2018-06-05 14:30:00

Watawa waadhimisha kilele cha kumbu kumbu ya miaka 170 ya utume!


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki, Jumapili tarehe 3 Juni 2018 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya kilele cha Jubilei ya miaka 170 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili la Watawa kutoka Armenia. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa la San Nicola da Tolentino, Jimbo kuu la Roma na kuhudhuriwa na viongozi kadhaa wa Makanisa ya Mashariki.

Kardinali Sandri katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa waamini kutekeleza Amri za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha yao hapa duniani. Mwenyezi Mungu anawataka binadamu kushiriki kikamilifu katika mpango wa Ukombozi.  Wakristo wakumbuke kwamba, wameteuliwa, wakaitwa na kutumwa kwenda sehemu mbali mbali za dunia kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto, waamini wajitahidi kumsaidia Kristo Yesu: kufahamika na kupendwa; kuabudiwa na kutolewa sadaka kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kardinali Sandri anamshukuru Mungu kwa uwepo na karama ya Shirika inayosimikwa katika ukarimu, elimu na malezi kwa vijana wa kizazi kipya. Katika kipindi chote hiki, watawa hawa wamekuwa ni mama na dada kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi. Watoto hawa walikuwa ni matunda ya madhara ya “Mauji ya Kimbari”, “Metz Yegern”. Watawa hawa kwa msaada wa Papa Pio XI kunako mwaka 1922 walifanikiwa kuokoa maisha ya watoto yatima kwa kushirikiana na Serikali ya Italia.

Shirika likalipa gharama kubwa kwa watawa wake 13 kuuwawa kikatili na wengine 26 kuhamishiwa uhamishoni. Kunako mwaka 1991 watawa hawa wakafungua nyumba huko nchini Armenia. Kardinali Sandri anasema, kwa njia ya utume wao kwa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, wamechukua ni chechemi ya furaha ya Injili inayobubujika kutoka katika elimu.

Watawa hawa wametakiwa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya upendo, unaobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Malezi na majiundo makini kwa vijana wa kizazi kipya yapewe umuhimu wa pekee, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoajiandaa kuadhimisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Muda wa maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Sinodi iwe ni fursa kwa vijana kutafuta na kuambaya furaha ya kweli; kulinda na kukuza uhuru unaowajibisha. Vijana wakubali kutikia miito mitakatifu katika maisha yao; wawe ni vyombo na mashuhuda wa: haki na amani dhidi ya ghasia, chuki, vita, dhuluma na nyanyaso. Kwa maombezi ya Mtakatifu Gregori wa Narek, Mwalimu wa Kanisa, Mwenyezi Mungu awakirimia amani, upendo na mshikamano wa dhati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.