2018-06-30 07:47:00

Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani ya Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, Ijumaa tarehe 29 Juni 2018 anasema, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na Makardinali wapya, akabariki Pallio Takatifu kwa ajili ya Maaskofu wakuu wapya 29 walioteuliwa katika kipindi cha mwaka 2017-2018. Baba Mtakatifu amewashukuru wajumbe mbali mbali waliofika mjini Vatican kwa ajili ya maadhimisho haya mawili, ili kuwasindikiza Makardinali na Maaskofu wao katika mchakato wa kujisadaka zaidi kwa ajili ya huduma ya Injili na Kanisa. Baba Mtakatifu ametambua pia uwepo wa Ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza katika maadhimisho haya, alama makini katika mchakato mzima wa majadiliano na hija ya kiekumene; umoja na udugu, kielelezo cha neema ya Mungu katika Makanisa haya mawili!

Baba Mtakatifu katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, amekazia zaidi majadiliano kati ya Kristo Yesu na wafuasi wake na hatimaye, jibu makini lililotolewa na Mtakatifu Petro akishuhudia kwamba, Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai. Katika historia, Kristo Yesu amefahamika kuwa ni: Nabii wa haki na amani; Mwalimu mwenye hekima, ujuzi na maarifa; wengine walimwona kuwa ni Mwana mapinduzi, lakini Petro Mtume anakiri kwamba, Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ndio upya ulioletwa kwa njia ya imani kuhusu Fumbo la Maisha ya Kristo Yesu. Ufunuo huu ni matokeo ya kukutana na Yesu, Chemchemi ya maisha mapya; Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake na kwamba, ufunuo huu ni zawadi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, inayofumbatwa katika kiri ya imani ya Mtakatifu Petro, Mtume! Kwa njia hii, Kristo Yesu anamkabidhi Petro dhamana na utume kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa lake. Kwa mara ya kwanza kabisa, Yesu anatamka neno Kanisa, analitamka kwa upendo wake wote, kielelezo cha Jumuiya ya Agano Jipya inayojikita katika imani kwa Kristo Yesu, Uso wa huruma ya Baba wa milele. Mwenyeheri Paulo VI anasema, Kristo Yesu ni kiungo muhimu sana katika kujenga na kudumisha umoja na Mwenyezi Mungu, kwani Yesu ni Mwana wa pekee wa Baba na wengine wote ni watoto wateule wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.