2018-07-06 15:19:00

Papa Francisko: Laudato si: Ushauri wa wanasayansi; Ekolojia na Vijana


Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto inayojikita katika misingi ya haki na amani kwa sababu, mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” ambao ulizinduliwa rasmi mwezi Mei, 2015. Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka mitatu tangu kuchapishwa kwake, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu limeitisha kongamano la kimataifa kuanzia tarehe 5-6 Julai 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kuokoa nyumba ya wote na maisha duniani kwa siku za usoni.”

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake kwa washiriki wa mkutano huu wa kimataifa, Ijumaa, tarehe 6 Julai 2018 amekazia kwa namna ya pekee, mchango unaotolewa na Jumuiya ya wanasayansi kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi; changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga kwa kujikita katika wongofu wa kiekolojia na kwamba, vijana na watu mahalia wanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe wa mkutano huu wa kimataifa kwa kusikiliza kwa moyo kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini, wanaohitaji msaada na uwajibikaji ili hatimaye, kuleta mageuzi makubwa yanayofumbatwa katika wongofu wa kiekolojia, kama sehemu ya mchakato wa maboresho ya dunia ambayo inaendelea kuchakaa kama “jani la mgomba”. Wanasayansi wanasema, tabia ya ulaji wa kupindukia, matumizi mabaya ya rasilimali za dunia na uchafuzi wa mazingira umevuka kiwango cha dunia kuweza kustahimili, kiasi kwamba, kwa sasa kinachofuatia ni majanga asilia kama yanavyoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia. Kuna hatari kubwa ya kukiachia kizazi kijacho: mashimo, jangwa na taka.

Wasi wasi huu anasema Baba Mtakatifu hauna budi kuvaliwa njuga na kufanyiwa kazi kama sehemu ya ekolojia fungamani! Binadamu wana uwezo na mbinu za kuweza kushirikiana kwa ajili ya utekelezaji na uwajibikaji utakaowawezesha kutumia na kulinda dunia kwa busara zaidi. Itakumbukwa kwamba, mji wa Katowice Poland mwezi Desemba 2018, utakuwa ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira unaoandaliwa na Umoja wa Mataifa, kwa ajili ya kutekeleza Mkataba wa mabadiliko ya tabianchi uliofikiwa mjini Paris, Ufaransa kunako mwaka 2015. Serikali zote zinapaswa kutekeleza dhamana hii inayofumbatwa katika ukweli, ujasiri na uwajibikaji zaidi kutoka kwa nchi zilizoendelea zaidi duniani na kwamba, hapa hakuna tena muda wa kupoteza!

Wadau mbali mbali wanapaswa kushirikishwa ili kukoleza mchakato wa ekolojia fungamani. Mkutano wa Mazingira Kimataifa utakaofanyika kuanzia tarehe 12-14 Septemba 2018  huko San Francisko, Marekani ni fursa makini za kujibu kilio cha changamoto za utunzaji bora wa mazingira unaohitaji: sera, mikakati na wajibu wa kutekeleza kwa pamoja kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mshikamno na huduma. Taasisi na vyombo vya fedha kimataifa kama vile Benki ya Dunia na Shirika la Fedha Kimataifa vina nafasi kubwa katika kukuza na kudumisha maendeleo endelevu na fungamani kwa binadamu. Fedha ianze kutumika kama chombo cha kuzalisha utajiri na kukoleza maendeleo endelevu sanjari na utunzaji bora wa mazingira, hali inayohitaji wongofu wa kiekolojia. Kanisa na dini mbali mbali pia zina mchango wake katika mchakato wa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Ili kukabiliana na changamoto ya ekolojia fungamani kuna haja ya kuwashirikisha vijana na watu mahalia, lakini kwa namna ya pekee kabisa wananchi wa Amazonia, ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi; kwa kujikita katika mshikamano shirikishi unaofumbatwa katika haki, mila na tamaduni za watu. Inasikitisha kuona uharibifu mkubwa wa maliasili unaofanywa kwa watu mahalia; kuibuka kwa mifumo ya ukoloni mamboleo, utamaduni usiojali wala kuguswa na maendeleo ya wengine pamoja na ulaji wa kupindukia.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2019 hapa mjini Vatican inaongozwa na kauli mbiu Sinodi ya Amazonia: Njia mpya ya Kanisa kwa ajili ya ekolojia fungamani. Kwa wananchi wa Amazonia, ardhi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, eneo takatifu, utambulisho na chemchemi ya tunu msingi za maisha. Wananchi wa Amazonia ni kumbu kumbu endelevu ya utume wa Mungu aliowakabidhi binadamu wote, yaani utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Changamoto changamani zinaendelea kuibuka kila kukicha anasema Baba Mtakatifu Francisko, lakini mchango wa wajumbe hawa ni mkubwa sana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kizazi kijacho, changamoto kwa walimwengu kuwa na kiasi katika matumizi ya rasilimali za dunia, hali inayohitaji kuvunjilia mbali mambo yote yanayosababisha ukosefu wa haki, ili kuwajengea watu furaha na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.