2018-06-18 09:20:00

Siku ya Wakimbizi Duniani 2018: Onesheni huruma, ukarimu na upendo!


Siku ya Wakimbizi Duniani inayoadhimishwa tarehe 20 Juni kila mwaka, ilianzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2000 kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mkataba wa utambuzi wa hadhi ya wakimbizi ulipotiwa mkwaju kunako mwaka 1951, baada ya Jumuiya ya Kimataifa kujionea athari za Vita kuu ya Pili ya Dunia. Siku hii ikaanza kuadhimishwa rasmi mwaka 2001.Takwimu zinaonesha kwamba, leo hii kuna idadi kubwa zaidi ya wakimbizi kuliko wakati mwingine wowote wa historia ya mwanadamu.

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 17 Juni 2018, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ameyaelekeza mawazo yake kwenye Siku ya Wakimbizi Duniani kwa mwaka 2018. Umoja wa Mataifa ulianzisha Siku hii ili kuwashirikisha watu mateso na changamoto wanazokabiliana nazo wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Ni watu wanaokimbia vita, dhuluma na nyanyaso. Maadhimisho haya kwa mwaka huu, yanaangukia wakati ambapo viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaendelea kushauriana kuhusu “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018”.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wataweza kufikia muafaka, ili kuweza kuwa na mfumo wa uhamiaji wenye usalama, unaoratibiwa na kuzingatia sheria kanuni. Dhamana hii inapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia utu na uwajibikaji; huduma na ulinzi kwa watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha moyo wa upendo na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji. Iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana; kutambua na kuthamini mchango wao katika uzalishaji na huduma; ili hata wao, waweze kujizatiti ili hatimaye, kujishikamanisha na jumuiya zinazowakaribisha. Katika mchakato kama huu, Baba Mtakatifu anasema, kuna suluhu ya changamoto, matatizo na fursa zinazotokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani.

Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018  unaondaliwa na Umoja wa Mataifa unalenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Umuhimu wa Jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na maisha bora zaidi. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa wahamiaji unapania pamoja na mambo mengine, kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na wakimbizi kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa.

Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao pamoja na  uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi. Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unapania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa baadhi ya serikali pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika kuzalisha na kutoa huduma, mwishoni ni suala la udhibiti wa mipaka!

Kanisa Katoliki katika sera na mikakati yake kuhusu huduma kwa wakimbizi na wahamiaji linapenda kukazia kwa namna ya pekee umuhimu wa: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowakirimia. Baba Mtakatifu Francisko, tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameguswa sana na matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni watu wanaokimbia vita, dhuluma, nyanyaso, majanga asilia na umaskini, changamoto na mwaliko kwa familia ya binadamu kusoma alama za nyakati!

Katika mchakato wa kukabiliana na changamoto hizi, Baba Mtakatifu ameanzisha kitengo maalum cha wakimbizi na wahamiaji katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya binadamu, ambacho kinawajibika moja kwa moja kwake, kama kielelezo makini cha huduma ya mshikamano wa Kanisa na wakimbizi, wahamiaji, watu wasiokuwa na makazi pamoja na waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaobisha hodi kwenye malango ya watu mbali mbali duniani, ni nafasi muhimu sana ya kuweza kukutana na Kristo Yesu, ambaye anajitambulisha kama mkimbizi na mhamiaji anayekataliwa na kubezwa na watu wa nyakati mbali mbali.

Mama Kanisa anapenda kuwaonesha upendo wake wa dhati, wakimbizi na wahamiaji, katika hatua mbali mbali za safari yao, tangu wanapoondoka, wanapofika na hatimaye, kurejea tena makwao hali inaporuhusu. Waamini wakishirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, wanaalikwa kuyavalia njuga matatizo na changamoto zinazowakabili wakimbizi na wahamiaji, kwa kuwaonesha moyo wa ukarimu, hekima na busara, kila mmoja kadiri ya uwezo na nafasi yake. Lakini, wote kwa pamoja wanaweza kujibu kilio na changamoto hizi kwa kujikita katika mchakato unaofumbatwa katika mambo makuu yafuatayo yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika uhalisia wa maisha ya watu wanaowakirimia.

Kutokana na mwelekeo wa ubaguzi, wasi wasi pamoja na kukosa imani na vyombo vya ulinzi na usalama kuhusu hatima yao, mara nyingi wakimbizi na wahamiaji wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo na kazi za suluba, mambo yanayo dhalilisha utu na heshima yao kama binadamu pamoja na haki zao msingi. Ni watu wasiojulikana kisheria na matokeo yake, hawawezi kuheshimiwa wala kuthaminiwa hata kidogo!

Kuna umuhimu wa Serikali husika kulinda mipaka ya nchi yake na kuratibu wimbi la wakimbizi na wahamiaji, lakini pia inapaswa kuwa na mfumo bora wa sheria unaoratibu na kusimamia shughuli za wakimbizi na wahamiaji kwa kuzingatia: utu wao kama binadamu na haki zao msingi, kipaumbele cha kwanza wakiwa ni wanawake, watoto na wazee. Hapa sheria, mikataba na itifaki za kimataifa hazina budi kuzingatiwa na vyombo vya sheria katika nchi husika.

Pili kuna haja ya kukazia sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutumiwa kama njia halali za uhamiaji badala ya kuendekeza sheria na taratibu ambazo si rafiki sana kwa utu na heshima ya binadamu! Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kushughulikia changamoto ya wakimbizi na wahamiaji katika misingi ya ukweli na uwazi, kwa kuongeza fursa ya watu kupata vibali halali vya uhamiaji hali ambayo inaweza pia kuchangia uhusiano mwema na jumuiya mahalia, mambo yanayosimikwa katika utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kama ndugu badala ya kujenga hofu zisizo na mashiko dhidi ya wahamiaji, hali inayochangia ubaguzi, nyanyaso na dhuluma dhidi ya wakimbizi na wahamiaji duniani. Usalama, utu na mahitaji msingi ni mambo ambayo yanatiliwa mkazo na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu wakimbizi na wahamiaji duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.