2018-06-05 09:29:00

Waziri mkuu wa Poland akutana na Papa Francisko mjini Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu, tarehe 4 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na Bwana Mateusz Morawiecki, Waziri mkuu wa Poland pamoja na msafara wake. Baadaye, amepata fursa ya kukutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wameridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili; sanjari na ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na Kanisa Katoliki nchini Poland katika utekelezaji wa huduma makini kwa familia ya Mungu nchini humo. Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mgeni wake, wamegusia tema mbali mbali ikiwa ni pamoja na sera na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; umuhimu wa kusimama kidete: kulinda, kutunza na kudumisha mazingira nyumba ya wote. Itakumbukwa kwamba, mji wa Katowice, Desemba 2018, utakuwa ni mwenyeji wa mkutano wa kimataifa kuhusu mazingira unaoandaliwa na Umoja wa Mataifa.

Viongozi hawa wameshirikishana pia masuala ya kimaadili na utu wema wakati wa mazungumzo yao. Mwishoni, wamejikita zaidi katika masuala changamani ya Bara la Ulaya na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kwa kufanya rejea hasa katika mchakato wa kukabiliana na wimbi kubwa na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya, hasa huduma kwa wakimbizi na wahamiani kutoka Ukraine na Mashariki ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.