2018-06-30 16:50:00

Kardinali Parolin: Jumuiya ya Ulaya inapaswa kudumisha haki na amani!


Kumekuwepo na ushirikiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Vatican na Serikali ya Montenegro, kwa lengo la kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika nchi hii. Uhusiano wa kihistoria na majadiliano katika ukweli na uwazi yalipelekea, miaka saba iliyopita, Vatican na Montenegro kutiliana sahihi mkataba wa ushirikiano. Pamoja na mambo mengine, mkataba huu unaheshimu dhamana na wajibu wa Serikali na Kanisa katika kuihudumia familia ya Mungu nchini Montenegro. Hatua inayofuata kwa sasa ni kuanzisha Ubalozi wa Vatican nchini Montenegro, ili kukuza na kudumisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya pande hizi mbili!

Haya yamesemwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa safari yake ya kikazi nchini Montenegro kuanzia tarehe 27-30 Juni 2018. Ubalozi mpya wa Vatican utakuwa ni kielelezo makini cha mchakato unaopania kujenga na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya pande hizi mbili; amani, umoja na mshikamano wa dhati. Kardinali Parolin, amewashukuru viongozi wa Serikali ya Montenegro kwa mapokezi na ukarimu wao; heshima na nafasi inayotolewa na Serikali kwa ajili ya utume na maisha ya Kanisa nchini humo. Ameitaka Serikali kuendeleza majadiliano ya kiekumene na kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali nchini humo, ili kukuza na kudumisha udugu na umoja wa kitaifa, amani na utulvu! Juhudi hizi ziende sanjari na udumishaji wa uhuru wa kuabudu mhimili mkuu wa haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Wananchi wa Montenegro wajenge umoja na kitaifa na kuondokana na ukabila usiokuwa na mvuto waka mashiko!

Kardinali Parolin, amemshukuru na kumpongeza Rais Milo Dukanovic wa Montenegro; viongozi wa Serikali pamoja na wawakilishi wa Kanisa mahalia, viongozi wa kidini na Makanisa ya Kikristo! Serikali na Montenegro imekwisha kupiga hatua kubwa katika mchakato wa kujiunga na Jumuiya ya Ulaya. Vatican inapenda kuchukua fursa hii, kuipongeza Serikali kwa hatua hii muhimu na kukumbusha kwamba, Umoja wa Ulaya ni Jumuiya inayojikita katika sheria kanuni na tunu msingi za maisha na wala si tu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kisheria. Kardinali Parolin, amemhakikishia Bwana Dusko Markovic, Waziri mkuu wa Montenegro kwamba, Umoja wa Ulaya unapaswa kujielekeza zaidi katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano sanjari na kuendeleza uhuru wa kidini, ustawi na maendeleo ya wengi; bila kusahau kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.