2018-06-06 10:06:00

Makanisa Mahalia yanapaswa kuzingatia: Malezi makini na kujitegemea


Mwezi Oktoba 2019 kitakuwa ni kipindi “cha patashika nguo kuchanika”  kwa maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Ni wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, muda muafaka wa kupyaisha mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha, kielelezo cha imani tendaji. Kanisa linahitaji wongofu wa kimisionari ili kuweza kutekeleza vyema dhamana na utume wake duniani. Wakristo wanakumbushwa kwamba, wameteuliwa, wakabatizwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu; kumbe, wanashiriki: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo, daima wanapaswa kusoma alama za nyakati!

Itakumbukwa kwamba,  Mwezi Oktoba 2019, Kanisa litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Papa Benedikto XV alipochapisha Waraka wa Kitume "Maximum Illud" yaani “Kuhusu Shughuli za Kimisionari.” Ni muda wa: sala, katakesi, tafakari na matendo ya huruma! Haya yamesemwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za kimisionari. Lengo kuu ni kutaka kutangaza Injili, kuadhimisha Sakramenti na Wakristo kutoa ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.

Baba Mtakatifu anasema, matukio haya makuu mawili, yaliwezeshe Kanisa kuutaza Uso wa huruma ya Mungu, wakati wa kuyashughulia: matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika mchakato mzima wa uinjilishaji. Ni muda muafaka wa kujitosa bila kujibakiza kuhudumia Injili kwa ajili ya wokovu wa walimwengu; kwa kupambana kikamilifu na mambo yote yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Katika mkutano huu, Padre Tadeusz J. Nowak, OMI, Katiku mkuu wa muda wa Mashirika ya Kipapa ya Kazi za kimisionari amekazia umuhimu wa kuratibu shughuli mbali mbali za kimisionari katika Makanisa mahalia, kama utekelezaji wa wito wa uinjilishaji unaofanywa na Mama Kanisa. Dhamana hii inapaswa kusimikwa katika mchakato mzima wa ujenzi wa tasaufi kimisionari, kwa kujikita katika malezi na majiundo makini ya ari na moyo wa kimisionari kwa Makanisa mahalia. Kumbe, kuna haja ya kuwa makini sana na matumizi ya rasilimali fedha ya Kanisa inayopaswa kuelekezwa zaidi katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Ukomavu wa Makanisa mahalia unapimwa pia kwa kuanza kujitegemea: kiuchumi, kwani waamini wanapaswa kuhamasishwa kushiriki kikamilifu katika kuyategemeza Makanisa mahalia, ikikumbukwa kwamba, kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa, sadaka na mchango unaotolewa na familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, unaendelea kupungua kila mwaka. Inafurahisha kuona kwamba, hata familia ya Mungu Barani Afrika katika umaskini wake, imeanza kucharuka kuchangia katika mchakato wa kulitegemeza Kanisa Barani Afrika.

Padre Fernando Domingues, MCCJ, Katibu mkuu wa Mashirika ya Kipapa ya Mtakatifu Petro Mtume, “POSPA” anasema, Mwongozo wa Malezi ya Kipadre  unaojulikana kama “Ratio Fundamentalisi Institutionis Sacerdotalis”  yaani “Zawadi ya wito wa Kipadre” ni muhtasari wa mambo msingi yanayopaswa kuzingatiwa katika malezi na majiundo ya kipadre yanayopaswa kupyaishwa, kuendelezwa na kupewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Mama Kanisa kwa kusoma alama za nyakati. Mwongozo wa sasa unazingatia na kukidhi mahitaji msingi ya malezi na majiundo ya Kipadre ili kuweza kukabiliana na changamoto za ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni mwongozo unaotoa mwelekeo na uwiano sahihi wa malezi: kiutu, kiroho, kiakili na kichungaji kwa njia ya safari ya malezi na majiundo makini ya Kipadre, taratibu, lakini kila jandokasisi akiangaliwa kwa jicho la pekee.

Padre Fernando Domingues anakaza kusema, majiundo makini ya mapadre na watawa ni muhimu sana kwa Makanisa mahalia. Kumbe, kuna haja ya kuonesha moyo wa mshikamano na upendo, unaoongozwa na kanuni auni ili kusaidia malezi na majiundo ya mapadre na watawa kwenye Makanisa mahalia. Mabaraza la Maaskofu yanapaswa kuzingatia Mwongozo huu kwa kusoma alama za nyakati na kujibu mahitaji msingi, fursa na changamoto za shughuli za kichungaji.

Padre Fernando Domingues  anasema Katiba ya Kitume “Veritatis gaudium” yaani “Furaha ya ukweli” iliyoidhinishwa na Baba Mtakatifu Francisko tarehe 8 Desemba 2017 na kuchapishwa rasmi tarehe 29 Januari 2019 ni mwongozo makini unaovihusu vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu zinazomilikiwa na kuongozwa na Kanisa Katoliki, kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayowagusa na kuwaambata watu wa Mungu katika mwelekeo mzima wa utekelezaji wa utume wa uinjilishaji mpya. Hii ni dhamana inayojikita katika mang’amuzi, utakaso na mageuzi ya dhati yanayopania kupyaisha mfumo mzima wa elimu inayotolewa na Mama Kanisa katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.

Katiba hii ni mwongozo na mbinu mkakati katika mageuzi ya elimu inayopania kumpatia mwanadamu furaha ya ukweli katika maisha yake. Hii ni “Furaha ya ukweli” unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu ambaye ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu; ni njia, ukweli na uzima. Ni kiungo muhimu cha umoja katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na umoja kati ya watoto wa Mungu, kwani Roho Mtakatifu ni: Roho wa ukweli na upendo; uhuru, haki na umoja.

Kumbe, Mashirika ya Kipapa ya Mtakatifu Petro Mtume yataendelea kujikita katika: Malezi na majiundo makini ya walezi; kwa kutoa ruzuku kwa taasisi na seminari kuu sanjari na ulinzi kwa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia. Makanisa mahalia yanapaswa pia kuanza kuwa na mbinu mkakati wa kujitegemea walau katika mahitaji yake msingi, kuwashirikisha waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kuchangia katika malezi na majiundo ya kipadre na kitawa. Kuna matumaini makubwa kwamba, Seminari kwa siku za usoni zitaweza kutegemezwa zaidi na Makanisa mahalia, kama sehemu ya wajibu wa familia ya Mungu katika malezi na majiundo ya viongozi wao wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.