2018-06-18 15:52:00

Changamoto ya Wahamiaji Duniani: Maendeleo, Usalama na Mawasiliano


Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi, wahamiaji na maendeleo endelevu imeendelea kupewa kipaumbele cha pekee kati ya Vatican na Mexico tangu mwaka 2014, kiasi kwamba, hata mwaka 2018, pande hizi mbili, zimeamua kwa mara nyingine tena kujadiliana kwa kina na mapana, lakini kwa kujikita katika mambo makuu matatu. Mosi: Maendeleo na athari za Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji, 2018 “Global Compact 2018”. Pili, Uhamiaji na maendeleo mintarafu Mkataba huu wa Kimataifa. Tatu: Uhamiaji na vyombo vya mawasiliano katika mwanga wa Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa wahamiaji. Baada ya majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi, Vatican na Mexico, kwa pamoja wametoa tamko rasmi!

Wajumbe wanakiri kwamba, wakati wa majadiliano yao, wametiwa shime na Baba Mtakatifu Francisko kujizatiti zaidi katika dhamana hii kwa kuongeza nguvu, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuwa na uwajibikaji wa pamoja katika kushughulikia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Sera na mikakati itakayoibuliwa inapaswa kuzingatia kwa namna ya pekee kabisa: haki, mshikamano na huruma. Lengo ni kuanzisha mchakato wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuweza: Kuwapokea, Kuwalinda, Kuwaendeleza na Kuwahusisha” wakimbizi na wahamiaji katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwakirimia.

Serikali ya Mexico inapenda kuhakikisha kwamba, inatekeleza dhamana na wajibu wake, ili Mkataba wa Kimataifa usaidie uhamiaji kuwa ni: Salama, Unaodhibitiwa na kufuata sheria na kama chombo cha kuleta mageuzi kutoka katika mwono finyu wa watu kutaka kujiangalia wenyewe na kuanza mchakato wa ujenzi wa mwono mpana zaidi unaosimikwa katika utu na heshima ya binadamu. Kwa upande wake, Kanisa Katoliki, katika sera na mikakati yake ya huduma za kichungaji kwa wakimbizi na wahamiaji, linataka kujikita zaidi katika: Kuwapokea, Kuwalinda, Kuwaendeleza na Kuwahusisha” ili kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana.

Haya ni mambo msingi yaliyobanishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018. Wajumbe wanatambua changamoto changamani zinazosababishwa na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani. Wengi wao ni watu wanaokimbia: vita, majanga asilia, baa la umaskini pamoja na kutafuta maisha bora zaidi na fursa za kujiendeleza. Waathirika wakubwa wa wimbi la wakimbizi ni watoto!

Changamoto hii inaweza kujibiwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuzingatia: mshikamano, kanuni auni na uwajibikaji wa pamoja. Utu na heshima ya binasamu vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza kwa watu wote wale wanaolazimika kuzikimbia nchi zao. Mexico na Vatican zinataka kushikamana ili kuwepo na uwezekano wa kuanzisha uongozi wa kimataifa kuhusu wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, kwa kuwahusisha wadau mbali mbali. Lengo ni kuwezesha mchakato wa uhamiaji unakuwa ni: Salama, Unaodhibitiwa na Kufuata sheria kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wote wanaohusika sanjari na kuunda mazingira yatayowezesha watu kuona kwamba kuhama ni jambo la kawaida na wala si shinikizo kutokana na sababu mbali mbali. Pande hizi mbili, zitaendelea kushirikiana na kushikamana ili kuhakikisha kwamba Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji unafikia malengo yake; kwa kuwa salama, kwa kudhibiti na kuzingatia sheria.

Kwa hakika, wimbi kubwa la wakimbizi ni changamoto changamani, lakini pia ni fursa muhimu ya kuweza kuweka uwiano bora zaidi kati ya Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji na Mkataba wa Wahamiaji Duniani. Mexico na Vatican zitaendelea kujibidisha ili kuhakikisha kwamba kunakuwepo na hali na mazingira rafiki yatakayosaidia kutajirisha jamii zinazowapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji, ili nao pia waweze kuchangia katika mchakato wa maendeleo endelevu katika ngazi mbali mbali. Mwishoni, wajumbe hawa wamevitaka vyombo vya mawasiliano ya jamii kusaidia kadiri ya uwezo na nafasi zao, kusambaza habari zenye uhakika kuhusu wimbi la wakimbizi duniani. Wanasikitishwa sana na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyopotosha umma kwa kutoa taarifa tenge kuhusu wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.