2018-06-20 09:30:00

Siku ya Maskini Duniani 2018: Maskini huyu aliita, Bwana akasikia!


Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Mwaka wa Huruma ya Mungu. Siku hii kwa mwaka 2018 inaadhimishwa Jumapili ya XXIII ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa ambayo kwa Mwaka huu itakuwa ni tarehe 18 Novemba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Maskini huyu aliita, Bwana akasikia”. Zab. 34: 6 (Katika Biblia ya Kiswahili). Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Siku ya Pili ya Maskini Duniani kwa mwaka 2018 anakazia mambo makuu matatu: Kilio, Kujibu na Kuokoa.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Uinjilishaji mpya, akiwa ameambatana na Monsinyo Graham Bell, Katibu mkuu msaidizi, hivi karibuni, wamezindua ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Siku ya Pili ya Maskini Duniani. Kilio, Kujibu na Kuokoa ni maneno yanayohitaji tafakari ya kina, ili hata waamini nao waweze kuchukua hatua makini katika kupambana na baa la umaskini. Ni fursa ya kusikiliza kwa makini kilio cha maskini na kukipatia majibu muafaka.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini wote kuungana pamoja na Mwenyezi Mungu,  ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Mungu ili kusikiliza kilio cha maskini kwa kuwaokoa na kuwajengea uwezo wa kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya kijamii. Hata leo hii kuna maskini wanaojitambulisha kama akina: Bartimayo kipofu, aliyepaaza sauti yake, kiasi hata cha kumfikia Yesu, akamponya upofu wake, akapata kuona tena. Hata leo hii pia kuna watu ambao hawana: fursa za ajira wala fedha ya kutosheleza mahitaji yao msingi na matokeo yake, wengi wao wanatumbukizwa kwenye utumwa mamboleo! Wote hawa bado wanayo matumaini ya mtu anayeweza kuwaambia !Jipe moyo; inuka, anakuita!

Askofu Fisichella anasema, Siku ya Maskini Duniani ni mwaliko kwa Kanisa na waamini katika ujumla wao, kujibu kilio cha maskini kwa vitendo! Ni mwaliko wa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu Francisko anafafanua aina mbali mbali za umaskini na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayeweza kutengwa na huruma pamoja na upendo wa Mungu. Kwa bahati mbaya, mali na utajiri wa ulimwengu huu, unawapofusha watu wengi, kiasi cha kujifungia katika ubinafsi wao. Kilio cha maskini kijenge utamaduni wa kusikiliza na kujibu kwa njia ya kukutana na watu.

Kwa kawaida maskini ni watu wa kwanza kuonja na kutambua uwepo wa Mungu katika maisha yao, kiasi hata cha kuweza kutolea ushuhuda wa maisha yao, hata nyakati za giza na usiku mnene, daima atawakirimia upendo na faraja yake. Lakini, ili kuweza kupata ukombozi wa kweli, kuna haja ya kuwepo na watu ambao  wataweza kujisadaka kuwasikiliza, kwa kuwafungulia malango ya nyoyo na maisha yao, ili kuwawezesha kujisikia kuwa ni marafiki, ndugu na jamaa. Kwa njia hii watawaweza kuonja nguvu inayokoa na kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa.

Huu ni ujumbe wa matumaini unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko anasema, Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella. Maskini wanaomlilia na kumtafuta Mungu katika maisha yao, atawajibu kwa wakati muafaka; atawaokoa na kuwajalia maisha tele! Siku ya Maskini Duniani inaadhimishwa kwa kutana na jirani. Jumapili tarehe 18 Novemba 2018 atakutana na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na vyama na mashirika ya kitume yanayojihusisha kwa namna ya pekee na huduma kwa maskini. Baba Mtakatifu atashiriki chakula cha mchana na maskini 3, 000. Chakula hiki kimeandaliwa kwa hisani ya “Rome Cavalieri-Hilton, Italia” kwa kushirikiana n ana taasisi ya “Ente Morale Tabor. Tukio kama hili litafanyika pia parokiani na kwenye vituo mbali mbali vya kuhudumia maskini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko Siku ya Maskini Duniani, itaadhimisha kama chemchemi ya furaha: kwa kusali pamoja, kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa baadaye kushirikishana chakula cha mchana.

Jumamosi, tarehe 17 Novemba 2018 kutakuwa na mkesha wa sala kwenye Kanisa kuu la “Mtakatifu Lorenzo Fuori le mura”. Kwa muda wa Juma zima yaani kuanzia tarehe 12- 18 Novemba 2018 katika Uwanja wa Pio wa XII, kutawekwa hema kwa ajili ya huduma ya afya. Mwaka 2017 wagonjwa 600 waliweza kupima afya zao na kupatiwa tiba. Huduma hii itatolewa bure na Madaktari kutoka Vatican, Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Gemeli pamoja na Chuo Kikuu cha Tor Vergata. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella anavialika vyama na mashirika ya huduma kwa maskini, kuhakikisha kwamba, wanawapeleka maskini ili waweze kupata huduma hii. Kilio cha maskini ni ujumbe unaogusa wote ndani na nje ya Kanisa. Watu wajibidishe kufahamu mahitaji msingi ya maskini na kuwasaidia kwa njia ya mshikamano wa upendo katika Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.