2018-06-30 16:15:00

Papa Francisko aungana na maskini kumpongeza Kardinali Konrad


Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa, Ijumaa, tarehe 28 Juni 2018, amemshukuru Mungu kwa kumpatia dhamana na wajibu wa kujizatiti zaidi katika kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo, kwa kuhakikisha kwamba, imani inamwilishwa katika matendo; daima akijielekeza zaidi katika huduma kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ili nao pia waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.

Makardinali wanaojitambulisha kwa mavazi mekundu, wanaitwa kusadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, tayari kuwashirikisha watu wa Mataifa, ile furaha ya Injili. Ni mwaliko wa huduma makini kwa watu wa Mungu. Katika mazingira kama haya, Kardinali Konrad Krajewski, amewaalika: maskini, wahamiaji na wakimbizi; bila kuwasahau wafungwa waliomaliza adhabu yao, ili kumshukuru Mungu kwa dhamana na wajibu kama Kardinali. Idadi yao ilikuwa ni watu 280, tukio ambalo lilipambwa pia kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye alikiri kwamba, amekwenda kuonesha mshikamano wa umoja, upendo na udugu kwa maskini. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kusikiliza historia, maisha, mateso, changamoto na matumaini ya baadhi ya watu waliokuwepo mezani kwa muda wa masaa mawili na ushehe, tukio ambalo kamwe halitaweza kufutika kwa urahisi sana katika maisha maskini hawa!

Baba Mtakatifu amesalimiana na kila mmoja wao. Amepata nafasi ya kuzungumza na wakimbizi pamoja na wahamiaji wanaohudumiwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio. Mmoja kati ya maskini hao amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, katika maisha yake amebahatika kupata chakula na Mtakatifu Yohane Paulo II, Benedikto XVI na sasa Papa Francisko, viongozi ambao wameendelea kumwonjesha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake hata kama kwa sasa umri umepita! Baba Mtakatifu amezungumza na jirani zake, wanaohudumiwa kwenye Hosteli zilizoko kwenye viunga vya Vatican.

Baba Mtakatifu ameonesha wasi wasi wake mkubwa kwa watoto wahamiaji na wakimbizi wanaotenganishwa na wazazi wao huko Texas, nchini Marekani. Uamuzi wa Jumuiya ya Ulaya kutowapokea tena wakimbizi na wahamiaji kunahatarisha sana maisha ya watu wengi wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Mlevi mmoja amemwambia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, huu ni ugonjwa unaoweza kumkumba mtu yeyote na kumtumbukiza katika majanga makubwa ya maisha. Baba Mtakatifu amemwambia kwamba, Kanisa linajitahidi kutaka kuwasaidia watu walioathirika ili waweze kujikwamua kutoka katika hali hiyo na kuanza maisha mapya. Sherehe hii imehitimishwa kwa walengwa kuonesha furaha na shukrani zao kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Kardinali Konrad Krajewski, ambao kwao wataendelea kumwita na kumtambua kama “Don Konrad”, ingawa kwa wakati huu, alikuwa amebadilika kwa kuvaa vazi jekundu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.