2018-06-07 14:59:00

Dhamiri ni mahali patakatifu panapopaswa kuheshimiwa!


Mambo matatu makuu yanaonekana katika Neno la Mungu Jumapili hii ya leo na yanatusaidia katika tafakari yetu;1. Yesu anakataa kwamba anawinga pepo kwa nguvu ya Belzebuli. 2. Habari juu ya dhambi ya kukufuru dhidi ya Roho Mtakatifu. 3. Mama yangu na ndugu zangu ni wale wasikiao Neno la Mungu na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao! Yesu amekuja kufanya mapenzi ya Baba Yake. Jambo hili liko wazi katika injili zote; kwamba, Yesu alikuja kufanya mapenzi ya Baba yake. Kadiri ya mwinjili Yohane, huu ndio utambulisho wa Yesu kama tusomavyo katika Yoh. 5:30 – ‘mimi siwezi kufanya kitu kwa amri yangu; nahukumu kama ninavyosikia, na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu nafanya si nitakavyo mimi, bali atakavyo yeye aliyenituma’. Na kwa ufahamu huo huo Yohane anawatambulisha wale wafanyao mapenzi ya Baba na wanaoshiriki mapenzi ya Mungu, ambao ndio wale wanaoisikia sauti ya Mungu.

Wayahudi walionekana kumiliki uhusiano wao na Mungu kwa vile  ni kizazi cha Abrahamu. Huu mtazamo mpya wa Yesu wa kuwapokea wote unaenda kinyume na nini kinaunda familia katika utamaduni wa kiyahudi. Kwa jamaa wa Yesu, ilionekana anainajisi nyumba yao.  Yesu anakaza kwamba watakuwa hivyo kweli yaani wana wa Abrahamu kama watamsikiliza Mungu – angalia Yoh. 8:39-47.... wakajibu wakamwambia, Baba yetu ndiye Abrahamu. Katika utamaduni wa kiafrika, utambulisho wa mtu umefungamana sana na familia na kabila. Yesu anawachangamotisha watu wa Yuda kuelewa kwamba utendaji mwadilifu wa kimaadili na si ukoo ndio unaonesha uhusiano na Baba. Na ndivyo anavyoelezea jibu rasmi kwa kipengele cha tatu hapo juu – mama yangu na ndugu zangu ni wale wasikiao neno la Mungu. Kwa namna hii, Yesu anazindua maana mpya ya uhusiano wetu na Mungu.... Yoh. 8:47 ... aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu. Hapa anatoa jibu kwa wale watu waliomwambia  ... mama yako na ndugu zako wako nje wanakutafuta.

Mtu mmoja anaelezea haja ya kujinasua na vifungo vinavyotutesa akitumia mfano wa mfungwa mmoja. Mfungwa mmoja Mrusi alikamatwa na askari wa Napoleoni alipovamia Urusi. Huyu mtu alichukuliwa mateka na ili kuwatambua kila mfungwa aliwekewa alama katika sehemu inayoonekana ya mwili. Huyu mfungwa aliwekewa alama ya ‘N’ katika mkono wake. Alama hii ilimtambulisha na askari alimtumia kadiri alivyopenda. Huyu mfungwa alipotambua kuwa alama ile ilimfanya mfungwa na mtumwa aliikata ile sehemu ya mkono wake na kwa namna hii akawa huru kumtumikia adui katika nchi yake mwenyewe. Pengine ndio mwaliko wa Yesu leo wa kututaka tuachane na vifungo vyetu na kuwa huru kuyafanya mapenzi ya Baba. Ni mwito wa kuchunguza tena dhamiri zetu, yaani ule ufahamu binafsi wa mtu juu ya uwepo wake, juu ya matendo yake.

Katika maana halisi yake Yesu, anataka watu wavuke hali hiyo ya kiasili (watu wa damu – wenye mipaka) vile vifungo visivyokuwa na maana na kuukubali ufalme wa Mungu, usio na mipaka. Yesu anasema wazi kuwa amekuja kuutangaza huo ufalme. Katika Agano Jipya, pepo walikuwa ni kinyume cha alichokuwa anafanya Yesu. Belzebuli ni mfalme wa pepo. Hivyo isingekuwa rahisi kwake Yesu kushirikiana nao. Ndiyo maana Yesu anasema wazi kama nikitoa pepo kwa nguvu ya pepo basi ufalme utakuwa umegawanyika. Utume wake ulikuwa ni kubomoa nguvu hii ya pepo na kuwaweka watu huru ili kumtangaza Mungu na ufalme wake. Katika Maandiko, Roho ya Mungu huonekana kama ile nguvu ya kimungu inayofanya kazi ndani ya uumbaji katika kuleta wokovu. Huyu Roho wa Mungu ndiyo nguvu ya wokovu inayounganisha Mungu na mtu wake. Mungu Baba hujenga familia yake.

Tunaendelea kuona kuwa Yesu anasema wazi kwamba dhambi husamehewa; hata dhidi yake – Mt. 12:32 – ‘Basi, mtu amtetaye Mwana wa Mtu atasamehewa, bali mtu amtetaye Roho Mtakatifu hatasamehewa, wala katika enzi hii wala katika enzi ijayo’ ila hakuna msamaha kwa kufuru dhidi ya Roho Mtakatifu. Aina hii ya dhambi dhidi ya Roho Mtakatifu ni kule kuukana huo uwepo wa Roho anayefanya huo wokovu upatikane, ni dhidi ya ile nguvu ya wokovu inayounganisha Mungu na mtu. Ni kule kukataa hata ile nia ya Mungu ya kuokoa. Ni kukaa nje ya huo mpango wa Mungu wa wokovu. Ni kukataa ile neema ya kupata nguvu ya kutubu dhambi. Tunaona katika somo la kwanza kuwa dhambi iliharibu kabisa uhusiano wetu wa kiroho na Mungu.

Uhusiano uliofungamanishwa na upendo na uaminifu. Tangu hapo mtu akaanza kumwonea aibu Mungu na kujificha, kukaa mbali. Akapoteza kabisa uhuru wake wa kuchagua na zaidi sana hata kushindwa kumchagua Mungu. Ndiyo maana katika somo la pili, Mtume Paulo anatukumbusha haja ya kuweka wazi tofauti kati ya mambo ya ulimwengu na yake Mungu. Sisi tuko ulimwenguni lakini si wa ulimwengu huu. Hatuna budi kumchagua roho wake Mungu ili tuweze kuyajua mambo yake Mungu na kumchagua yeye. Kwa hiyo, injili yote yaeleza taalimungu kamili juu ya familia ya kweli ya kikristo. Ni familia inayokubali mapenzi ya Mungu. Ni familia inayoishi na kupokea mapenzi ya Mungu. Ni familia iliyo wazi kwa Roho Mtakatifu na inayofanya mapenzi ya Mungu yawezekane. Mwaliko ni kufanya mapenzi ya Mungu. Yesu anasisitiza kuwa kinachounda uhusiano wa kweli kwake ni kufanya mapenzi ya Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

 
All the contents on this site are copyrighted ©.