2018-06-16 06:30:00

Ufalme wa Mungu unapata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka!


Utangulizi: Kristo Bwana wetu kwa kuyatimiza mapenzi ya Baba ameanzisha ufalme wa Mungu. ufalme ambao ujio wa utawala wake unatekelezwa kwa fumbo la Pasaka; mateso, kifo chake Msalabani na ufufuko wake. Naye anasema “Nami nikiinuliwa juu ya nchi nitawavuta wote kwangu” (Yoh. 12:32). Watu wote wanaitwa kuingia katika ufalme huu, ndio maisha ya muungano na Mungu, maisha ya uwepo wa Mungu na maisha ya uendelezaji wa tunu za kimungu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu.

Masomo kwa ufupi: Somo la kwanza: (Ez. 17:22-24) ni unabii wa Nabii Ezekieli katika kipindi cha kihistoria ambacho Waisraeli walikuwa utumwani Babiloni. Wakiwa huko waliona Mungu amewaacha kabisa na hata ile ahadi yake ya kuusimika milele utawala wa mfalme Daudi haitatimia. Kinyume cha mawazo yao hayo, nabii Ezekieli anatoa unabii wa matumaini kwao, unabii wa matumaini kuwa Mungu atauinua tena ufalme kati yao. Katika somo hili tuliolisikia nabii anatumia lugha ya picha ya kitawi kidogo mororo cha mwerezi ambacho Mungu mwenyewe atakitwaa na kukipanda juu ya mlima mrefu ulioinuka sana. Kitawi ambacho kitatoa matawi makubwa na chini yake watakaa ndege wa kila namna. Ndio ufalme atakaouinua kati yao, ufalme ambao utatoa hifadhi kwa wote wanaoukimbilia.

Somo linaongeza kuwa ufalme ambao Mungu atauinua ni ufalme ambao utamtukuza Yeye mwenyewe kati ya falme zote. Anasema “Na miti yote ya mashamba itajua ya kuwa mimi, Bwana nimeushusha chini mti mrefu na kuuinua mti mfupi”.Ufalme anaoutolea unabii Nabii Ezekieli katika somo hili ni ufalme wa uzao wa Daudi ambao utachanua tena katika Israeli baada ya kuangushwa na wao kupelekwa utumwani. Hii pia ni alama inayodokeza ufame ambao utakamilika kwa ujio wa Kristo Masiha anayekuja kuanzisha ufalme halisi wa Mungu.

Somo la pili (2Kor. 5:6-10) ni sehemu ya kifungu kipana ambacho Mtakatifu Paulo anaeleza sababu ya kuwafanya wanaomwamini Kristo kusonga mbele licha ya magumu mbalimbali wanayokutana nayo katika utume na katika maisha yao. Baada ya kuwa ameelezea “roho ya imani” hapo awali, katika somo la leo anaongeza na kusema kuwa tumaini la kuwa na Bwana baada ya maisha ya hapa duniani ni sababu nyingine inayowafanya wanaomwamini Kristo kusonga mbele licha ya magumu mbalimbali. Anasema kuwa wanaomwamini Kristo wawapo hapa duniani katika hali ya kimwili wapo mbali na Bwana, ni wageni na wahujaji wasio na makazi ya kudumu. Makazi yao ya kudumu ni uwinguni na huko ndiko watakuwa na ukamilifu wa uwepo wao na Kristo wanaye mtumikia hapa duniani.

Hili ni tumaini kama analokuwa msafiri yoyote ambaye akishaweka mawazo yake yote katika lengo la safari yake, yaani kufika mahala anapokusudia, anakuwa tayari kuvumilia adha safarini, uchovu wa mwili, wakati mwingine njaa na hata uchakavu wa barabara na chombo cha usafiri anachotumia. Mawazo yake yote yanakuwa ni juu ya hatima ya safari yake. Mtume Paulo katika somo hili la pili anaweka hatima ya maisha ya mkristo kama sababu ya kutokukata tamaa na kama sababu ya kumfanya mwanadamu azidi kusonga mbele katika changamoto mbalimbali anazokutana nazo.

Injili (Mk.4:26-34) ni mafundisho ya Yesu kuhusu ufalme wa Mungu. Yesu amekuwa akifundisha kwa mifano katika mambo mbalimbali. Lakini mifano ya injili ya leo ni mifano inayogusa mojakwamoja ufalme wa Mungu na inaitwa mifano ya ufalme. Anaanza “nifaufananisha na nini ufalme wa Mungu?” Katika mfano wa kwanza, mfano wa mbegu na mpanzi ambapo mbegu inakua pasipo mpanzi kujua muda, wakati na namna ya ukuaji Yesu anakusudia kueleza namna ya ukuaji wenyewe wa ufalme wa Mungu. kwamba ufalme huo hukua kwa wakati wake, kwa namna yake na hata kwa kasi yake ambayo si lazima iwe kadiri ya mapenzi ya mwanadamu au ulimwengu.

Katika mfano wa pili Yesu anaeleza asili ya ufalme wenyewe; asili si kwa maana ya chanzo bali kwa maana ya namna (natura). Nayo ni kwamba ufalme wa Mungu kwa asili huwa na mwanzo hafifu au mwanzo wa kawaida kabisa. Na hatua kwa hatua hukua hadi kufikia kama anavyoelezea Yesu kutoka udogo wa punje ya haradali hadi ukubwa wa mti ambao ndege wa angani wanaweza kukaa chini ya uvuli wake.

Tafakari: Ndugu msikilizaji na msomaji wa Vatican News katika dominika hii ya 11 ya mwaka B wa Kanisa, MaandikoMatakatifu yanaangaza tafakari yetu juu ya ufalme wa Mungu. ufalme ambao watu wote wanaalikwa kuuingia na ambao sisi kwa ubatizo wetu tumeupokea na tunajitahidi kuuishi na kuuakisi kila siku ya maisha yetu. Kutokana na mafundisho ya Yesu mwenyewe tunapata kufahamu kuwa kuwa ndani ya ufalme wa Mungu ni kuishi katika uwepo wa Mungu; ni kuishi tukijua kuwa tumo ndani ya himaya ya Mungu; tupo ndani ya uongozi wa nguvu ya mkono wake. Kumbe tunapotafakari leo kuhusu ufalme wa Mungu tunaalikwa kufakari kwa kina juu ya uwepo wa Mungu katika maisha yetu; kuhisi uwepo huo unaotuzunguka. Lakini, Je, ni kwa nini wakati mwingine nahisi Mungu yuko mbali namimi? Najiona niko mtupu na niliye mbali na mkono wa ulinzi wake? Na tena ni kwa nini sasa wakati mwingine ufalme huu wa Mungu unaonekana kumezwa labda na “falme” nyingine za kidunia kiasi ambapo nguvu yake haionekani waziwazi kama tunavyotegemea? Na tena ni kwa nini tunaona kana kwamba ufame huu unachelewa kuwafikia na wengine ili wayajue ayatakayo Mungu kama sisi tujuavyo?

Kama walivyoweka bayana manabii wa kale na kwa namna ya pekee nabii Ezekieli katika masomo ya leo, uwepo wa Mungu haumwachi kamwe mwanadamu. Ni mwanadamu anayeweza kuwa haoni au hata hauhisi uwepo huo ila Yeye mwenyewe anatuhakikishia kuwa hatuachi kamwe. Ahadi ya Mungu ya kuusimika milele ufalme wa Daudi haikufa hata mara moja bali hatua kwa hatua Mungu alizidi kuikuza na kuikamilisha kwa ujio wa Kristo aliyepewa jina pia la Mwana wa Daudi.

Kuuishi uwepo wa Mungu katika maisha ni namna ambayo waalimu wa maisha ya kiroho wanatuambia inakuza maisha ya kiroho ya mwamini. Mtu anakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kukua kiroho, pamoja na njia nyingine, kwa kuuishi uwepo wa Mungu katika maisha yake. Na hapa sio tu kumuona Mungu katika wale wanaomzunguka au katika hali za maisha alizomo bali hasa kuona kuwa jicho la Mungu na mkono wake wenye nguvu viko naye katika kila hatua ya maisha: katika kila ayawazayo, kila ayasemayo na kila ayatendayo. Mwanadamu hawezi kwa yeye mwenyewe kusema sasa anakuwa kiroho. Na hata anapokua, jinsi ya ukuaji wake kiroho hawezi kuufafanua. Maana yeye akishaipokea mbegu ya imani, ukuaji wake kiroho na kipimo chake anacho Mungu mwenyewe. Juhudi yake ndiyo kuipokea imani na kujiweka daima chini ya maongozi yake kama alivyofundisha Kristo mwenyewe, kusali “Baba ufalme wako ufike, utakalo lifanyike duniani kama mbinguni”.

Padre William Bahitwa.

VATICAN NEWS.








All the contents on this site are copyrighted ©.