2018-06-04 09:08:00

Papa Francisko: Ghasia Nicaragua: Dumisheni maisha na majadiliano


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili, tarehe 3 Juni 2018, ameungana na Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua ili kuonesha masikitiko yake kutokana na machafuko pamoja na ghasia zinazoendelea nchini humo ambazo tayari zimepelekea watu kadhaa kupoteza maisha yao na wengine wengi kujeruhiwa vibaya. Kikundi cha watu wenye silaha kinachounga mkono serikali iliyoko madarakani kimeamua kuanzisha mashambulizi ya silaha ili kupambana na raia wanaopinga mchakato wa mageuzi unaofanywa na serikali ya Nicaragua.

Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na mashambulizi haya. Anasema, Kanisa daima litaendelea kujikita katika mchakato wa majadiliano, yanayohitaji uwajibikaji unaomwilishwa katika matendo kwa kuheshimu uhuru wa watu, lakini zaidi kwa kuheshimu maisha ya watu! Baba Mtakatifu anaiombea nchi ya Nicaragua, ili iweze kusitisha ghasia na hatimaye, kuwa uhakika wa kuanza tena majadiliano katika ukweli na uwazi!

Tangu tarehe 18 Aprili 2018 kumekuwepo na maandamano makubwa ya kupinga mchakato wa mageuzi ya masuala ya pensheni kwa kupunguza kiasi cha asilimia 5%, mchakato ambao ulikuwa umeridhiwa na Rais Daniel Ortega wa Nicaragua. Baada ya mshike mshike na patashika nguo kuchanika, Rais Daniel Ortega, akanyoosha mikono juu na kuondoa muswada wa mageuzi! Lakini, wananchi wakaendeleza mapambano kwani walisema, Rais Daniel Ortega, ndiye aliyekuwa “mzigo kwa Serikali” baada ya kuongoza Nicaragua kwa muda wa miaka 30.

Wachunguzi wa mambo wanasema, hadi sasa kuna watu zaidi 100 wamefariki dunia baada ya vikosi vya ulinzi na usalama kuwarushia risasi za moto wananchi waliokuwa wanaandamana kudai haki zao pamoja na kumtaka Rais Daniel Ortega, kung’atuka kutoka madarakani haraka iwezekanavyo! Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu, likaamua kuingilia kati ili kuanzisha mchakato wa majadiliano kati ya Serikali na raia wake, ombi lililokuwa limetolewa na Rais Daniel Ortega. Lakini kwa sasa, Rais Ortega amefutilia mbali mchakato wa majadiliano na kwamba, kwa sasa ameamua “kutembeza mkong’oto”.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nicaragua katika tamko lake, linasikitika na kulaani mashambulizi dhidi ya raia na kwamba, hivi ni vitendo vinavyokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu. Maaskofu wanakaza kusema, raia wanao uhuru wa kuandamana kikatiba, lakini Serikali imeamua kuwashughulikia bila huruma, kiasi hata cha kuwafutilia mbali kutoka katika uso wa dunia. Wakati huo huo, habari kutoka Vatican zinasema kwamba, Askofu mkuu Waldemar Stanislaw Sommertag, Balozi wa Vatican nchini Nicaragua, Jumamosi, tarehe 2 Juni 2018 amekutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu yale yanayojiri huko Nicaragua.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.