2018-07-08 08:48:00

Siku ya Sala ya Kiekumene Bari: Uekumene wa sala, umoja na amani!


Viongozi wa Makanisa pamoja na Jumuiya za Kikristo kutoka Mashariki ya Kati, Jumamosi, tarehe 7 Julai 2018 wameungana kwa pamoja kuadhimisha Siku ya Sala ya Kiekumene ambayo imeongozwa na kauli mbiu “Amani ikae nawe: Umoja wa Wakristo kwa ajili ya Mashariki ya Kati”.  Hii ni hija ya uekumene wa sala na maisha unaowabidisha kufanya hija ya pamoja, inayofumbatwa katika ukarimu na nguvu ya maisha ya kiroho kiasi hata cha kujisikia kuwa karibu zaidi.

Viongozi wamekusanyika mjini Bari, kielelezo cha utamaduni wa ukarimu na watu kukutana. Hapa ni mahali ambapo, waamini wanamheshimu sana Bikira Maria wa “Odegitria” yaani, “Mama anayeonesha njia”. Ni mahali anapoheshimiwa sana Mtakatifu Nicholaus wa Bari na waamini wa Makanisa yote. Ni mtakatifu aliyebahatika kuwa na karama ya kuganga na kuponya madonda ya watu! Ndiyo maana viongozi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo walipofika mara baada ya kusalimiana, waliteremka wote kwa pamoja kwenda kusali, ili kuomba ulinzi na tunza ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari pamoja na kumwomba aweze kusaidia kuganga na kuponya madonda ambayo waamini wengi wanabeba katika sakafu ya mioyo yao. Hapa ni mahali ambapo waamini wa dini kuu duniani wamebahatika kukutanika na kwamba, mji huu ni kielelezo cha ustaarabu wa watu wa Mataifa!

Viongozi wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wanahimizwa kuiadhimisha Siku ya Sala ya Kiekumene huku akili na nyoyo zao zikiwa zimeelekezwa Mashariki ya kati ili kuombea amani na umoja. Viongozi hawa wamewasha taa ya matumaini kwa familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati! Baadaye, wote kwa pamoja wamesali ufukweni mwa Bahari ya Adriatic, mjini Bari! Baba Mtakatifu Francisko ametoa utangulizi wa Sala ya Kiekumene akielezea umaarufu wa Mashariki ya Kati sanjari na umuhimu wa sala katika umoja na amani!

Mwenyezi Mungu ni mwangaza utokao juu na mionzi yake imeujaza ulimwengu kwa imani na hivyo ukawa ni chemchemi ya tasaufi ya imani kwa Mungu mmoja huko Mashariki ya Kati. Ni mwanga unaobeba Ibada za kale na ambazo ni za pekee kabisa; ni mahali penye amana na utajiri mkubwa wa sanaa takatifu, taalimungu na urithi mkubwa wa Mababa wa imani. Mapokeo haya ni utajiri na amana inayopaswa kulindwa na kudumishwa kwa nguvu zote, kwani huko Mashariki ya Kati kuna mizizi ya nyoyo zao. Lakini eneo la Mashariki ya Kati katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni limegeuka kuwa ni uwanja wa fujo: vita, ghasia na uharibifu mkubwa; uvamizi, chimbuko la misimamo mikali ya kidini na kiimani, uhamiaji wa shuruti pamoja na baadhi ya watu kutelekezwa. Kumekuwepo na kimya kikuu kwa watu wengi na baadhi yao kuhusika moja kwa moja. Mashariki ya Kati limekuwa ni eneo ambalo watu wake wanalikimbia, kiasi cha kutishia uwepo wa imani ya Kikristo katika eneo hili, lakini, ikumbukwe kwamba, bila Wakristo utambulisho wa Mashariki ya Kati unaingia “mchanga”.

Uekumene wa Sala na huduma: Baba Mtakatifu anasema, wameianza Siku ya Sala ya Kiekumene kwa kuwasha taa alama ya umoja wa Kanisa na kwamba, kwa pamoja wanataka kuwasha taa ya matumaini itakayofukuzia mbali giza la usiku katika historia. Lengo ni kuwasha moto wa matumaini kwa mafuta ya sala na upendo. Huu ni mchakato wa sala kwa Mwenyezi Mungu inayomwilishwa katika huduma kwa jirani na huu ndio uekumene wa huduma makini kwa watu wa Mungu, kwa kutafuta: ustawi, maendeleo na mafao yao. Kwa njia hii, moto wa Roho Mtakatifu utaweza kung’ara katika umoja na amani!

Sala ya Umoja: Baba Mtakatifu anaendelea kusema, viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wanasali ili kumwomba Mwenyezi aweze kuwakirimia amani ambayo viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wameshindwa kuwapatia watu wao. Kilio cha amani kinaendelea kusikika huko Mashariki ya kati. Wanaombea amani kwa mji wa Yerusalemu unaopendwa na Mwenyezi Mungu lakini umeharibiwa na binadamu.

Sala ya amani: bado kuna damu ya watu kama Abeli inayomlilia Mwenyezi Mungu na kamwe kilio cha watu hawa hakiwezi kufumbiwa masikio kwa kulalama kuwa wao si  walinzi wa ndugu zao. Kutojali kunaua! Wakristo wanataka kuwa ni sauti inayopingana na mauaji kwa kutojali. Kanisa linataka kuwa ni sauti ya wale wasiokuwa na sauti; watu ambao wamelia sana kiasi kwamba, sasa machozi yamekauka mashavuni mwao! Baba Mtakatifu anakaza kusema, leo hii Mashariki ya Kati, watu wanalia sana; wanateseka na kukaa kimya, wakati kuna watu wengine wanaoendelea kuwanyanyasa na kuwadhulumu haki zao msingi, kutokana na uchu wa mali na madaraka! Kwa watu wadogo na waliojeruhiwa; watu wa kawaida, ambao kimsingi ni watu wa Mungu; hao ndio wanao ombewa amani, faraja, ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kuganga na kuponya majeraha na hatimaye, aweze kusikiliza sala na dua zao!

Mara baada ya kusali mbele ya Masalia ya Mtakatifu Nicholaus wa Bari na kuwasha taa ya matumaini; viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wakarejea tena kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari ili kuendelea na mkutano wao wa faragha! Haya ni majadiliano katika ukweli na amani miongoni mwa viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo! Viongozi wote hawa wamepata chakula cha mchana kwenye Makao Makuu ya Jimbo kuu la Bari-Bitonto na Askofu mkuu Francesco Cacucci.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.