2018-06-29 13:29:00

Papa Francisko: Utukufu wa Kanisa unafumbatwa katika Fumbo la Msalaba


Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, miamba wa Kanisa, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Juni, Baba Mtakatifu Francisko, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu na kutoa Pallio Takatifu kwa Maaskofu wakuu wapya 29, walioteuliwa kati ya Mwaka 2017 hadi mwaka 2018. Maaskofu wakuu kutoka Kanisa la Afrika ni pamoja na: Askofu mkuu Isaack Amani Massawe wa Jimbo kuu la Arusha, Tanzania. Askofu mkuu Alick Banda wa Jimbo kuu la Lusaka, Zambia. Askofu mkuu Gervais Banshimiyubusa wa Jimbo kuu la Bujumbura, Burundi pamoja na Askofu mkuu Gabriel Charles Palmer-Buckle wa Jimbo kuu la Cape Coast, Ghana.

Pallio Takatifu walizopewa Maaskofu wakuu alama ya umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, watavishwa kwenye Majimbo yao Makuu na Mabalozi wa Vatican kwenye nchi husika, ili kuwawezesha watu wa Mungu katika Majimbo haya, kushiriki katika maisha na utume wa Maaskofu wao wakuu! Haya ni mabadiliko yaliyoletwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia sana umuhimu wa Mapokeo hai ya Kanisa yanayopyaisha furaha ya Injili na hivyo kuwawezesha waamini kutangaza na kushuhudia kwamba: Kristo Yesu ni Bwana kwa utukufu wa Mungu Baba! Ni Masiha, Mpakwa wa Bwana, aliyetumwa na Baba wa milele kwa ajili ya kuwakomboa binadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Ni Masiha aliyetumwa kuwapaka mafuta na kuwaganga, wale waliokufani, wagonjwa, wanaotubu na kumwongokea Mungu bila kuwasahau wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, ili wote hawa waweze kujisikia kuwa ni sehemu ya familia ya Mungu inayowajibika!

Kristo Yesu kwa njia ya: maisha, matendo na mahubiri yake, aliwatangazia na kuwashuhudia watu kwamba, wote walikuwa ni sehemu ya urithi wake na wala hakuna mtu awaye yote aliyetengwa na upendo wa Mungu. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, hata leo hii, waamini wanaweza kuthubutu kumkiri, kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa njia ya midomo, lakini zaidi kwa njia ya nyoyo zao, kile ambacho wamesikia, wakaona na kung’amua katika maisha yao! Hawa ni watu waliokuwa wamekufa kutokana na dhambi, lakini wamefufuliwa; wakaondolewa, wakapyaishwa katika undani wao na kupakwa mafuta ya matumaini.

Kongwa la dhambi likavunjiliwa mbali na sasa kwa furaha kuu na kumbu kumbu endelevu, waamini wanaweza kukiri kwamba, kwa hakika Kristo Yesu ni Mwana wa Mungu aliye hai! Kwa kiri hii ya imani kama ilivyoshuhudiwa na Mtakatifu Petro, Mtume, Baba Mtakatifu Francisko anasema, huo ukawa ni mwanzo kwa Yesu kutangaza Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu. Anawahimiza mitume wake, kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwani wamepakwa mafuta ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani!

Utume huu ni pevu, kwani una gharama zake: unaweza kuwapatia jina zuri, maisha ya raha mustarehe na nafasi katika uongozi wa Kanisa, lakini zaidi wakumbuke kwamba, kuna pia kifodini! Hapa ndipo Petro mtume, anapopigwa na bumbuwazi na kutaka kukimbia mateso na matokeo yake, anakuwa ni kikwazo kwa Kristo Yesu anayetaka kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni. Petro Mtume, alidhani kwamba, kwa njia hii alikuwa analinda haki ya Mungu, lakini akajikuta anageuka kuwa shetani na kwamba, alipaswa kutafakari na kufahamu vishawishi na majaribu ya shetani, mambo ambayo yatawaandama wafuasi wa Kristo katika maisha yao yote! Vishawishi vya shetani, daima vitaendelea kuwa ni kikwazo kikuu katika utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kushiriki mpako wa Kristo maana yake ni kushiriki katika utukufu wake unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba; mambo mawili ambayo ni sawa na chanda na pete, yanategemeana na kukamilishana. Wakati mwingine, Wakristo wanashawishika kuwa aina ya wale Wakristo wanaoyaweka madonda ya Kristo karibu sana na wao! Lakini, Yesu anawataka kugusa taabu na mahangaiko ya binadamu; kugusa miili ya wale watu wanaoteseka. Ikumbukwe kwamba, kukiri imani kwa midomo na mioyo yao, kuna maanisha kujifunza kufanya mang’amuzi ili hatimaye, kugundua yale mambo ambayo yanawafanya kutoguswa na mahangaiko ya wengine kama mtu binafsi na kama Jumuiya ya waamini, tayari kufanya maamuzi machungu!

Kristo Yesu kwa kuunganisha: Utukufu na Fumbo la Msalaba anawataka wafuasi wake na Kanisa katika ujumla wake kujikita katika huduma makini inayofumbatwa katika huruma na mapendo; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza sanjari na kuhakikisha kwamba, wanazamisha mizizi yao katika maisha ya watu wa Mungu. Tafakari na ufuasi wa Kristo unawataka Wakristo kuwafungulia malango ya nyoyo zao, wale wote ambao Kristo Yesu amejifananisha nao, kwani kwa hakika, Kristo Yesu, hawezi kuwaacha watu wake katika ombwe na utupu! Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu anawataka waamini kuendelea kuimba na kukiri kwamba, Kristo Yesu ni Bwana kwa utukufu wa Mungu Baba, tayari kuliwezesha Kanisa kung’ara kwa mwanga wa Kristo Yesu; Mwanga wa haki, ili kama ni kuishi, waamini waishi kwa ajili ya Kristo Yesu anayeishi na kutenda kazi ndani mwao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.