2018-06-02 13:00:00

Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu iwe ni chemchemi ya utakatifu


Tume ya Kipapa ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa ilianzishwa rasmi na Papa Leo XIII kunako mwaka 1876 ili kusaidia mchakato wa kumwezesha Kristo Yesu: kufahamika, kupendwa na kutumikiwa kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kongamano la 52 la Ekaristi Takatifu Kimataifa litaadhimishwa huko Budapest, nchini Hungaria kuanzia tarehe13-20 Septemba, 2020 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Visima vyangu vyote vimo kwako”. Zab. 87:7.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kufunga Kongamano la 51 la Ekaristi Takatifu huko nchini Ufilippini aliwatakia wajumbe wote imani thabiti na upendo kwa Kristo anayeendelea kuwepo katika Ekaristi Takatifu, ili kweli waweze kuwa ni Wamissionari na wafuasi amini wa Kristo; kwa kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa sanjari na kuendeleza ari na mwamko wa kimisionari katika Makanisa mahalia. Ekaristi Takatifu iwe ni chachu ya upatanisho na amani duniani kote. Ekaristi Takatifu iwe ni shule ya huduma ya unyenyekevu, tayari kujisadaka kwa ajili ya wengine; kiini cha umisionari na ufuasi wa Kristo.

Waamini wawe mstari wa mbele kuonesha mshikamano, upendo na wema; wapanie daima kujenga maisha yao, kielelezo cha nguvu ya Ekaristi Takatifu inayopyaisha maisha na kubadili mioyo ya waamini, tayari kuwahudumia na kuwalinda maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kuwa wakamiliifu kama baba yao wa mbinguni alivyo mkamilifu kwa kupinga ukosefu wa haki, rushwa na ufisadi; mambo yanayovuruga umoja, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu iwasaidie waamini kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; mahali pa katekesi endelevu katika maisha ya kiroho,  kama ilivyokuwa kwa wale wanafunzi wa Emau, waliobahatika kufafanuliwa Maandiko Matakatifu na hatimaye, wakamtambua Kristo Yesu kwa kuumega Mkate. Mama Kanisa anatukumbusha kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Sadaka; Shukrani na masifu kwa Mungu Baba; Ni kumbu kumbu ya sadaka ya Kristo na ya Mwili wake; Kanisa ni kielelezo cha uwepo wa Kristo kwa nguvu ya Neno na Roho wake Mtakatifu.

Ekaristi Takatifu ni Fumbo la Imani na kutokana na ukuu wake, tunaweza kuthubu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Thoma, Bwana wangu na Mungu wangu! Kongamano hili litafanyika Barani Ulaya, ambako katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, familia ya Mungu imeguswa na kutikiswa katika misingi yake ya imani, maadili na utu wema. Kanisa linataka kuwa kweli ni chombo cha haki, amani, umoja na mshikamano. Maadhimisho haya yawe ni chachu ya kupyaisha maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Ekaristi Takatifu ni kumbu kumbu endelevu ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, changamoto na mwaliko kwa waamini kuifia dhambi na kuanza kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha.

Padre Jànos Brenner, Shahidi wa Ekaristi Takatifu, alipewa Daraja Takatifu ya Upadre kunako mwaka 1955, anakumbukwa sana kwa ushuhuda wa maisha na utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya; alikuwa amejanga sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa makini. Aliuwawa kikatili na utawala wa Kikomunisti hapo tarehe 15 Desemba 1957, wakati akiwa analinda Ekaristi Takatifu na sasa Kanisa limetambua utakatifu wake kama “Shahidi wa Ekaristi Takatifu.” Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga pamoja naye katika sala, ili kuombea maandalizi na hatimaye mafanikio katika maadhimisho ya Kongamano hilo.

Kardinali Peter Erdo’ Erdo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Esztergom-Budapest, Hungaria anasema, kwa mara ya kwanza, Hungaria ilikuwa mwenyeji wa Kongamano la Ekaristi Takatifu kunako mwaka 1938. Anasema, maadhimisho ya Makongamano ya Ekaristi Takatifu Kimataifa yanaanza kuwa na mwelekeo mpana zaidi kwa kugusa uhalisia wa maisha ya watu ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu ya kukuza na kudumisha umoja, udugu na mshikamano kati ya waamini, kwa kuwa na jicho la upendo kwa walemavu ndani ya jamii. Ekaristi Takatifu ni chachu makini ya Injili ya familia inayokumbatia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Ekaristi Takatifu, inalisukuma Kanisa kutembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya utume wa vijana, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Umuhimu wa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kitamaduni ili kukoleza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Kumbe, maadhimisho ya Makongamano la Ekaristi Takatifu katika ngazi mbali mbali ni fursa makini inayopania kupyaisha imani inayomwilishwa katika maisha ya watu, kielelezo makini cha imani tendaji.

Itakumbukwa kwamba, hata Familia ya Mungu nchini Tanzania na hasa  kutoka katika Majimbo yanayounda Jimbo kuu la Tabora, Kanda ya Magharibi mwa Tanzania, nayo inajiandaa kwa ajili ya maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa yatakayozinduliwa rasmi tarehe 30 Juni 2020 Jimbo kuu la Tabora.  Askofu mkuu Paulo Ruzoka anasema, hii ni dhamana na wajibu mkubwa, unaohitaji moyo wa umoja na mshikamano, kwani maadhimisho haya yatakuwa ni alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu baada ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, ambayo kilele chake ni hapo Jumapili 7 Oktoba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu "Miaka 150 ya Uinjilishaji, Furaha ya Injili".

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 
All the contents on this site are copyrighted ©.