2018-06-08 15:19:00

Papa Francisko: Mitandao ya kijamii iwe ni maskani ya ubinadamu!


Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Juni 2018 anasema, mitandao ni zawadi ya Mungu, lakini pia ni wajibu mkubwa. Kuna maendeleo na matumizi makubwa ya mitandao ya kijamii, kielelezo makini cha kukua na kupanuka kwa teknolojia ya mawasiliano ya jamii, ambacho kimekuwa ni chombo kinachowakutanisha watu kutoka sehemu mbali mbali, ili kuimarisha sanjari na kupanua mtazamo wa mambo mbali mbali katika maisha ya watu wengi duniani.

Teknolojia ya mawasiliano ya jamii anaendelea kudadavua Baba Mtakatifu kwa kusema kwamba, inatoa mianya ya watu kukutana na kujenga umoja na mshikamano wa dhati. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, mitandao ya kijamii haitakuwa ni fursa wala mwanya wa kuwatenga watu, bali nafasi maalum na muhimu inayotajirisha utu na heshima ya binadamu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa pamoja, ili kweli mitandao ya kijamii isaidie kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii, kwa kuheshimu na kuthamini tofauti zinazojitokeza kati yao. Ujumbe wa nia za Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya video umeandaliwa na Mtandao wa Utume wa Sala kwa kushirikiana na kampuni ya La Machi inayojihusisha na utengenezaji na usambazaji wa ujumbe huu pamoja na Vatican Media, ambayo imerekodi ujumbe huu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.