2018-06-30 15:32:00

Wosia wa Papa kwa Familia ya Damu Azizi: Ujasiri, Upendeleo & Ushuhuda


Mama Kanisa ametenga mwezi Julai kwa ajili ya kukuza na kudumisha Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, Mto wa rehema, shule ya utakatifu, haki, haki, upendo na msamaha. Damu Azizi ya Kristo ni chemchemi ya huruma ya Mungu kwa binadamu. Hii ni Ibada ambayo inaenezwa kwa namna ya pekee kabisa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, Mashirika ya Kitawa pamoja na waamini walei. Fumbo la upendo wa Kristo limekuwa ni kivutio kikubwa cha waamini na waanzilishi wa Mashirika ya Kitawa kama vile Mtakatifu Gaspari del Bufalo na Mtakatifu Maria de Mathias, kiasi kwamba, fumbo hili la upendo limekuwa ni msingi wa Katiba ya Mashirika haya!

Damu Azizi ya Kristo ni chemchemi ya wokovu wa ulimwengu na kwamba, ni alama ya juu kabisa inayoshuhudia upendo na sadaka ya maisha kwa ajili ya wengine. Sadaka hii inajirudia tena na tena katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiasi cha Kristo kuwajalia waamini Mwili na Damu yake Azizi; Damu ya Agano Jipya na la milele, iliyomwagika kwa ajili ya maondoleo ya dhambi. Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 30 Juni 2018 alipokutana na kuzungumza na familia ya Damu Azizi ya Yesu inayoundwa na Wamisionari, Watawa na Waamini walei ambao wako chini ya Ushirika wa Damu Ya Kristo “Unione Sanguis Christi” “USG”.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, tafakari ya Sadaka ya Kristo Msalabani inawabidisha waamini kujikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu na jirani; tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwaganga na kuwaponya wale wote wanaoteseka kutokana na kumong’onyoka kwa sheria kanuni maadili; utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine bila kusahau ulaji wa kupindukia; unaopelekea mamilioni ya watu kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Hiki ndicho kiini cha huduma inayotolewa na Mashirika haya ya kitawa na kazi za kitume kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Katika maisha na utume kwa Kanisa na Jamii, Wamisionari wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume katika ushuhuda na kazi zao za kitume anasema Baba Mtakatifu, hawana budi kujikita katika mambo makuu yafuatayo: Ujasiri wa ukweli; Jicho la upendeleo kwa wote, lakini zaidi maskini; mvuto wenye mashiko na uwezo wa kuwasiliana na wengine. Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Ujasiri wa ukweli ni mchakato unaoiwezesha Jumuiya kujikita katika tunu msingi za Kiinjili, ukweli kuhusu ulimwengu na binadamu katika ujumla wake; kwa kukuza na kudumisha Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi kifo kinapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Ni mwaliko wa kuzungumza katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia utu na heshima ya binadamu  hasa kutokana na dhambi jamii na mifumo mbali mbali ya umaskini.

Pili, Baba Mtakatifu anawahimiza kutoa ushuhuda unaogusa maisha ya watu katika medani mbali mbali za maisha, ili kusaidia mchakato wa kuleta mageuzi katika maisha na nyoyo zao. Watumie lugha inayofahamika na wengi, ili ujumbe wa Injili uweze kgota katika maisha yao.  Watambue kwamba, walengwa wa upendo na wema wa Kristo Yesu ni watu wote lakini zaidi wale walioko mbali zaidi, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba wanawaendea na kuwatangazia uwepo wa Ufalme wa Mungu kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha na utume wake. Wamisionari wawe ni kielelezo na mfano wa Kanisa linalotembea mitaani, kati pamoja na watu, kiasi hata cha kuhatarisha maisha, lakini kwa kushirikishana furaha na mateso na wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha na utume wao!

Tatu ni mvuto wenye mguso na mashiko pamoja na uwezo wa kuwasiliana katika mchakato mzima wa: kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, Katekesi; Utume wa Biblia. Lengo ni kuhakikisha kwamba, waamini wanashirikishwa kikamilifu, ili waweze kuonja na kufurahia tunu msingi za maisha ya imani ya Kikristo, ili kuanza kujenga maisha mapya yanayojikita kwa Kristo Yesu. Wawe makini kwa Neno la Mungu na wasikivu kwa Roho Mtakatifu, anayewapatia maneno na matendo yanayowawezesha waamini kumfungulia Kristo na jirani zao malango ya maisha yao!

Utume wa kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu hauna budi kujikita katika majadiliano kama Kristo Yesu alivyokuwa anafanya kwa watu aliokutana nao katika maisha na utume wake. Yesu aliwafahamu watu wake upeo; akatambua utajiri na udhaifu wao, kwani hawa ndio wale ambao Mwenyezi Mungu anapenda kuwajalia Ufalme wake wa mbinguni. Kwa kuiga mtindo wa mahubiri ya Yesu, kutawawezesha wamisionari kuwa karibu zaidi na watu wa Mungu, na hivyo kuwaonjesha wema na huruma ya Mungu. Pamoja na ushauri wote huu, ikumbukwe kwamba, nguvu ya ushuhuda wa Injili inabubujika kutoka katika Injili yenyewe; kwa kuambata upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Damu Azizi ya Kristo na tasaufi yake.

Damu Azizi ya Kristo ni mto wa rehema na chemchemi ya upendo wa Mungu unaowavuta Mababa wa Kanisa na Watakatifu kama Bonaventura, Katharina wa Siena na Mtakatifu Gaspari del Bufalo, Padre na muasisi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Kristo, aliyejitaabisha kuhakikisha kwamba, anatangaza na kushuhudia upendo, huruma na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu kwa njia ya mahubiri na mafungo yake. Mtakatifu Gaspar alikuwa mnyenyekevu mbele ya Mungu, akavikwa na fadhila ya upendo; akawa ni chombo na shuhuda wa upatanisho na amani; kwa kuwapatia watu mambo msingi: kiroho na kimwili pamoja na kuwaonjesha upendo wa Mungu wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu amehitimisha tafakari yake kwa kuwakumbusha kwamba, Kristo Yesu ni mwamba wa matumaini yao ya daima. Katika maisha yao ya Kijumuiya na kitume, kipaumbele cha kwanza kiwe ni sala; Kusoma na Kulitafakari Neno la Mungu; watii kwa sauti ya Roho Mtakatifu; wajenge na kudumisha umoja, mshikamano na ushirikiano, mambo msingi yatakayowawezesha kuzaa matunda mengi ya maisha ya kiroho, kwa ajili ya mafao ya familia ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.