2018-06-20 16:27:00

Sherehe ya Kuzaliwa kwa Yohane Mbatizaji!


Leo Jumapili tarehe 24 Juni 2018, Kanisa latualika tusherehekee sikukuu ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji. Katika Lk. 1:13-14 tunasoma neno hili – lakini malaika akamwambia, usiogope, Zakaria, sala yako imesikilizwa. Elizabeti, mke wako, atakuzalia mwana, naye umwite Yohane.  Kadiri ya Bilblia, mtu ni yule anayefahamika na Mungu, ni yule ambaye Mungu anamwita kwa jina. Na tunaamini kuwa Mungu anatujua tangu kutungwa mimba. Katika Zaburi ya 119 .. tunasoma neno hili – ‘maana wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu, uliniunga tumboni mwa mama yangu .....nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa. Na nafsi yangu yajua sana’. Katika somo la kwanza toka nabii Isaya tunasoma ‘habari ya mtumishi wa Bwana aliyeitwa na Mungu tangu tumboni mwa mama yake, yaani Isaya’.

Sayansi yazungumzia kiumbe kama ule ukuaji wa chembechembe – embryo – hai ambayo itakakamilika na kujulikana pole pole kadiri ya muda na wakati. Imani inaongeza hapa – siyo kitu kisichojulikana ila ni kitu ambacho kiko katika mpango wa upendo wa Mungu wa uumbaji. Kwa mfano wito wa utume wa Yohane ulijulikana tangu mwanzo – ‘nawe mtoto utaitwa nabii wa Mungu aliye juu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake’. Kanisa linatambua kuwa Yohane alibarikiwa tayari katika tumbo la mama yake katika Kristo. Hapa kuna tofauti ya uelewa kati ya sayansi na imani yetu. Ndiyo maana kanisa husherehekea kuzaliwa kwake Yohane mbatizaji.

Katika adhimisho la kumbukumbu, sikukuu au sherehe ya mtakatifu, kanisa huadhimisha siku ya kifo chake, ndiyo siku ya kuzaliwa kwake kwake mbinguni. Ila siyo kwa Bikira Maria na Yohane mbatizaji. Wengine wote, tangu kuzaliwa tuna yale madoa ya dhambi ya asili, hivyo hatumpendezi Mungu. Katika Mt. 11:10-12 tunasoma neno hili – ‘amin, nawaambieni, katika wote waliozaliwa na mwanamke hajapata kutokea mtu aliye mkubwa kuliko Yohane Mbatizaji. Lakini katika ufalme wa mbingu, mdogo wa mwisho ni mkubwa kuliko yeye. Tangu siku za Yohane Mbatizaji hata sasa, ufalme wa mbingu hupatikana kwa juhudi tu, nao wenye juhudi ndio wanaonyakua’. Bikira Maria tangu kuzaliwa kwake alikingiwa dhambi ya asili. Ndiyo maana tunasherehekea kuzaliwa kwake. Yohane alipata upendeleo wa Mungu. Alizaliwa bila dhambi ya asili. Ndiyo maana tunasherehekea kuzaliwa kwake tofauti na watakatifu wengine.

Mtakatifu Agostino anasema, ‘ukiacha sherehe ya Noeli, yaani kuzaliwa kwake Bwana na Yohane Mbatizaji, Kanisa linasherehekea yule aliyetukuzwa (watakatifu) baada ya kushinda mahangaiko ya dunia, yaani siku yake ya ushindi hapa ulimwenguni. Hufanyiwa sherehe baada ya ushindi. Kwake Yohane Mbatizaji, tangu siku ya kwanza kwake ni takatifu. Bwana wetu Yesu Kristo alitangaza kuja kwake kupita kwake Yohane. Bwana wetu hakupenda kuja bila kujulikana. Yohane anawakilisha Agano Jipya na sheria. Hivyo, anamtangulia mkombozi, kama vile sheria ilivyotangulia na kuacha njia kwa ujio wa neema’.

Hakika sherehe ya kuzaliwa Yohane Mbatizaji ni utangulizi wa sherehe ya kuzaliwa Bwana, sherehe ya Noeli. Kwa ujumla katika kipindi kizima cha mwaka tunaadhimisha mafumbo makuu mawili: Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Ukombozi. Fumbo la Umwilisho hugusa moja kwa moja moyo wa mtu. Fumbo la ukombozi, yaani pasaka yote huadhimishwa toka Kwaresima mpaka Pentekoste na katika kila jumapili ya mwaka sababu kila adhimisho la dominika ni adhimisho la Pasaka. Yohane alikuwa ni mwanga unaowaka na kumulika. Katika adhimisho hili nasi tunaalikwa kuwa taa iwakayo ili tuweze kuwa ile njia na kuonesha njia kwa wengine. Yohane mwenyewe hakusikia ile sauti toka tumboni mwa mama yake. Aliitambua baada ya kutolea maisha yake kumtangaza mtangulizi wake. Hata sisi, Mungu anatuita toka tumboni mwa mama zetu. Tukimwamini basi tutaweza kumtambua vizuri na kumtangaza kwa wengine.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre. Reginald Mrosso, C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.