2018-06-09 15:50:00

Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya Amazonia: Kuona, Kung'amua na Kutenda


Uinjilishaji na Utamadunisho ni mchakato unaolitajirisha Kanisa na kwamba, Kanisa linataka kuwajengea watu uwezo wa kupambana na changamoto za maisha, ili siku moja Kanisa liweze kuwa na sura ya Amazonia inayofumbatwa na uwepo wa watu mahalia. Hiki ndicho kiini cha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Amazonia itakayoadhimishwa mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2019 kwa kuongozwa kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia endelevu”. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wataendelea kuimarisha mafungamano ya kijamii, kimaumbile na mang’amuzi ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Kanisa linapenda kukazia Injili ya upendo na mshikamano unaowashirikisha wananchi mahalia katika maamuzi na utekelezaji wa sera na mikakati yake kwa kuongozwa na mbinu mkakati wa kuona, kung’amua na kutenda kwa kukazia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imewasilisha Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia ambayo imegawanyika katika sehemu kuu tatu.

SHEMU YA KWANZA NI KUONA: Utambulisho wa kilio cha Amazonia. Amazonia ni eneo lenye utajiri mkubwa wa maliasili, maji na misitu linalozungukwa na nchi tisa yaani: Brazil, Bolivia, Equador, Gayana, Perù, Suriname, Venezuela pamoja na Guayana ya Kifaransa. Kanisa katika maisha na utume wake katika Ukanda wa Amazonia limejitahidi kujibu kilio cha watu wa Mungu katika eneo hili, mintarafu haki msingi za binadamu na utunzaji bora wa mazingira. Hili ni eneo ambao lina utajiri mkubwa wa watu, tamaduni na mitindo mbali mbali ya maisha. Lakini pia ni eneo ambalo limekumbana sana na changamoto za ukoloni na ukoloni mamboleo kiasi cha kuwafanya baadhi ya watu wake kukimbia maeneo yao ya asili na kuwaondoa katika mtindo wa maisha unaowawezesha kuwa walinzi wa misitu na utajiri wake asilia.

Uharibifu mkubwa wa mazingira, unaotokana na hitaji kubwa la malighafi na madini ili kukidhi ukuaji wa sekta ya viwanda hali ambayo imepelekea uporaji wa rasilimali na utajiri wa Ukanda wa Amazonia kiasi hata cha kusababisha kinzani katika sekta ya kilimo, maisha ya kijamii pamoja na sera za utunzaji bora wa mazingira. Matokeo yake ni umaskini mkubwa wa wananchi mahalia; uvunjwaji wa haki msingi za binadamu; ukosefu wa usawa na matokeo yake ni kukua na kuongezeka kwa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na ulevi wa kupindukia. Kutokana na hali ngumu ya maisha, watu wengi wanalazimika kukimbilia mijini au nje ya Ukanda wa Amazonia ambako wanajikuta wakiwa kama wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum!

Matokeo yake, utu na heshima yao kama binadamu vinawekwa rehani na wanawake na wasichana wanatumbukizwa katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Mambo yote haya yanachangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa utu na heshima ya binadamu sanjari na tunu msingi za maisha ya kijamii na kitamaduni. Kumbe, hapa kunahitaji mchakato wa maendeleo endelevu yanayowahusisha watu wote bila ubaguzi. Kanisa baada ya kutambua kilio cha wananchi wa Amazonia, linataka kukijibu kwa sera na mikakati ya shughuli za kichungaji na kijamii zinazomwilisha katika uhalisia wa maisha ya watu! Utambulisho wa wananchi wa Ukanda wa Amazonia ni muhimu sana kwani hii ni sehemu ya utajiri wa Ukanda huu. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuwalinda, kuwaheshimu na kuwaenzi watu mahalia pamoja na kuwaboreshea maisha, ili waweze kushiriki kikamilifu katika ustawi na maendeleo yao! Hapa Kanisa linaendelea kutoa ushuhuda kama sehemu ya mchakato wake wa Uinjilishaji wa kina unaotekelezwa na wamisionari mbali mbali.

Katika historia ya Kanisa, hapa, wamisionari wameonja maana ya kutundikwa Msalabani, kwani Ukanda wa Amazonia, umekuwa ni uwanja wa shuhuda za mateso na sadaka ya maisha yanayotolewa na wamisionari kila kukicha! Lakini pia, watu wake wamemfungulia Roho Mtakatifu nyoyo zao na hivyo kupokea kweli za Kiinjili. Hili ni eneo ambalo tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; utu na heshima ya binadamu; umoja na mshikamano; Ibada na uchaji wa Mungu vinapewa kipaumbele cha pekee. Kumbe, kuna haja ya kujikita katika haki pamoja na kusimamia haki msingi za wananchi wa Amazonia; kukuza na kudumisha tasaufi ya maisha na hekima ya wahenga wa Ukanda huu kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu yanayogusa undani wa mtu!

SEHEMU YA PILI KUNG’AMUA: Mwelekeo wa wongofu wa kichungaji na kiekolojia. Mama Kanisa anataka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo katika Ukanda wa Amazonia mintarafu mwelekeo wa Kibiblia na Kitaalimungu ili kulinda na kudumisha mazingira nyumba ya wote; kukuza na kudumisha mahusiano mema kati ya Mwenyezi Mungu muumbaji na binadamu; ili kupata udhibiti katika ukweli, wema, sheria na kanuni msingi. Lengo ni kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kutokana na kazi yake ya uumbaji.

Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo mintarafu mwelekeo wa kijamii unaofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu unaokazia utu, heshima, uhuru na haki msingi za binadamu. Ni Injili ya haki, amani na mshikamano wa dhati unaopania kuganga na kutibu madonda ya wananchi wa Ukanda wa Amazoni. Kanisa linataka kutoa utambulisho wake kama Msamaria mwema. Hili ni Kanisa linalotumwa kuinjilisha na kuinjilishwa; kwa kusimama kidete kulinda Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo na uharibifu wa mazingira. Kanisa linataka kujikita katika majadiliano ya ukweli na uwazi; uvumilivu na ukarimu. Ili kutekeleza yote haya kuna haja ya kuwa na wongofu wa kichungaji, ili kusikiliza na kujibu kilio na mahangaiko ya watu wa Ukanda wa Amazonia.

Kanisa linataka kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo mintarafu mwelekeo wa ekolojia endelevu unaofumbatwa katika utunzaji bora wa mazingira; kwa kusimama kidete kupambana na changamoto zinazojitokeza katika Ukanda huu kiasi hata cha kutishia maisha, ustawi na maendeleo ya wengi. Mchakato wa uinjilishaji unajikita katika utunzaji bora wa mazingira unaofumbatwa katika wongofu wa mtu binafsi, kijami na kiekolojia. Huu ni mwaliko wa kutambua dhambi zilizotendwa, ili kutubu na kumwongokea Mungu; kwa kubadili mfumo na mtindo wa maisha kwa kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kadiri anavyotaka!

Kanisa linataka kutangaza Injili ya Kristo Amazonia kwa kujikita katika mwelekeo wa Kisakramenti; kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kutambua na kuthamini maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kukazia katekesi endelevu ya maisha ya Kisakramenti, kwani maji katika Sakramenti ya Ubatizo ni kielelezo cha uhai na maisha mapya katika Kristo Mfufuka. Kwa njia ya Fumbo la Ekaristi, waamini wanaendelea kuadhimisha upendo wa Kristo usiokuwa na kikomo kwa waja wake. Ekaristi Takatifu inajenga na kuimarisha umoja wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Kwa njia hii, waamini wanahamasishwa kuwa ni walinzi na watetezi wa kazi ya Uumbaji. Damu ya watu wasiokuwa na hatia iliyomwagika kwenye Ukanda wa Amazonia, iwe ni chachu ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Amazonia.

Injili ya Kristo itangazwe Amazonia kwa kukazia mwelekeo wa kikanisa na kimisionari, kwa kutambua kwamba, Kanisa kwa asili ni la kimisionari, linatumwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili, Sheria kanuni maadili na utu wema; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu na kwa ajili ya wokovu wa roho za watu! Kanisa linataka kukuza umoja na utofauti kwa kuzingatia “sensus fidei” yaani “utambuzi wa imani ya watu wa Mungu; kwa kuungama Kanuni ya Imani; Kwa kuungana ili kulinda: maisha, mazingira na tamaduni za watu; ili kujenga na kudumisha Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa katika Ukanda wa Amazonia. Kanisa linataka kujenga utamaduni na sanaa ya kuwasilikiza watu; kwa kudumisha na kumwilisha “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” pamoja na kukuza ari na mwamko wa kimisionari. Yote haya ni sehemu ya mchakato kuona na kusikiliza; kung’amua na kutenda kadiri ya hali halisi ya wananchi wa Ukanda wa Amazonia.

SEHEMU YA TATU: KUTENDANjia mpya za Kanisa zenye Uso wa Amazonia, ili kuwa kweli Kanisa na familia ya Mungu; kwa kutambua na kuthamini utakatifu wa Ukanda wa Amazonia; kwa kukuza na kudumisha utambulisho wake; utandawazi wa umoja na mshikamano wa upendo; kwa kushuhudia na kuinjilisha; kwa njia ya huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na maskini pamoja na kupembua njia mpya za sera na mikakati ya shughuli za kichungaji.

Kanisa linataka kujikita katika mwelekeo wa kinabii kwa kukazia: Maendeleo endelevu ya binadamu; utambulisho wa wananchi wa Amazonia; haki zao msingi pamoja na kuwapatia maji safi na salama kama sehemu ya haki zao msingi. Ni mwaliko wa kufanya wongofu wa kiekolojia; kwa kudumisha haki msingi za binadamu. Kanisa linataka kulinda mazingira kwa kujikita katika: uhuru, ukweli na uzuri, ili kujimanua kutoka katika ulaji wa kupindukia kwa kutambua kwamba, kwa hakika maisha ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni muda muafaka wa kukazia Injili ya upendo na mshikamano wa dhati.

Kanisa linataka kuwadumisha Mitume wenye sura ya Amazonia ili kuendeleza utamadunisho na kukuza dhana ya Kanisa la Kristo ambalo: Ni moja, takatifu, katoliki na la mitume; ili kuweza kukabiliana na changamoto changamani katika Ukanda wa Amazonia wenye utajiri mkubwa wa watu na tamaduni zao. Kanisa linataka kujikita katika mfumo wa maendeleo endelevu kwa kutangaza Injili ya haki, mshikamano, ustawi na mafao ya wengi; kwa kuwashirikisha waamini katika utekelezaji wa dhamana yao ya Ubatizo unaowashirikisha utume wa Kristo: Kuhani, Nabii na Mfalme. Lengo ni kuwajengea uwezo watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia ili kweli waweze kujisikia kuwa ni wadau katika mustakabali wa maisha yao.

Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji haina budi kujikita katika utamadunisho, ili kusoma alama za nyakati na kujibu kwa ufasaha changamoto mamboleo. Kanisa halina budi kuibua mifumo mbali mbali ya utume unaoweza kutekelezwa na mihimili ya uinjilishaji kadiri ya dhamana na wajibu wao katika Jumuiya za waamini. Wanawake wanayo nafasi kubwa katika mchakato wa uinjilishaji. Kanisa linapaswa kuibua njia mpya zitakazokumbatia: Mihimili ya uinjilishaji; Liturujia na Taalimungu, daima likijitahidi kua aminifu kwa kwa Injili ya Kristo.

Tasaufi inayogusa maisha halisi ya wananchi wa Amazonia; majadiliano, unabii pamoja na kukuza dhana ya ushuhuda wa imani ili kulinda Injili ya uhai na kuanza ujenzi wa historia mpya! Umefika wakati kwa Kanisa kuvumbua mbegu na matunda ya Neno la Mungu yaliyopandikizwa kati ya watu wa Amazonia, ili waweze kuwa ni mashuhuda, vyombo vya uinjilishaji na watunzaji bora wa mazingira. Hati ya utangulizi wa Sinodi inahitimishwa kwa kutoa maswali dodoso yatakatohaririwa na baadaye kutoa “Hati ya Kutendea Kazi!, Instrumentum Laboris. Haya ni maswali yanayobubujika kutoka katika sehemu kuu tatu za Hati ya Maandalizi ya Sinodi ya Amazonia yanayojikita katika: Kuona, Kung’amua na Kutenda.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.