2018-07-06 07:46:00

Yesu Kristo anakataliwa nyumbani kwao Nazareti! Maamuzi mbele!


Mwinjili Marko anasema Yesu alipofika Nazareti siku ya Sabato, alianza kufundisha ndani ya sinagogi. Ila hasemi alifundisha nini au namna gani. Mwinjili Luka anaweka wazi zaidi kile alichofundisha na kusema siku hiyo ya Sabato, kwamba alifundisha habari njema kwa maskini, msamaha kwa wafungwa, kurudisha uono kwa vipofu, kufungua wafungwa na kutangaza mwaka wa Bwana – Lk. 4:18-19. Aidha kile alichofundisha Yesu siku ile hutambulika na Kanisa kuwa Jubilei ya kwanza katika historia ya ukristo, tangazo la mwaka wa kwanza wa neema.

Ndugu zangu, tunachosikia leo katika injili ni tofauti kabisa na kilichotokea jumapili iliyopita. Jumapili iliyopita wale wagonjwa na wenye wagonjwa walimtambua Bwana wa uzima, wakamwendea na wakaponywa na magonjwa yao. Imani yao kwa Kristo iliwaokoa. Hawa wa leo wanamkana na sababu kubwa tu ni kwa vile wanamfahamu na familia yake. Wanakosa imani.

Leo tunasoma mojawapo ya sehemu yenye habari mbaya kabisa katika Injili – kwamba Yesu hakuweza kufanya miujiza na pia aliwaponya wagonjwa wachache – Mk 6:5. Sikitiko kubwa zaidi lipo katika sababu ya kutokuweza kufanya hivyo. Yesu hakuweza kufanya hivyo kwa vile wale watu hawakuwa na imani – alishagazwa na imani yao – Mk. 6:6. Na Sababu ya kukosa kwao imani inaelezwa pia na Yesu – nabii hakosi heshima isipokuwa nyumbani kwake – Mk. 6:4. Dhana ya kudhani kujua yote inawaponza wao wa wakati ule na pengine hata wakati wetu huu. Mhubiri mmoja anasema, kinachowaponza watu wengi ni kudhani kuwa wanamfahamu Mungu. Anaendelea kusema, wengi wetu huuongea sana juu ya Mungu na hatuongei na Mungu. Ndicho kilichowapata Waisraeli katika somo la kwanza – Eze.2:5 – wakaadhibiwa sababu ya kukosa kwao imani. Nabii Ezekieli alijaliwa roho ya kusikia na kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu kwa ufasaha. Lakini hawakumsikiliza wala yeye, wala neno alilokuwa anawaambia. Wakaishia utumwani.

Hali hii ya kukosa imani inaonekana sehemu mbalimbali katika Agano la Kale. Hii inaonekana tangu dhambi ya mwanzo pale mwanadamu alipoacha kumsikiliza Mungu na kumsikiliza nyoka – Mwa. 3.1.  Hata katika Agano Jipya tunaona muendelezo wa dhambi hii – Mdo. 7:51 – shemasi Stefano anaongea kuhusu ugumu wa mioyo yao na kukosa kwao imani. Hata kumpinga Roho Mtakatifu. Katika Lk. 19:41- hata Yesu alipoingia Yerusalemu hawakujua saa yao ya wokovu – wakaangamia. Ndicho tunachoona leo katika Injili – wanamkataa Yesu. Wanatafuta kila sababu ili kumkataa. Eti sababu wanamfahamu na ndugu zake.

Hali hii inaonekana hata katika mazingira yetu leo. Ni watu wangapi wanaishi kadiri ya amri na maagizo yake Mungu? Yule anayemkataa Kristo, atatoa kila aina ya sababu ili kulinda msimamo wake. Wapinga Kristo wako wengi kati yetu. Tunamshukuru Mungu kwamba anaheshimu uhuru wetu. Ila tumefanya matumizi mabaya ya uhuru huo. Hatuna budi kukumbuka kuwa ye yote yule anayeenda peke yake, yaani bila Mungu hupotea. Katika maandiko matakatifu, twaona kuwa pale ambapo mwanadamu alienda bila Mungu, kilichofuata ni maafa – Mwa. 3:1. Angalia somo la kwanza la leo na Injili.

Mtakatifu Agostino katika mojawapo ya tafakari zake anaandika akisema ‘naogopa Yesu aliye kati yetu au Yesu anayepita “timeo Iesum transeuntem’ anasema kuwa anaogopa Yesu anaweza kupita bila kumtambua, bila kuwa tayari kumpokea. Naye Mtakatifu Yohane Paulo II, katika mojawapo ya maandiko yake anasema kwamba ye yote anayemkana Mungu, atamkana na mwanadamu mwenzake. Je, ni mambo au hali zipi zinazochangia kumkataa Kristo katika mazingira yetu au wakati wetu wa leo? Kila mmoja atafakari changamoto hii.

Ndugu zangu, baada ya kusikia Neno la Mungu siku ya leo, tunaalikwa kutafakari sana juu ya maisha yetu ya imani. Imani ni zawadi toka kwa Mungu. Ni zawadi ambayo hatuna budi kuipokea kwa mikono miwili, kwa moyo mmoja na kwa shukrani kubwa. Mtume Paulo anapoungama juu ya imani yake katika 2Kor. 5:17 – anasema- basi mtu akiwa katika Kristo, ni kiumbe kipya. Ya kale yamepita, mapya yamefika. Na katika Fil. 2:5 – anasema - muwe nao moyo aliokuwa nao Kristo Yesu. Hakika hii ndiyo imani inayotukumbusha leo uwepo wa Bwana wetu Yesu Kristo ili tuweze kweli kumwamini na kumshuhudia vyema katika maisha yetu ya imani. Ili tuweze kumtambua, kumpokea na kumkubali katika mazingira yetu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.