2018-06-29 08:30:00

Majadiliano ya kiekumene yanawawezesha Wakristo kutembea kwa pamoja


Katika mkesha wa Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa Imani inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 29 Juni, Kila mwaka, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 28 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na Ujumbe wa wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza, wa Kanisa la Costantinopoli kielelezo makini cha umoja wa Kanisa hilo na Kanisa Katoliki. Sherehe hii ni kumbu kumbu muhimu sana ya mafundisho na ushuhuda wao, mambo msingi yanayojenga Makanisa haya mawili sanjari na kutambua utume wa kutangaza na kushuhudia Injili kwa ajili ya binadamu wapya, wanaoelekea kwa Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, jamii nyingi ambazo zilijitambulisha kuwa ni za Kikristo hapo awali, zikawa ni mfano angavu wa uaminifu kwa Kristo Yesu, lakini leo hii zinaendelea kutumbukia katika ombwe na giza nene, kiasi hata cha kukosa mvuto na mashiko katika maisha ya hadhara. Hizi ni Jumuiya ambazo utu na heshima ya binadamu haupewi tena kipaumbele cha kwanza na matokeo yake uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka vinatawala; vita; maendeleo ya sayansi na teknolojia; uporaji wa maliasili yanaonekana kuwa ni matukio ya kawaida! Lakini, hakuna sababu ya kukata tamaa!

Baba Mtakatifu anasema kimsingi anakubaliana kabisa na maneno ya Patriaki Bartolomeo wa kwanza aliyotoa hivi karibuni mjini Roma kwamba, katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, badala ya kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano, yamejenga moyo wa uchoyo na ubinafsi na madhara yake ni makubwa katika maisha ya watu: yaani maana ya maisha na mahitaji msingi ya binadamu yamebadilika sana. Teknolojia kwa sasa imegeuka kuwa kama mungu mdogo!

Si haki kabisa kwamba, kuna kuwepo kwa maendeleo mbadala; nguvu ya mshikamano na mafungamano ya kijamii pamoja na haki zinapuuzwa! Makanisa yanaweza kuwa ni chachu ya mabadiliko katika ulimwengu mamboleo! Kanisa kimsingi ni nguvu ya mabadiliko, mshikamano, upendo na uwazi na kwamba, leo na kesho bora zaidi inafumbatwa si kwa kuwa na vitu bali kwa kuwa jinsi walivyo tayari kushirikiana na wengine katika kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na upendo badala ya kumezwa na vitu, ubinafsi pamoja na mipasuko.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anafarijika sana kuona kwamba, wanashirikiana kwa karibu sana na Patriaki Bartolomeo kwa kwanza; kwa kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya maendeleo endelevu yenye umuhimu wa pekee katika maisha ya watu kama: vile mapambano dhidi ya mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; ulinzi na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote; kutafuta, kulinda na kudumisha amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa kukubali kushiriki katika mkutano wa Sala kwa ajili ya kuombea Amani Mashariki ya Kati.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Julai 2018 atatembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, ili kusali na kutafakari juu ya mateso na mahangaiko ya Wakristo huko Mashariki ya Kati. Hawa ni waamini wanaolazimika kuyakimbia makazi na nchi yao kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wakuu wa Makanisa ya Kikristo wamekubali kushiriki katika tukio hili la maisha ya kiroho! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, matukio kama haya yataendelea kuongezeka siku kwa siku, ili kukuza na kudumisha uekumene wa huduma, sala sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya Kristo kwa watu wa Mataifa, kama sehemu ya mchakato wa umoja na neema ya Mungu inayowaunganisha! Mwishoni, Baba Mtakatifu ameushukuru ujumbe wa Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa uwepo wake na kwamba, kwa maombezi ya Watakatifu Petro, Paulo na Andrea Mtume, wawasaidie Wakristo wa Makanisa haya kuwa watangazaji waaminifu wa Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.