2018-06-25 07:59:00

Mwenyeheri Sr. Maria Felicia: Mfano bora wa kuigwa na watawa na vijana


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 24 Juni 2018, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji amekazia kwa namna ya pekee kabisa matukio ya: furaha, mshangao na shukrani yaliyozunguka tukio zima la kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji. Amemshukuru Mungu kwa ajili ya Sr. Maria Felicia Guggiari Echeverria, kutoka Paraguay, aliyejisadaka kwa ajili ya wagonjwa, wazee na wafunga magerezani; akaboresha maisha yake ya kila siku kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, sasa ni Mwenyeheri.

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 23 Juni 2018, huko Asunciòn, Paraguay, amemtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Maria Felicia Guggiari Echeverria, kuwa Mwenyeheri. Wakati wa ujana wake, alijulikana kama “Chiquitunga” aliyesadaka maisha yake kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kiasi kwamba, kwake Kristo Yesu, alikuwa ni yote katika maisha yake. “Chiquitunga” alitamani kuyamimina maisha yake hata kiasi cha kumwaga damu kwa ajili ya Kristo. Hii ikawa ni dira na mwongozo wa maisha tangu ujana wake, hadi pale alipoitupa dunia mkono akiwa na umri wa miaka 34 tu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni changamoto kwa familia ya Mungu kutoka Paraguay, lakini zaidi kwa vijana wa kizazi kipya kutolea maisha yao kama sadaka safi inayompendeza Mungu na kutekeleza azma hii kwa moyo wa furaha na shukrani!

Kardinali Angelo Amato katika mahubiri yake anakaza kusema, hata wakati ule wa machafuko ya kisiasa nchini mwake, alijiweka tayari kusadaka maisha yake kwa ajili ya imani kwa Kristo na Kanisa lake. Haya ni maisha yaliyosimikwa katika upendo wa kidugu, ukarimu kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; maridhiano pale ambapo kulitokea tofauti katika mawazo na mitazamo ya maisha na hatimaye, msamaha ukawa ni nguzo ya maisha na utakatifu wake. Watu wengi walifurahishwa na ari pamoja na moyo wa huduma ulioneshwa na kushuhudiwa na Mwenyeheri Sr. Chiquitunga!

Hii ni huduma makini aliyoitekeleza si tu kwa kutenda, bali hasa kwa njia ya uwepo wake endelevu na makini, tayari kushirikiana na kushikamana na wengine kwa ajili ya huduma kwa watu. Wananchi wengi wanamkumbuka kutokana na huduma yake kwa: maskini, wagonjwa, wazee na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi hata cha kulinganishwa na Mama Theresa wa Calcutta, Mama na dada wa maskini. Katika utume wake, alikabidhiwa kufanya katekesi kwa watoto wadogo, akawafundisha upendo kwa maskini na kuwajali wanaoteseka kiroho na kimwili! Akawafundisha kuwatembelea wagonjwa na kuwafariji wafungwa.

Watu wengi, wakamwona Sr. Chiquitunga kuwa kweli ni Malaika mlinzi, aliyekuwa tayari kuwafariji wale waliovunjika moyo na kukata tamaa ya maisha. Watawa wenzake, wakamwona kuwa ni kimbilio na mfano bora wa kuigwa katika huduma, daima alikuwa tayari kusamehe na kusahau hata pale watawa wenzake walipomkosea na kumtenda mabaya. Kwao wote hawa, akaonesha tabasamu la kukata na shoka na uvumilivu mkuu!Alipofariki dunia, wale watawa waliokuwa wakimnyooshea kidole na kumpinga katika maisha yake, wakawa wa kwanza kububujika machozi ya huzuni na kuanza kushuhudia ile nguvu ya upendo iliyokuwa inatenda kazi ndani mwake.

Kardinali Amato anaendelea kudadavua kwa kusema, maisha ya Sr. Chiquitunga yaliboreshwa kwa matukio yaliyosheheni wema, huruma, upendo na unyenyekevu mkuu, chemchemi na maktaba ya utakatifu wa maisha. Sr. Maria Felicia  wa Yesu wa Sakramenti, alijitahidi kuishi Ubatizo wake kikamilifu, akajisadaka bila ya kujibakiza katika maisha ya kitawa na huduma makini kwa jirani zake. Kwa hakika, alikuwa kama Bikira Maria, Mtumishi wa Bwana! Alipenda kufanya kazi kama utimilifu wa utu na heshima ya binadamu; akatoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na mwaminifu kwa maisha na utume wake wa kitawa, daima mashauri ya Kiinjili yakiwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wake.

Mwenyeheri Sr. Maria Felicia  wa Yesu wa Sakramenti anaendelea kutoa changamoto kwa watawa wenzake kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili na sadaka safi inayompendeza Mwenyezi Mungu. Ni mwaliko kwa waamini wote kuambata na kukumbatia tunu msingi za maisha ya Kikristo, tayari kuzitangaza na kuzitolea ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kama kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Anawaalika watu wa Mungu, kumpatia Kristo Yesu nafasi katika maisha yao, ili kweli aweze kuwa ni taa inayoongoza mapito yao ya kila siku. Ushuhuda wa utakatifu unaiwezesha jamii kujikita katika utu wema, upendo, udugu na mshikamano wa dhati!

Mwenyeheri Sr. Maria Felicia  wa Yesu wa Sakramenti ni mfano bora wa utakatifu unaopata chimbuko lake kutoka Paraguay kwa ajili ya walimwengu wote. Ni mfano wa utakatifu hata kwa vijana wa kizazi kipya, kwa ari na moyo wake wa kutangaza na kushuhudia imani yake kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni kielelezo makini cha utekelezaji makini wa wito na utume wa maisha ya kitawa. Upendo na huruma yake kwa maskini na wagonjwa, ni mfano bora wa kuigwa katika kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu! Ni kijana na mtawa aliyejisadaka kwa ajili ya Kristo na huduma kwa jirani zake. Alibahatika kuvikwa taji ya huruma na upendo; unyenyekevu na ukarimu, kiasi hata cha kuomba msamaha pale alipokosewa na watawa wenzake.

Mwenyeheri Sr. Maria Felicia  wa Yesu wa Sakramenti, aliboresha maisha yake ya kiroho na utume kwa njia ya tafakari ya kina ya Neno la Mungu, hasa Agano Jipya, Biblia, ikawa ni Maktaba yake na mahali pa kujichotea hekima na busara ya maisha. Alikuwa ni mwaminifu sana kwa Mafundisho ya viongozi wa Kanisa; akasali na kufunga kwa ajili ya utakatifu wa maisha na wito wa Mapadre, kiasi hata cha kuacha mwongozo wa maisha na utume wa Kipadre ndani ya Kanisa Katoliki!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.