2018-06-12 11:00:00

KOMBE LA DUNIA 2018: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu


Mama Kanisa anatambua na kuthamini kwamba, michezo ni nyenzo muhimu sana katika kusimamia haki msingi za binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Michezo ni muhimu sana katika ujenzi wa jamii na ushiriki mkamilifu katika kudumisha: haki, amani na utulivu bila vita, kinzani na mipasuko ya kijamii. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kuendelea kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa njia ya michezo, umuhimu wa kujikita katika urafiki, udugu na haki, mambo muhimu sana katika ulimwengu mamboleo.

Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni katika uzinduzi wa Waraka wa “Dare il meglio di se”, yaani “Kujitoa Kikamilifu”: Mtazamo wa Kikristo kuhusu michezo na binadamu” uliochapishwa na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, michezo ni mahali pa kuwakutanisha watu katika ngazi mbali mbali, ili kufikia lengo maalum. Michezo ni kiungo maalum cha majiundo na tunu msingi za maisha ya kiutu. Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha: ukarimu, unyenyekevu, sadaka, udumifu, furaha, kila mtu akijitahidi kuchangia kadiri ya uwezo na karama zake, kielelezo makini cha ujenzi wa umoja na mshikamano unaobomolea mbali tabia ya ubinafsi na uchoyo.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, michezo katika mtazamo wa Kikristo ni njia ya utume na mchakato wa utakatifu wa maisha. Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ni Sakramenti ya wokovu; ni mtangazaji wa Habari Njema na shuhuda wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Michezo katika nafasi  mbali mbali ni jukwaa la kutangaza na kumshuhudia Kristo kwa walimwengu. Ni wakati wa kuwashirikisha wengine, ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Michezo ni wakati muafaka wa kuonja: uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji kwa kukutana na watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Wanamichezo wa kweli ni wajumbe na mashuhuda wa Kristo Mfufuka wanapokuwa uwanjani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, hata wanamichezo wanaweza kuwa ni watakatifu, kwani daima wanaitwa na kuhamasishwa kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao kila kukicha!

Michezo inapania kujenga na kuimarisha urafiki na udugu kati ya watu; maelewano na amani; kuheshimiana, maridhiano na utulivu kwa kuthamini tofauti zinazojitokeza kati ya watu. Tunu msingi za michezo zinapaswa kusisitizwa miongoni mwa vijana na watoto, ili kuwasaidia kutambua kwamba, kila fursa iliyopo inaweza kutumika kwa ajili ya maboresho ya maisha ya mtu: kiroho na kimwili. Kufaulu na kushindwa katika masuala ya michezo ni ukweli usioweza kupingika. Hii iwe ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu; kwa kuzingatia na kuheshimu sheria, kanuni, maadili na utu wema; mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika masuala ya michezo.

Lakini inasikitisha kuona kwamba, nyakati hizi, michezo inahusishwa sana na masuala ya kiuchumi, mashindano yasiyokuwa na tija, vurugu pamoja na ubaguzi kwa wale ambao hawana kiwango cha juu cha ushindi. Mashindano ya kimataifa, kimekuwa ni kichaka cha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na umati mkubwa wa wasichana na wanawake kutumbukizwa katika utalii wa ngono pamoja na mifumo yote ya utumwa mamboleo.

Wakati huo huo, Patriaki Cyrill wa Kanisa la Kiorthodox la Moscow na Urusi nzima katika ujumbe wake kwa ajili ya wanamichezo na mashabiki kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watakaokusanyika mjini Moscow kuanzia tarehe 14 Juni hadi tarehe 15 Julai 2018 kushuhudia Fainali za mashindano ya Kombe la Dunia kwa mwaka 2018 anapenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wote kwa moyo mkunjufu, kwa kusema kwamba, michezo ni furaha! Lakini, kuna haja kwa wanamichezo kuhakikisha kwamba, wanazingatia sheria kanuni na taratibu za michezo pamoja na kujikita katika kanuni maadili na utu wema.

Patriaki Cyrill anakaza kusema, michezo ni sehemu ya mchakato kuelekea utakatifu wa maisha kwa kufunga na kujinyima mambo mengi. Lakini, matumizi haramu ya dawa za kulevya, rushwa na ufisadi kwa ajili ya kujipatia ushindi kwa gharama yoyote ile ni jambo ambalo kamwe haliwezi kukubaliwa. Anawataka wanamichezo na mashabiki wao kujikita katika kanuni maadili na utu wema na kamwe wasipoteze heshima na utu wao kwa mambo mpito! Ufanisi katika maisha unafumbatwa kwa namna ya pekee katika: nidhamu, sadaka, uvumilivu na udumifu katika kupambana na changamoto za maisha!

Michezo ni sehemu ya maisha ya Kikristo!Hakuna njia ya mkato katika maisha! Wale waliotafuta njia ya mkato wamejichumia majanga na maafa kwao wenyewe, familia na jamii zao! Wanamichezo wanaotumia dawa haramu za kulevya na kuongeza nguvu wanakwenda kinyume cha mtazamo wa Kikristo katika uelewa wa michezo, utu na heshima ya binadamu. Wanamichezo wanapaswa kuongozwa na nguvu ya maisha ya kiroho katika mapambano yao, ili kuweza kupata mafanikio na ushindi wanaoutarajia.

Kwa sasa dunia nzima inawaka moto wa mashindano ya Kombe la Dunia huko  nchini Urusi. Watu wengi wanatafuta nafasi ya kuweza kushuhudia “mpambano huu ukirushwa mubashara na wanamichezo wakionesha ujuzi na weledi wao katika kusakata kabumbu”. Lakini baada ya Mashindano ya Kombe la Dunia nchini Urusi, maisha yataendelea kama kawaida. Viongozi wa Kanisa wanahamasishwa kuwa karibu sana na wanamichezo na kwamba, kuna haja kwa Kanisa la Kiorthodox kuibua mbinu mkakati wa michezo kwenye Parokia zake. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kumfunda mtu mzima: kiroho na kimwili. Kuanzia sasa, Kanisa linataka kuweka mbinu mkakati, kuunda timu za michezo katika ngazi mbali mbali na kuanzisha mashindano ya michezo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.