2018-06-23 16:00:00

Yaliyojiri kwenye mahojiano kati ya Papa Francisko na Wanahabari!


Uzoefu na mang’amuzi ya kutembea, kusali na kushirikiana; matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya; umuhimu wa kuwa na maandalizi makini kwa ndoa za mseto; changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuondokana na dhana ya vita halali na ya haki kwani vita haina macho wala pazia!  Haya ni kati ya mambo mazito yaliyojadiliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 21 Juni 2018 wakati akiwa njiani kurejea mjini Vatican baada ya kuhitimisha hija yake ya kiekumene, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Kardinali mteule Giovanni Angelo Becciu, ametumia fursa hii kuagana na waandishi wa habari, baada ya kuteuliwa kuwa Kardinali na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu.

Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa siku moja, ili kuwajuza walimwengu kile kilichokuwa kinajiri katika maadhimisho ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Anasema, kwake, hii ilikuwa ni siku nzito sana, lakini, anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kufanikisha tukio hili muhimu sana katika mchakato mzima wa majadiliano ya kiekumene. Anasema, ni siku ambayo imepambwa kwa: Sala na Ibada; kwa chakula na mazungumzo na hatimaye, kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya familia ya Mungu ndani na nje ya Uswiss.

Baba Mtakatifu anasema, kati ya mambo yaliyogusa undani wa moyo wake, ni ile nafasi ya kuweza kukutana na watu mbali mbali kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Amekutana na kuzungumza na viongozi wa Shirikisho la Uswiss, ambamo wamejadili kwa kina mapana masuala mbali mbali ya Jumuiya ya Kimataifa. Wakati wa chakula, wahusika wamepata nafasi ya kubadilishana mawazo, mang’amuzi na vipaumbele katika mchakato mzima wa majadiliano ya kiekumene. Viongozi mbali mbali wa Makanisa wameonesha wasi wasi wao kuhusu hatima ya vijana wa kizazi kipya kwa kulipongeza Kanisa Katoliki kutoa kipaumbele cha pekee, ili kusikiliza na kujibu kilio cha vijana wa kizazi kipya, katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana.

Maadhimisho ya Utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, yaliyofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 19 Machi hadi Jumapili ya Matawi. Vijana 315 na wengine 15, 000 walikuwa wanafuatilia tukio hili kwa njia ya mitandao ya kijamii, limewagusa sana viongozi wa Makanisa. Hii ni kwa sababu, maadhimisho haya yaliwakusanya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakiwa na imani, tamaduni na mapokeo yao, hapa kilichokuwa kinaangaliwa anasema Baba Mtakatifu ni matamanio ya vijana wa kizazi kipya! Kumbe, hii imekuwa ni hija ya kiekumene iliyomwezesha kutembea, kusali na kushirikiana na viongozi wa Makanisa katika kuziangalia changamoto mamboleo zinazoendelea kuibuliwa katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Maadhimisho ya Ndoa Mseto kati ya waamini wa Makanisa mbali mbali ya Kikristo anasema Baba Mtakatifu, yamefafanuliwa vyema na Sheria Kanuni za Kanisa na Maaskofu mahalia wamepewa dhamana na mamlaka ya kuangalia kila kesi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na ukuaji wa watoto. Hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, liliwasilisha ombi maalum kwa Kiti cha Kitume, ili kuangalia uwezekano wa waamini wenye Ndoa Mseto kuweza kushiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu. Askofu mahalia anasema Baba Mtakatifu anaweza kutumia busara na kuangalia kila kesi kwa jicho la kichungaji.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani kwa kuangalia changamoto za kichungaji nchini Ujerumani, kwa muda wa takribani mwaka mmoja, waliamua kuivalia njuga changamoto hii, ili hatimaye, kupata ushauri kutoka kwa Kiti kitakatifu. Maaskofu wakatoka na uamuzi kwamba, Sakramenti ya Ekaristi si kwa ajili ya waamini wote, bali wale wanaostahili kadiri ya Sheria kanuni za Kanisa. Na hapa Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni moyo wa Kikanisa, kwani mambo yanayoamriwa na Baraza la Maaskofu ni kwa ajili ya familia ya Mungu katika nchi husika! Kumbe, haya mambo hayamo katika Sheria kanuni za Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, baada ya kusoma na kujadiliana na viongozi wakuu wa Vatican, Kardinali mteule Luis Francisco Ladaria Ferrer kwa idhini ya Baba Mtakatifu akaliandikia Barua Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani akielezea kwamba, tema hii, bado ilikuwa inapaswa kuboreshwa zaidi, ili kupata ukomavu unaotarajiwa. Hati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani, itakuwa ni Mwongozo wa majadiliano ya kina kuhusu Ndoa Mseto.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, masuala mazito kama haya yanayogusa maisha na utume wa Kanisa yanajadiliwa na hatimaye, kutolewa uamuzi mkomavu! Maaskofu wa Majimbo wafanye tena rejea kuhusu Sheria na Kanuni za Kanisa kuhusu masuala haya! Baraza la Maaskofu linaweza kushughulikia masuala yanayohusu waamini wao na kuyapatia maamuzi, lakini hata Askofu Jimbo bado anayo dhamana na maamuzi halali Jimboni mwake.

Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itamwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na aina mbali mbali ya nyanyaso dhidi ya utu na heshima yao.

Baba Mtakatifu anaipongeza Italia na Ugiriki kwa kuwapokea na kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi. Huko Mashariki ya Kati, Uturuki imekuwa ni mfano bora wa kuigwa, kwa kupokea wakimbizi wengi kutoka Siria. Biashara haramu ya binadamu na viungo vyake ni kati ya hatari kubwa sana wanazokabiliana nazo wakimbizi na wahamiaji. Magereza yanayotunza wafabiashara haramu ya binadamu yanatisha sana, hali ambayo haijawahi kuonekana kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Viongozi wa Jumuiya ya Ulaya wanataka kupitia upya Mkataba wa Dublin unaotoa mwongozo wa kuchunguza wakimbizi na wahamiaji wanaoomba hifadhi ya kisiasa, ulinzi na usalama. Mkataba huu ulipitishwa kunako tarehe 15 Juni 1990; Ukafanyiwa marekebisho kunako mwaka  1997 na kupyaishwa tena mwaka 2003 na hatimaye, mwaka 2013 Mkataba wa III wa Dublin ukapitishwa. Nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zinasema kwamba, Mkataba huu una mapungufu makubwa kuhusu sheria ya hifadhi ya wakimbizi pamoja na utekelezaji wake.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, changamoto zote hizi zinaweza kupatiwa kisogo ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa itawekeza zaidi katika sekta ya elimu; kilimo ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya nchi inatumika kwa ajili ya mafao ya wengi. Lakini kwa sasa, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuivalia njuga changamoto ya wimbi kubwa na wakimbizi na wahamiaji ili kulipatia jibu muafaka! Kuhusu hali ya wakimbizi na wahamiaji nchini Marekani, Baba Mtakatifu Francisko anawaunga mkono kwa dhati kabisa na kukubaliana na sera zinazotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Marekani.

Jumuiya ya Kimataifa katika mwaka 2018 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 70 tangu Umoja wa Mataifa ulipochapisha Tamko Kuhusu Haki Msingi za Binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, vita, kinzani na mipasuko ya kidini ni matokeo ya kuporomoka kwa kanuni maadili na utu wema! Nchi nyingi zimeshindwa kutekeleza kwa vitendo Tamko la Haki Msingi za Binadamu. Kwa bahati mbaya sana, haki msingi za binadamu zinatafsiriwa kwa mwono binafsi, kiasi kwamba, hata amani linakuwa ni jambo la binafsi, hatari kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Dhana ya vita halali na ya haki imepitwa na wakati kwani, vita haina macho wala pazia! Kanisa kwa asili, maisha na utume wake anasema Baba Mtakatifu Francisko linapaswa kuwa ni chombo cha haki, amani na upatanisho. Leo hii amani ni changamoto pevu kutokana na kushamiri kwa biashara ya silaha duniani! Uchu wa mali na utajiri wa muda mfupi unawafumba watu macho kiasi cha kushindwa kuona mahitaji ya jirani zao. Kumbe, amani inafumbatwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru.

Injili ya Amani kadiri ya mpango wa Mungu inajikita kwenye majadiliano katika ukweli na uwazi; umoja na udugu; imani, matumaini na mapendo. Hata miongoni mwa Wakristo kuna waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani. Hawa ndio wale wanaoshahabikia vita. Baba Mtakatifu Francisko, amehitimisha mahojiano na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake huko Geneva, Uswiss kwa kusema, kwamba, kwa hakika, hii imekwa ni Siku ya Kiekumene. Umefika wakati wa kuondolea mbali “wongofu wa shuruti” kwa kujikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 
All the contents on this site are copyrighted ©.