2018-06-21 17:55:00

Hija ya Kiekumene ya Papa Francisko yawasha moto wa kiekumene Geneva!


Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi 21 Juni 2018 ameanza hija yake ya kitume ya 23 kimataifa, huko Geneva, Uswiss. Ni hija inayojikita zaidi katika mchakato wa kiekumene, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutembea, kusali na kushirikiana”. Hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 70 tangu kuanzishwa kwa Baraza la Makanisa Ulimwenguni. Kabla ya kuanza hija hii, kama kawaida yake, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano jioni, alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu na kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi, kadiri ya taarifa iliyotolewa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican.

Akiwa njiani, kuelekea nchini Uswiss, Baba Mtakatifu Francisko amemtumia Rais Sergio Mattarella wa Italia, ujumbe wa matashi mema, huku akimshirikisha kwamba, anakwenda mjini Geneva ili kukutana na Jumuiya ya Wakatoliki nchini Uswiss, lakini kwa namna ya pekee kabisa, anataka kuchochea majadiliano ya kiekumene na Makanisa mbali mbali ya Kikristo. Baba Mtakatifu anamtakia heri na baraka, Rais Mattarella na familia ya Mungu nchini Italia, ustawi na maendeleo: kiroho na kimwili na hatimaye, amewapatia baraka zake za kitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.