2018-06-30 15:53:00

Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu, Mto wa rehema!


Damu Azizi ya Kristo ni utimilifu wa maisha! Hii ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza hija ya wamisionari, watawa na waamini walei wa Ushirika na Waamini walei ambao wako chini Ushirika wa Damu Ya Kristo “Unione Sanguis Christi” “USG”, walipokutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican. Hili ni tukio ambalo limetanguliwa kwa katekesi ya kina kuhusu tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo iliyotolewa na Padre Marko Rupnik pamoja na shuhuda mbali mbali kutoka kwa kwa wamisionari, watawa na waamini mbali mbali walioguswa kwa tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo katika maisha yao!

Padre Terenzio Pastore, Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Italia, C.PP.S. amemwelezea Baba Mtakatifu umati wa taifa la Mungu uliokuwa mbele yake kwamba, unaundwa na wamisionari, watawa na waamini ambao wako katika hija ya kujitakatifuza kwa njia ya tasaufi ya Damu Azizi ya Kristo. Ni watu wenye imani, shida, changamoto na fursa katika maisha, lakini wote hawa wanafumbatwa katika kifungo cha upendo wa Damu Azizi ya Kristo Yesu. Padre Terenzio amemshukuru sana Baba Mtakatifu Francisko kwa wema, uwepo na ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kiasi cha kuwafanya waamini wengi kujisikia kuwa majirani! 

Kuna familia ambazo zimeguswa na kutikiswa sana kutokana na kuondokewa na wapendwa wao! Lakini pia, kuna familia ambazo zimesimama kidete kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika Injili ya uhai, kwa kukubali kuwapokea watoto kama zawadi kubwa kutoka kwa Mungu, ingawa walikuwa na ulemavu mkubwa! Hawa ni mashuhuda wa imani hai inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu. Kuna wazee wanaopambana na hali ngumu ya maisha, lakini pia vijana ambao wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kushiriki katika kazi ya ukombozi. Umati huu, umepambwa pia kwa uwepo wa waseminari na wanovisi wa mashirika mbali mbali wanaotaka kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kwa upande wake Sr. Nicla Spezzati, ASC, Mama Mkuu wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu Kanda ya Italia anasema, watawa na wamisionari wanatambua dhamana na wajibu wao wa kujitakatifuza kila kukicha, ili waweze kuwa kweli ni vyombo upatanisho. Wote hawa wanaunda familia moja ya Damu Azizi ya Kristo, Damu ya Agano Jipya na la milele, Fumbo la upendo, huruma na msamaha wa Mungu. Damu Azizi ya Kristo inawabidisha kusikiliza na kujibu kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wao pia waweze kuinua Kalisi ya matumaini katika maisha yao!

Damu ya Kristo, mto wa rehema ni chemchemi ya umoja na mshikamano wa watu kutoka katika kabila, lugha na jamaa waliokombolewa, tayari kuwashirikisha wengine ile furaha ya Injili inayowakutanisha na Kristo Yesu Mkombozi wa ulimwengu. Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Wafiadini wa Roma na mkesha wa Siku kuu ya Damu Takatifu ya Yesu, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Julai, familia ya Damu Azizi ya Yesu, uimependa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kuwaimarisha katika imani, ili waendelee kujikita katika furaha ya kuwa ni sehemu ya Kanisa. Hii ni dhamana inayowataka kutubu na kumwongokea Mungu, kuendelea kupyaisha maisha, ili kupokea, kuitangaza na kuishuhudia Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 
All the contents on this site are copyrighted ©.