2018-06-09 16:18:00

Umuhimu wa nishati mpito, changamoto na fursa za maendeleo endelevu!


Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Notre Dame, kuanzia tarehe 8-9 Juni 2018, limefanya kongamano la kimataifa kwa kuongozwa na kauli mbiu “Nishati mpito na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote”: Mjadala kuhusu hatari, fursa, changamoto na njia za kufuata”. Kati ya wawezeshaji waliojipambanua zaidi ni Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu aliyetoa hotuba elekezi baada ya ufunguzi kufanywa na Askofu Marcelo Sànchez Sorondo, Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi pamoja na Sayansi Jamii.

Kongamano hili limefafanua: Lengo lake; mapitio ya ajenda, maana ya nishati mpito; nguvu zinazoongoza mabadiliko makubwa na katika kiwango cha hali ya juu cha nishati mpito; fursa na changamoto zilizopo katika uwanja huu; matokeo na madhara yake katika masuala jamii, kiteknolojia na kiuchumi. Wajumbe pia wameshirikisha umuhumu wa kudhibiti ongezeko la nyuzi joto duniani na baadaye, Jumamosi, tarehe 9 Juni 2018 wamekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko!

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amejikita zaidi katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia; changamoto zilizopo; mbinu mkakati wa muda mrefu ili kukidhi kiu ya nishati duniani; fursa makini inayoweza kusaidia Jumuiya ya Kimataifa kupambana na umaskini na ukosefu wa usawa katika jamii, pamoja na changamoto endelevu zinazopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa na kwa siku za usoni! Baba Mtakatifu anawapongeza washiriki wote waliochangia mawazo katika kongamano hili la kimataifa, kwa kusikilizana, kwa kuhakiki na kuanza kuangalia matarajio mapya kwa siku za usoni!

Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanayowezesha mawasiliano kusambaa kwa haraka zaidi; watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuweza kukutana; uwezekano wa kubadilishana bidhaa na huduma ni mkubwa kiasi hata cha kuvuka mabonde na milima, bahari na mito kwa muda mfupi kabisa! Lakini, pamoja na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, kuna watu ambao bado hawabahatika kupata nishati ya umeme na idadi yao inakadiriwa kuwa ni zaidi ya watu bilioni moja!

Hii ni changamoto kubwa anasema Baba Mtakatifu inayohitaji kuvaliwa njuga ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uhakika wa nishati ya umeme kwa watu wengi zaidi, ili kuepuka uharibifu na uchafuzi mkubwa wa mazingira, hali ambayo itasababisha majanga na maafa makubwa kwa binadamu. Ubora wa hali ya hewa, kiwango cha ujazo wa bahari; maji safi na salama; mazingira na baianuai ni kiu ya nishati ambayo inazimwa kwa kutokuwa na usawa hata kidogo kabisa kutokana na umaskini na ubaguzi unaowatenga baadhi ya watu ndani ya jamii kutokana na hali yao ya maisha. Kumbe, kuna hajna ya kujikita katika utunzaji bora wa mazingira, ili kuzima kiu ya nishati kwa gharama nafuu pamoja na kuwa na matumizi bora zaidi ya rasilimali ya dunia. Uratibu wa nishati unatarajia zaidi ubora wa maisha pamoja na udhibiti wa vita, kinzani na migogoro inayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kutokana na changamoto hizi zote kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuibua mbinu mkakati wa muda mrefu utakaosaidia kukuza na kudumisha uchumi; kulinda na kuendeleza afya bora; kutunza mazingira; kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu sanjari na kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Baba Mtakatifu katika Wosia wake wa kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji bora wa mazingira” ametumia fursa hii kuwaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuanza kujikita katika mchakato wa kutafuta nishati mbadala ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotokana kwa kiasi kikubwa na uchafuzi wa mazingira.

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwa kusema, hii ni changamoto kubwa na fursa inayopaswa kuvaliwa njuga na wadau mbali mbali; kwa kusaidia nishati kupatikana hata maeneo ya vijijini; kwa kuhakikisha kwamba, nishati inayotolewa ni safi na rafiki kwa mazingira na kwamba, inasaidia kupunguza ongezeko la joto duniani. Utekelezaji wa Makubaliano ya Itifaki ya Paris ya mwaka 2015 kuhusu Mazingira; ni muhimu sana katika mapambano dhidi ya umaskini; kwa kukuza mafungamano ya kijamii pamoja na kulinda mazingira. Yote haya yanawezekana ikiwa kama kutakuwepo na ushirikiano wa kifedha na kiuchumi; uhamishaji wa teknolojia sanjari na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unaoongozwa na kauni auni, ili kukuza uchumi na mafungamano ya kijamii.

Changamoto ya nishati mpito ni kubwa inayohitaji sera na mikakati makini; uwaibikaji wa kijamii pamoja na kubainisha kanuni msingi za uwekezaji ili kukuza na kudumisha umoja na mshikamano; kwa kuondokana na ubinafsi na uchoyo ili kukazia kanuni maadili na utu wema. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa sana, lakini waathirika wakuu ni maskini, wanaoteseka kutokana na kusua sua kwa uzalishaji katika sekta ya kilimo, kiasi kwamba, baadhi ya wakulima wanaamua kufunga biashara zao na kwenda kutafuta maisha bora sehemu nyingine za dunia. Kuna watu bilioni moja hawana nishati ya umeme. Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuungana ili kufutilia mbali tofauti hizi. Changamoto na athari za mabadiliko ya tabianchini zinahitaji umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii ili kuweza kupambana nazo! Kuna haja pia ya kuwafunda viongozi, watakaotoa dira na kuonesha njia ya kufuata, ili kuthamini na kudumisha Injili ya uhai. Uharibifu wa mazingira una hasara zake katika; maisha ya ndoa na familia; mafungamano ya kijamii na kiuchumi sanjari na kuboresha hali ya maisha. Wataalam watumie ujuzi na maarifa yao ili kuboresha huduma ya binadamu; kwa kujali na kuendeleza familia ya binadamu; kwa kuwajibika, kulinda na kutunza mazingira, kwa ajili ya mahitaji ya sasa na yale ya kijazi kijacho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.