2018-06-07 13:42:00

Papa Francisko awataka waamini kuwa na kumbu kumbu endelevu ya imani


Ili Wakristo waweze kusonga mbele katika imani, matumaini na mapendo, hawana budi kuhakikisha kwamba, wanadumisha kumbu kumbu hai ya siku ile ya kwanza walipokutana na Kristo Yesu katika safari ya maisha yao; watu waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwarithisha imani bila kusahau muhtsari wa mafundisho makuu ya Yesu yanayofumbatwa katika Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani! Paulo Mtume, anamkumbusha Timoteo kuhusu: Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, Neno wa kuwaminiwa siku zote kwani kamwe hawezi kujikana mwenyewe!

Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, 7 Juni 2018 wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakaza kusema, “Mkumbuke Kristo Yesu aliyefufuka” ili kupata nguvu, ari na mwamko wa kusonga mbele kwa imani na matumaini, kwani, kumbu kumbu hai ya Mkristo ni kukutana na Kristo Yesu! Kwa njia hii, Wakristo wanakuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, tayari kumwilisha katika uhalisia wa maisha yao ile Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani.

Waamini wajitahidi kadiri wanavyoweza kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao: kwanza kabisa katika uhalisia wa matukio mbali mbali ya maisha yao; kwa njia ya wazazi na walezi wa imani na zaidi sana katika Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani. Sehemu ya kwanza, iliwawezesha waamini kutubu na kumwongokea Mungu. Waamini katika safari ya maisha hapa duniani, wamebahatika  kukutana na Kristo Yesu aliyejitahidi kujifunua katika maisha yao!

Hizi ni nyakati zinazopaswa kukumbukwa daima katika maisha ya waamini, kwani tangu siku ile Yesu aliwasaidia kufanya mageuzi katika maisha yao! Kristo aliwawezesha kung’amua wito na utume wao, au kwa kuwajalia neema na faraka katika nyakati ngumu za maisha. Haya ni matukio anasema Baba Mtakatifu Francisko ambayo yameacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu, kumbe, wanapaswa kuyatafakari.

Pili anasema Baba Mtakatifu Francisko, katika maisha kuna viongozi ambao wamewafundisha na kuwarithisha imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hawa wanaweza pia kuwa ni wazazi, babu na bibi! Huu ni umati mkubwa wa mashuhuda wa imani, ambao wanaweza kuwasaidia waamini kuchota nguvu, kwa kuiga mfano wa maisha na uvumilivu wao, uliowawezesha hata kukabili kifodini kwa imani na matumaini makuu. Katika shida na magumu ya maisha, Wakristo hawana budi kurejea tena na tena katika chemchemi ya imani ili kuchota nguvu ya kuweza kusonga mbele! Kumbe, waamini wanapaswa kuwa ni watu wenye mizizi iliyozama katika imani!

Tatu, Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kuhusu Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani! Mwinjili Marko anakazia Amri hii kwa kusema, “Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote. Amri kuu ya upendo ni kielelezo cha kumbu kumbu endelevu ya upendo wa Mungu kwa waja wake; upendo ambao umejidhihirisha katika historia nzima ya ukombozi, kiasi kwamba, historia hii imeandikwa katika sakafu ya nyoyo za waamini hadi leo hii. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiuliza ikiwa kama kweli wamekuwa ni waaminifu kwa Amri hii ya upendo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kujitaabisha kukumbuka Amri za Mungu, ili kuweza kuzimwilisha katika uhalisia wa maisha!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Kumkumbuka Kristo Yesu” maana yake ni kwa mwamini kumwinulia uso wake na kumwangalia katika historia na matukio mbali mbali ya maisha; siku ile alipokutana naye kwa mara ya kwanza; wazazi na walezi waliomsaidia kuonja amana ya imani pamoja na kuanza kumwilisha Amri ya upendo katika uhalisia wa maisha. Imani na kumbu kumbu ni chanda na pete anasema Baba Mtakatifu; kwani ni matukio mawili yanayokamilishana.

Hii ni kumbu kumbu endelevu ya Kristo Yesu aliyezaliwa, akafa na kufufuka kwa wafu, atakuja tena kuwahukumu wazima na wafu. Kristo Yesu, ni Bwana wa kumbu kumbu endelevu ni Bwana wa matumaini. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafuta muda na kufanya tafakari kidogo kuhusu kumbu kumbu ya siku ile walipokutana na Kristo Yesu kwa mara ya kwanza; wazazi na walezi; Amri ya Upendo na kuangalia mwelekeo wa matumaini katika maisha yake kwa sasa! Haya matumaini yanafumbatwa katika kitu gani?

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.