2018-06-22 09:47:00

Papa Francisko aishukuru familia ya Mungu Uswiss kwa moyo wa ukarimu


Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Palexpo, mjini Geneva, Ahamisi, tarehe 21 Juni 2018 amemshukuru kwa  namna ya pekee kabisa, Askofu Charles Morerod wa Jimbo Katoliki la Lausanne, Geneva na Frisbourg, kwa ukarimu, maandalizi na sala na kwamba, anapenda familia ya Mungu nchini Uswiss kukuza na kudumisha moyo huu. Baba Mtakatifu amewahakikishia uwepo wake wa daima kwa njia ya sala katika hija hii ya kiekumene. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kuwashukuru Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini Uswiss, Mapadre bila kuwasahau waamini waliotoka ndani na nje ya Uswiss ili kuhudhuria tukio hili la kihistoria, Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapoadhimisha Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwake.

Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini wa mji wa Geneva kwamba, takribani miaka 600 iliyopita, Papa Martino V alipata nafasi ya kutembelea mjini humu. Geneva ni makao makuu ya Mashirika ya Kimataifa na kati yake ni Shirika la Kazi Duniani, ILO, ambalo mwaka 2019 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, ukuaji hafifu wa uchumi kitaifa na kimataifa pamoja na hupatikanaji wa kazi zenye staha na zinazoheshimu utu na heshima ya binadamu ni kati ya changamoto endelevu kwa Shirika la Kazi Duniani. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii pia kuishuruku Serikali ya Shirikisho la Uswiss kwa mwaliko na ushirikiano mkubwa waliouonesha katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.