2018-06-11 13:14:00

Watanzania msikubali kuyumbishwa kwa misingi ya udini!


Majadiliano ya kidini yanapaswa kuwa ni mpango mkakati unaomwilishwa katika ngazi mbali mbali za maisha ya waamini, kuanzia kwenye familia, masuala ya kidiplomasia pamoja na mwingiliano wa tamaduni kati ya watu, ili kujenga msingi wa maridhiano, umoja na udugu, kwa kutambua kwamba, tofauti za kidini si chanzo cha kinzani, bali ni utajiri unaopaswa kufumbatwa na wote, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Waamini wa dini mbali mbali nchini Tanzania wanapaswa kukoleza moyo wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni, ili kujenga haki, amani, upatanisho, umoja wa kitaifa na uhuru wa kuabudu msingi mkuu wa haki nyingine zote za binadamu. Majadiliano katika ukweli ni kazi na zawadi ya Mwenyezi Mungu, kazi ambayo waamini na watu wenye mapenzi mema wanapaswa kuithamini, kwa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu.Tofauti msingi zinazojitokeza miongoni mwa familia ya Mungu nchini Tanzania ni utajiri unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na kamwe zisiwe ni chanzo cha vurugu, kinzani na mipasuko ya kijamii.

Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wasikubali kuchonganishwa na kwamba Serikali haiongozwi kwa misingi ya kidini bali imeziachia taasisi za kidini zifanye kazi kwa kuzingatia Katiba, Sheria za nchi na malengo yaliyokusudiwa katika uanzishwaji wake. Aliyasema hayo Jumamosi, Juni 9, 2018 alipozungumza na viongozi na wananchi wa Mkoa wa Mwanza baada ya kushirikiana nao katika futari aliyowaandalia. Shughuli hiyo ilihudhuriwa na waamini wa dini mbalimbali. Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanaishi kwa amani na utulivu, jambo litakalowawezesha kufanya shughuli zao kikamilifu, hivyo wasikubali kuchonganishwa kwa misingi yoyote. “Nawaasa viongozi wa dini msikubali kutumia makundi mengine nje ya taasisi zenu kwa ajili ya kuwazungumzia masuala yenu kwa sababu watawachonganisha na Serikali ambayo haipo kwa ajili ya kugombana na taasisi yoyote,” alisisitiza.

Waziri Mkuu alisema jukumu kubwa la taasisi za kidini ni kuhakikisha wanawalinda waamini wao pamoja na kuwaongoza kwa kuwapa mafundisho mema yanayompendeza Mwenyezi Mungu, ambayo yatawawezesha kuishi kwa amani. Alisema misingi ya amani na utulivu ikiwa pamoja na mshikamano walionao wananchi umesababisha Tanzania kupata heshima kubwa dunia kote, hivyo ni vema kila mwananchi ahakikishe suala la kudumisha amani linapewa kipaumbele. Pia Waziri Mkuu alisema amefurahi sana kujumuika na wananchi wa Mkoa wa Mwanza katika futari hiyo, ambapo aliwapongeza kwa kukamilisha uundaji wa kamani za amani kuanzia ngazi ya kata hadi mkoa.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. John Mongella amlishukuru Waziri Mkuu kwa ukarimu wake kwa kuwaalika wakazi wa Mwanza katika hafla hiyo, ambapo alisema Mwanza ni kitovu cha amani kwa kanda ya Ziwa na nchi za Maziwa Makuu. “Mwanza tumejipanga na tunashirikiana na taasisi zote kwenye njanja zote, tupo pamoja na tunashirikiana katika kuimarisha amani na utulivu. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli kwa kutuamini na tunamuahidi tutafuata falsafa zake katika utendaji wetu,”.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza na Askofu wa Kanisa la Charismatic Episcopal Church of Tanzania (CECT), Charles Sekelwa alisema wao wanaiunga mkono Serikali katika kudumisha amani na wataendelea kushirikiana nayo. Alisema awali kulikuwa na changamoto ya matabaka ya kidini iliyobabisha na kutoelewana baina ya waislamu na wakristo, ambapo kamati yao ilifanya kazi ya kuyasulisha na sasa hali ni shwari. “Matabaka ya kiimani yameisha na watu wa dini zote wanashirikiana vizuri,”. Askofu Sekelwa alisema wao kama viongozi wa pande hizo mbili hawawezi  kukubali kuona kunakuwa na matabaka ya kiimani miongoni mwa waumini, hivyo watakikisha wanaendelea kuwafundisha waumini wao umuhimu wa amani. Hafla hiyo ilihudhuriwa na Naibu Spika Dkt. Tulia Akson, Naibu Waziri wa Nchi, OR – TAMISEMI, Joseph Kakunda, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali baadhi ya wananchi wa mkoa wa Mwanza.

Na Padre Richard A. Mjigwa, kwa ushirikiano na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tanzania.

    
All the contents on this site are copyrighted ©.