2018-06-04 10:44:00

Maria na Consalata pacha wamerudi kwa Bwana baada ya ushuhuda!


Maria na Consolata, pacha waliozaliwa wakiwa wameungana nchini Tanzania na wakaishi hadi kujiunga na chuo kikuu wakiwa bado wameungana, wamefariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 3 Juni 2018. Pacha hao walifariki dunia wakiwa katika hospitali ya Iringa, ambapo kifo chao kimewagusa watu wengi Tanzania, kiasi kwamba walio wengi wametuma  salamu zao za rambirambi kupitia mitandao ya kijamii, maana mapacha hao walikuwa wamejulikana sana na hasa kwa ajili ya imani, akili busara, ucheshi, ujasiri na uvumulivu. Walikuwa kweli wamejazwa na nguvu ya Roho Mtakatifu, na wameacha uzoefu na mfano wa kuigwa hasa kwa wale walikaa nao kwa karibu.

Kufuatia kifo cha mapacha hao, hata Rais wa Tanzania Bwana John Magufuli, ambaye miezi kadha alikutana na pacha hao,wakiwa hospitali ya Taifa Dar Es Salam  ameeleza kusikitishwa kwake na vifo vyao katika ujumbe wake kwenye Twiter: "Nimesikitishwa na kifo cha Maria na Consolata. Nilipokwenda hospitali waliliombea taifa. Walikuwa na ndoto ya kulitumikia taifa. Poleni familia, Masista wa Maria Consolata na wote walioguswa, pumzikeni mahali pema wanangu. BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA JINA LA BWANA LIHIMIDIWE”. Mwaka 2017, walijiunga na Chuo Kikuu Katoliki  cha Ruaha (RUCU) na kuanza masomo ya kompyuta kabla ya kuanza masomo kamili Oktoba, kwa maana  Maria na Consolata walikuwa wamefanya mitihani yao ya mwisho ya kidato cha sita, katika shule ya Sekondari ya Udzungwa mjini Iringa, Kusini magharibi mwa Tanzania na kufaulu vizuri!

Maisha ya Maria na Consolata...
Maria na Consolata Mwakikuti walizaliwa eneo la Ikonda, wilaya ya Makete kusini magharibi mwa Tanzania mwaka 1996. Kwa maana hiyo walikuwa na umri wa miaka 22 na  wamekuwa wakitunzwa na watawa wa Kanisa Katoliki,  tangu na baada ya kuzaliwa tu. Walisoma shule ya msingi ya Ikonda kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Maria Consolata na baadaye wakasomea hadi kidato cha sita katika shule ya Udzungwa wilaya ya Kilolo. Septemba 2017, baada ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita, walijiunga na Chuo Kikuu Katoliki cha Ruaha, Iringa. Lakini wakati huohuo walianza kuugua maradhi ya moyo na Desemba wakahamishiwa taasisi ya maradhi ya moyo ya Jakaya Kikwete katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam ambako walilazwa kwa miezi miwili. Hata baada ya kutoka hospitali hiyo afya yao iliendelea kuwasumbua.

Maria na Consolata mara baada ya kufaulu mtihani wa kidato cha sita, walieleza furaha yao kuu na hata kulezea ndoto zao za baadaye kwamba walipokea matokeo yao wakiwa kwenye mazingira ya nyumbani kwao, wakiendelea na shughuli zao za kila siku, na kuambiwa kuwa matokeo yametoka na wamefanya vizuri. Ndiyo walikuwa wakiwaza kabla ya hapo kwa maana katika mitihani huwezi kujua na kujiamini sana. Aldha walieleza hata sababu za kuchagua chuo cha Ruaha kwenye mkoa walio kuwa wanaishi tofauti na vyuo vingine au kama ilivyo kwa wanafunzi wengine ambao hupenda kubadili mazingira. Walipenda kwa sababu walipenda mazingira ya Iringa, hawakutaka kwenda Dar es Salaam kwa sababu walipenda kuishi pamoja na walezi wao, Masista waliokuwa wanawalea tangu wakiwa wadogo pili mikoa mingine ilikuwa mbali na wanapoishi na tatu, hali yao ilivyo  isingeweza kumudu kuishi katika mazingira ya joto kwa maana mji wa wa Iringa ni baridi kwa asili na ambao wamezaliwa na kuzoea.

Kuhusu kujiunga na Chuo Kikuu
Walikuwa wamewasili mapema Chuo Kikuu cha Kanisa Katoliki Ruaha (RUCU) kujiandaa na masomo yao ya shahada ya elimu, na siku ya kwanza kufika chuo kikuu walifurahi sana na kuushukuru uongozi wa chuo na wanafunzi kwa kuwapokea kwa furaha na kuwaandalia mazingira mazuri ya kusomea na kuishi. Aidha walifika mapema kwa sababu, walitaka kujifunza kompyuta ili waendane na kasi ya wanafunzi wengine. Kwa mujibu wa pacha hao, walikuwa wamesema kuwa ndoto yao ya kufika chuo kikuu imetimia, hivyo walishukuru shirika la wamisionari la masista wa Consolata kwa kuwalea na kuwapa moyo. Pia walikuwa wamewashukuru wafadhili waliojitolea kuwalea mpaka walipofikia.

Hata hivyo ushuhuda wa Mtawa Jane Lugi  kutoka shirika la wakonsolata aliyekuwa amewasindikiza siku hiyo alithibitisha kuwa, wamewawahisha chuoni ili wajifunze kompyuta iwasaidie katika masomo yao na kwamba, waliwatunza wakiwa Kilolo, na kwa maana hiyo katika Chuo kikuu waweza kutunzwa  na masista wa Mtakatifu Teresa ambao wamewaandalia mazingira mazuri ya kuishi kama walivyoomba. Kwa maana hiyo mtawa huyo alithibitisha kuridhika na kuwatakia kila la heri kwa  kuahidi kuwatembelea mara kwa mara.

Kwa upande wa mapacha hao na msimamo wao: Maria na Consolata walikuwa wamewahimiza wazazi kuwajibika ipasavyo kwa watoto wao wenye ulemavu wakisema kwamba hakuna lisilowezekana. Katika maneno yao walisema: “Wazazi washukuru Mungu kupata watoto wenye changamoto kama wao wasione kuwa na mtoto mlemavu ni laana. Pili wawaone kama watoto wengine na kuwapa mahitaji yao ya msingi, wawawezeshe, wawapatie nafasi ya kujiendeleza maana wakiwezeshwa wana nafasi kubwa ya kufanya vizuri”.

Kwa hakika Jamii ya Mkoa wa Iringa na taifa la Tanzania kwa ujumla  wamepoteza tunu hii, lakini wakati huohuo wao sasa ni  mbegu bora  iliyopandwa katika ardhi ya mkoa huo na taifa zima... , mbegu hiyo itaendelea   kukua katika jamii nyingi hasa  kwa kujifunza na kuiga ujasiri, imani uvumilivu upendo kwa kila mmoja; kuwa watu wa sala, wanaosadiki na kuamini, kwa mfano wa mapacha mashujaa hao ambao wamethibisha hayo kuwa hakuna lisilo wezekana , kama vile pia Yesu asemavyo " Mbegu isipopandwa ardhini haiwezi kuota na kuzaa matunda yanayokusudiwa";wao sasa ni mbegu na mfano wa kuigwa, maana hiyo hatunabudi  kuwaombea kwa Mungu awapokee katika mikono yake mitakatifu na kuwapumzisha kwa amani.

Raha ya Milele uwape e Bwana Maria na Consolata na mwanga wa Milele uwaangazie, wapumzike kwa amani Amina

Na Sr Angela Rwezaula 
Vatican News

 
All the contents on this site are copyrighted ©.