2018-06-23 17:10:00

Baraza la Kipapa la Mawasiliano!


Kardinali mteule Giovanni Angelo Becciu, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican, katika mazungumzo aliyofanya na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 27 Februari 2018, kwa kuzingatia ushauri na maoni yaliyotolewa na Baraza la Makardinali Washauri, Baba Mtakatifu ameamua kwamba, kuanzia sasa na kuendelea, Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican, itajulikana kama Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Uamuzi huu utaanza kutekelezwa rasmi mara baada ya kuchapishwa kwenye Gazeti la L’Osservatore Romano na kwenye Nyaraka za “Acta Apostolicae Sedis.

Itakumbukwa kwamba, Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican ni sehemu ya mageuzi makubwa yanayofanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kuunganisha vyombo na taasisi zote za mawasiliano zilizokuwa chini ya Vatican, ili kuongeza nguvu katika mchakato mzima wa mawasiliano ndani ya Kanisa kwa kusoma alama za nyakati. Chini ya Baraza la Kipapa la Mawasiliano kuna: Vatican Media inayounganisha: Kituo cha Televisheni cha Vatican, CTV; Radio Vatican pamoja na Gazeti la L’Osservatore Romano. Vyombo vyote hivi kwa kushirikiana na kushikamana katika mchakato mzima wa kuandaa na hatimaye kurusha matangazo yake, kwa pamoja wanaunda “Vatican News! Yaani mtandao wa Habari kutoka Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.