2018-06-28 08:56:00

Makardinali wapya 14 wanatumwa kutangaza upendo wa huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko anasema Makardinali wapya wanaosimikwa, tarehe 28 Juni 2018, Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Ireneo, Askofu na shahidi ni changamoto na mwaliko kwa Makardinali wapya kuwa ni kielelezo cha Kanisa la Kiulimwengu. Makardinali wapya wanatumwa kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu wenye huruma kwa watu wote wa Mataifa. Tangu sasa Makardinali wapya watakuwa ni sehemu ya wahudumu wa Jimbo kuu la Roma, kielelezo cha umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Makanisa mahalia yaliyoenea sehemu mbali mbali za dunia!

Kati ya Makardinali wapya, wawili ni wale ambao wamejipambanua kutokana na huduma yao kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema hawa ni: Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico pamoja na Kardinali Aquilino Bocos Merino, Padre wa Shirika la Waklareti. Makardinali, wakiendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake ni wasaidizi wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baraza la Makardinali kwa sasa linaundwa na Makardinali 228 kati yao 121 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Makardinali wamegawanywa katika Madaraja Makuu matatu: Kuna Makardinali: Maaskofu, Mapadre na Mashemasi yanayowawezesha kushirikiana kwa karibu sana na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake kwa Kanisa la Kristo!

Baraza la Makardinali ni mkutano muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa. Huu ni muda wa kufanya maamuzi makubwa na mazito, lakini kwa wakati huu ni kwa ajili ya kuwasimika Makardinali wapya, walioteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko. Katika Ibada hii, Makardinali wapya wanakiri Kanuni ya Imani na kula Kiapo cha Utii. Utambulisho wao ni mavazi mekundu, kielelezo cha ushuhuda wao kwa Kristo na Kanisa lake hata kiasi cha kumwaga damu yao! Wanavishwa pete ya Kikardinali, alama ya uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake pamoja na kupewa Kofia ya Kikardinali, alama ya umoja na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Desiré Tsarahazana wa Jimbo kuu la Toamasina, nchini Madagascar ndiye peke yake katika awamu hii anayeliwakilisha Kanisa Barani Afrika. Makardinali wengine ni kutoka: Iraq, Bolivia, Italia, Japan, Pakistan, Poland, Ureno, Perù, Mexico na Hispania. Majina ya Makardinali Wapya na mahali wanakotoka ni kama ifuatavyo:

Patriaki Louis Raphaël I Sako wa Kanisa Katoliki la Wacaldea wa Babeli (Iraq).

Kardinali Luis  Francisko Ladaria, Mwenyekiti Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, (Hispania).

Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma. (Italia).

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. (Italia).

Kardinali Konrad Krajewski, Mtunza Sadaka mkuu wa Kipapa. (Poland).

Kardinali Joseph Coutts, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Karachi. (Pakistani).

Kardinali António dos Santos Marto, Askofu wa Jimbo Katoliki la Leiria-Fátima (Ureno).

Kardinali Pedro Barreto, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Huancayo (Peru).

Kardinali Desiré Tsarahazana wa Jimbo kuu la Toamasina (Madagascar).

Kardinali Giuseppe Petrocchi Jimbo Katoliki la L’Aquila (Italia).

Kardinali Thomas Aquinas Manyo wa Jimbo kuu la Osaka (Japan).

Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Xalapa (Mexico).

Kardinali Toribio Ticona Porco, Askofu mstaafu wa Jimbo Jimbo la Corocoro (Bolivia).

Kardinali Aquilino Bocos Merino, Padre wa Shirika la Waklareti. (Hispania).

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.