2018-06-30 16:37:00

Rais Juan Evo Morales akutana na kuzungumza na Papa mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 30 Juni 2018, amekutana na kuzungumza na Rais Juan Evo Morales Ayma wa Bolivia, ambaye baadaye, amekutana na kuzungumza pia na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Taarifa kutoka Vatican zinabaisha kwamba, Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake, wamefanya mazungumzo yaliyogusia uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Bolivia.

Kwa sasa pande hizi mbili zinaangalia uwezekano wa kuboresha mkataba wa makubaliano kati ya nchi hizi mbili pamoja na kuangalia changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza kikanda na katika Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake! Rais Juan Evo Morales Ayma amekuwepo mjini Roma ili kuhudhuria sherehe ya kusimikwa kwa Makardinali wapya na hatimaye, kushiriki katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani hapo tarehe 29 Juni 2018. Kardinali Toribio Ticona Porco, Askofu mstaafu wa Jimbo Jimbo la Corocoro (Bolivia) ni kati ya Makardinali wapya, waliopewa heshima hii na Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 28 Juni 2018 wakati wa Ibada maalum!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.