala ya Kiekumene Bari: Mageuzi makubwa katika uekumene!


Professa Andrea Riccardi, Muasisi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio anasema, Mji wa Bari, Kusini mwa Italia umeweka historia ya majadiliano ya kiekumene kati ya Makanisa na Jumuiya za Kikristo! Huu ni mji ambao Jumamosi, tarehe 7 Julai 2018 umekuwakutanisha viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo kutoka Mashariki ya Kati kwa ajili ya tafakari na kuombea amani na umoja huko Mashariki ya Kati. Siku hii imeongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”.

Professa Riccardi anakaza kusema, Siku ya Sala ya Kiekumene imekuwa kama maadhimisho ya Sinodi kwa kuwakutanisha viongozi wakuu wa Makanisa, Jumuiya za Kikristo na watu wa Mungu katika ujumla wao. Ni Sinodi ambayo imewaunganisha kwa ajili ya kujadili matatizo, changamoto na fursa zilizopo huko Mashariki ya Kati. Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo huko Mashariki ya Kati ndiyo mada iliyowakusanya Mababa hawa wa Kanisa ili kwa pamoja waweze kutafakari na kusali.

Hiki ndicho kielelezo makini cha uekumene wa sala unaomwilishwa katika uekumene wa huduma ili kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano miongoni mwa Wakristo kama njia pia ya kujenga na kudumisha amani duniani. Katika mkutano huu wa sala, Baba Mtakatifu amekazia umoja na udugu; umoja na utofauti, lakini mambo yote yanaunganishwa katika imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Siku ya Sala ya Kiekumene imeonesha umoja wa Makanisa; ushirikiano wa wakuu wa Makanisa na Jumuiya ya za Kikristo pamoja na familia ya Mungu iliyowaunga mkono kwa uwepo wenye furaha na sala.

Haya ni matunda ya ushirikiano wa kiekumene kati ya viongozi wa Makanisa. Professa Andrea Riccardi, Muasisi wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio anahitimisha kwa kusema, kifungo cha urafiki kati ya wakuu wa Makanisa kimewezesha Makanisa kukutana, kusali na kutafakari kuhusu hatima ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Itakumbukwa kwamba, ilikuwa ni tarehe 7 Julai 1972 Patriaki Athenagoras alipofariki dunia. Mwenyeheri Paulo VI  na Patriaki Athenagoras waliandika kurasa mpya za uekumene wa sala kwa kutembeleana, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kunako mwaka 1964.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 
All the contents on this site are copyrighted ©.