2018-06-07 11:13:00

Patriaki Bartholomeo: Athari za kiekolojia zinahitaji majibu ya pamoja


Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol anasema kuna haja ya kuunganisha nguvu na kutoa majibu muafaka mintarafu uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Hii ni changamoto changamani inayohitaji umoja na mshikamano; lakini zaidi toba na wongofu wa ndani, ili kukabiliana na changamoto za uharibifu mkubwa wa mazingira. Hapa jambo la msingi ni ushirikiano wa dhati ili kuweza kukamilishana na wala si kulumbana na kushindana kusikokuwa na tija wala mashiko!

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wakati huu, Kanisa hili linapoadhimisha Kongamano la Kimataifa juu ya Ekolojia kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kuelekea Attica ya kijani zaidi: Kuendeleza dunia na kutunza wakazi wake”. Kongamano limefunguliwa rasmi tarehe 4 na linahitimishwa tarehe 8 Juni 2018, huko Athens, nchini Ugiriki. Inasikitisha kuona kwamba, kutokana na mafao ya kiuchumi na siasa za kijiografia, kuna baadhi ya watu na nchi zimeamua kwenda kinyume na ushirikiano huu wa kimataifa kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote.

Huu ni uchumi usioguswa na mahangaiko pamoja na mahitaji msingi ya binadamu na matokeo yake ni uharibifu mkubwa wa mazingira na uporaji wa maliasili kwa ajili kwa ajili ya mafao ya binafsi, kielelezo cha uchu wa mali kwa njia ya mkato! Ikumbukwe kwamba, kuna uhusiano na mwingiliano mkubwa kati ya matatizo na changamoto za kijamii sanjari na mazingira. Kumbe, kuna haja ya kujifunga kibwebwe kupambana na hali hii; kwa njia ya ushirikiano na mshikamano; ili kulinda mazingira asilia. Dhamana hii, iwawezeshe watu kushirikiana na kushikamana katika huduma kwa binadamu; mambo msingi yanayoshikamana na kukamilishana.

Athari za kiekolojia zinatishia umoja na mafungamano ya kijamii na kiuchumi na waathirika wakuu ni maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuna uhusiano mkubwa unaobubujika kutoka katika falsafa ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; Ibada na Uchaji wa Mungu. Kuna mwilingiliano mkubwa kati ya umaskini na ekolojia ya dunia. Pale ambapo utu na heshima ya binadamu havithaminiwi, hapo pia kuna uharibifu mkubwa wa mazingira. Chuki na uhasama kati ya binadamu ni chanzo kikuu pia cha kuporomoka kwa uchumi na ekolojia.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuivalia njuga changamoto hii, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa kubadili mtindo na mfumo wa maisha, ili kujifunza kulinda mazingira nyumba ya wote pamoja na kuwahudumia jirani, kwani falsafa ya kulinda na kudumisha mazingira bora ni kushirikishana amana na utajiri wa dunia, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kwa njia hii, watu wataweza kuthamini utu na heshima ya binadamu kwa kuona na kutambua Uso wa huruma na upendo wa Mungu unaofunuliwa kwa njia ya Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 
All the contents on this site are copyrighted ©.