2018-06-07 10:49:00

Papa Francisko: Mediterrania imegeuka kaburi la wakimbizi na wahamiaji


Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni dhamana inayowawajibisha watu wote na wala si amana wala utajiri wa mtu binafsi! Kumbe, kuna haja ya kutambua na kuheshimu haki msingi za binadamu na haki za kila jamii! Hivi ndivyo anavyoandika Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomtumia Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol wakati huu, Kanisa hili linapoadhimisha Kongamano la Kimataifa juu ya Ekolojia kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kuelekea Attica ya kijani zaidi: Kuendeleza dunia na kutunza wakazi wake”.

Kongamano limefunguliwa rasmi tarehe 4 na linahitimishwa tarehe 8 Juni 2018, huko Athens, nchini Ugiriki. Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru na kumpongeza Patriaki Bartolomeo wa kwanza kwa kuendelea kusimama kidete katika kulinda, kutetea na kutunza mazingira nyumba ya wote. Amekuwa mstari wa mbele katika kuelimisha na kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira, kwani uharibifu wa mazingira ni chanzo kikuu cha majanga yanayoendelea kumwandama mwanadamu sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu bado anayo kumbu kumbu hai, ya siku ile ya tarehe 16 Aprili 2016 Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Askofu mkuu Hieronymos II wa Jimbo kuu la Athens na Ugiriki katika ujumla wake, walipoungana kwa pamoja ili kuonesha mshikamano wao na wakimbizi pamoja na wahamiaji waliokuwa wanateseka sehemu mbali mbali za dunia: Kisiwa cha Lesvos nchini Ugiriki, kikawa ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anasikitika kusema bahari nzuri ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi.

Baba Mtakatifu anaishukuru familia ya Mungu nchini Ugiriki kwa ukarimu na upendo inaoendelea kuwaonesha wakimbizi na wahamiaji; ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya kiutu na Kikristo zinazomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, licha ya hali ngumu ya uchumi na athari kubwa za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa nchini Ugiriki. Sadaka na majitoleo ya wananchi wa Ugiriki ni mwanga safi unaoweza kuwasaidia washiriki kutambua umuhimu wa kauli mbiu inayoongoza kongamano hili la kimataifa.

Baba Mtakatifu anaendelea kudadavua kwa kusema kwamba, kumekuwepo na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia. Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu anarejea kwenye kiini cha Waraka wake wa Kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” anamofafanua kwa kina na mapana athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuonesha wasi wasi wake kwa ajili ya kizazi kijacho!

Baba Mtakatifu anauliza swali la msingi, Je, ni ulimwengu wa namna gani, Jumuiya ya Kimataifa inataka kukiachia kikazi kijacho? Dunia ambayo imechakaa na kuharibika kabisa? Kumbe, kuna haja ya kuchunguza dhamiri katika ukweli na uwazi, ili kuibua mbinu mkakati utakaosaidia kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira bora. Uharibifu wa mazingira unaojionesha kwa wakati huu, unapata chimbuko lake ni katika moyo wa mwanadamu wenye uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka; moyo unaotaka kupata faida kubwa kwa gharama kubwa ya watu wa familia ya Mungu. Kamwe, binadamu hawezi kufumbia macho uharibifu wa mazingira unaoendelea kutendeka sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni changamoto pevu inayopaswa kuvaliwa njuga na watu wote, kila mmoja kadiri ya utamaduni, mang’amuzi, shughuli, karama na mapaji yake. Lengo ni kuanza kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu. Ni wajibu wa Wakristo kutambua mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya kimaadili na kiutu zinazochangia pia athari za uharibifu wa ekolojia; ili waweze kuunganisha nguvu zao kulinda, kutetea na kudumisha mazingira nyumba ya wote.

Maadhimisho ya Siku ya Kuombea Utunzaji Bora wa Mazingira Duniani,  inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi, Septemba, yanalenga kuwaunganisha Wakristo ili kusimama kidete kupambana na changamoto hii tete katika ulimwengu mamboleo. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa Katoliki litaendelea kushirikiana na kushikamana na Kanisa la Kiorthodox katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira; ili kuweza kujikita katika maendeleo endelevu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.