2018-07-08 08:20:00

Papa Francisko: Kilio cha watoto Mashariki ya Kati kisute dhamiri zenu


Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya wakuu wa Makanisa na Viongozi wa Jumuiya za Kikristo, Jioni, tarehe 7 Julai 2018 amehitimisha Siku ya Sala ya Kiekumene huko Bari, Kusini mwa Italia kwa kukazia Habari Njema ya Wokovu; umuhimu wa majadiliano; amegusia madonda ya vita huko Mashariki ya Kati na umuhimu wa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani duniani!

Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema, huruma na upendo wake, uliowawezesha kukutana kwa sala na kushirikishana: tafakari na mang’amuzi mbali mbali kutoka Mashariki ya kati, ili kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu ni Mfalme wa amani, anayewataka wafuasi wake kurudisha upanga alani mwake! Utambulisho wao kama Kanisa unakumbana na kishawishi cha kutaka kumezwa na malimwengu; kwa kujikita katika uchu wa mali na madaraka; kwa kukumbatia mantiki ya kutaka kufanya mambo kwa haraka na kadiri ya watu wanavyojisikia.

Dhambi inayoendelea kuwapekenyua Wakristo ni kule kushindwa kumwilisha na kushuhudia imani katika matendo, changamoto inayohitaji tena toba na wongofu wa ndani. Injili ya Kristo inawahakikishia waamini uhuru wa kweli unaohitajika wa haraka sana huko Mashariki ya Kati, kunakoendelea kuwaka moto wa vita, nyanyaso na dhuluma! Hakuna sababu ya kukimbia mateso kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu kule Bustanini Getsemani, bali kwa njia ya sadaka, majitoleo pamoja na kumuiga Kristo Yesu, wataweza kuona mapambazuko ya Pasaka ya Bwana!

Habari Njema ya Wokovu anasema Baba Mtakatifu inafumbatwa katika Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kielelezo cha upendo wake mkuu ambao umewafikia hata watu wanaoishi huko Mashariki ya kati, kiasi cha kuunganishwa na nguvu ya Msalaba ambayo ni chemchemi ya: Usalama na faraja; nguvu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa wote licha ya changamoto na magumu yanayojitokeza kwa sasa! Imani ya Wakristo inayobubujika kutoka huko Mashariki ya kati, iwe ni chemchemi ya utakaso, kama inavyofanyika kwa waamini wanapokwenda Yerusalemu, kwenye Madhabahu mbali mbali nchini Misri, Yordani, Lebanon, Siria, Uturuki na maeneo mengine matakatifu huko Mashariki ya Kati! Wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wamejadiliana katika udugu, alama ya kutafuta na kuambata umoja bila kuogopa tofauti zinazojitokeza kati yao!

Amani inapaswa kutafutwa kwa udi na uvumba, kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili kudumisha utashi wa majadiliano na sanaa ya kusikilizana kwa dhati! Viongozi wakuu wa Makanisa na Jumuiya za Kikristo wanasema, wanataka kutembea, kusali na kufanya kazi kwa pamoja kama kielelezo cha mshikamano wa dhati. Hakuna sababu ya kuogopana kuzungumza katika ukweli na uwazi; kukubali na kuridhia maoni na changamoto kutoka kwa wengine pamoja na kusumbukiana kwa hali na mali, ili kujenga na kudumisha uekumene wa huduma inayosimikwa katika mahitaji msingi, utu na heshima ya binadamu; kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini na amani, ili kilio cha vita kigeuke na kuwa ni wimbo wa amani! Ili kuweza kufanikisha yote haya, kuna haja kwa Wakristo kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya ujenzi wa amani duniani, kwa kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wote! Ni wakati wa kujikita katika ukweli na matumaini badala ya kutafuta kujinufaisha na hali ya kinzani na migawanyiko huko Mashariki ya Kati.

Madonda ya vita huko Mashariki ya Kati yanaendelea kuwaathiri wananchi wa kawaida huko Siria kiasi hata cha kuwatumbukiza katika majanga ya maisha: umaskini, magonjwa na njaa! Vita imekuwa ni sababu ya kuibuka kwa misimamo mikali ya kidini na kiimani, kiasi hata cha kufanya kufuru ya matumizi ya jina la Mungu. Lakini, vita hii, imeendelea kukuzwa kutokana na biashara haramu ya silaha, changamoto ambayo inapaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa, lakini zaidi na Nchi tajiri zaidi duniani.

Madhara ya vita ya Hiroshima na Nagasaki, bado hayajaweza kutoa fundisho kwa binadamu kutokana na uchu wa mali na faida kubwa; ni watu wanaotafura malighafi kama vile madini na gesi asili, bila kujali uharibifu wa mazingira nyumba ya wote! Hapa mafao ya kiuchumi ndiyo yanayotawala na wala si utu na heshima ya binadamu. Umefika wakati wa kutangaza na kushuhudia Injili ya amani anasema Baba Mtakatifu Francisko ili kukuza na kudumisha umoja, udugu na maridhiano kati ya watu kwa kuhakikisha kwamba, watu wote wanahakikishiwa haki ya kuendelea kuishi huko Mashariki ya Kati kwa kutambua kwamba, hata Wakristo wanayo haki ya kuishi huko Mashariki ya kati, wakiwa na haki sawa.

Mji wa Yerusalemu ni mji wa kale, mahali patakatifu pa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam, kumbe ni kitovu cha majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani! Mji wa Yerusalemu ni chemchemi ya amani, ustawi na maendeleo endelevu ya familia ya Mungu. Kumbe, unapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote na wala usiwe ni chanzo cha mipasuko ya kisiasa isiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa na hasa amani na matumaini kwa wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati! Majadiliano katika ukweli na uwazi kati ya Israeli na Palestina ni muhimu sana ili kupata amani ya kudumu kwa kuwezesha uwepo wa Mataifa mawili yanayojitegemea!

Injili ya Matumaini imeandikwa kwenye nyuso za watoto wadogo huko Mashariki ya kati! Hawa ni watoto wanaolia na kuomboleza kutokana na madhara ya vita, kiasi cha kudhani kwamba, kukimbia nchi yao ndiyo suluhu iliyobaki mbele yao! Vita ni kifo cha matumaini ya watu, kwani badala ya shule, watoto wanashuhudia magofu ya majengo yaliyobomolewa; ni watoto ambao milipuko ya mabomu imekuwa ni sehemu ya maisha yao ya kila siku, lakini, umefika wakati kwa Mashariki ya Kati kuwa ni sanduku la amani, linalowakusanya na kuwahifadhi watu wa dini mbali mbali! Jua la haki, liangazie giza la Mashariki ya Kati ili kuondokana na uchu wa mali na madaraka; vita na misimamo mikali ya kidini na kiimani; unyonyaji na dhuluma; iwe ni fursa ya kupambana na umaskini, ukosefu wa haki na pamoja na kutambua haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha hotuba yake ya shukrani kwa kusema, amani ikae nawe, haki ikae ndani mwake na baraka za Mwenyezi Mungu ziwashukie watu wote huko Mashariki ya Kati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.